MWONGOZO WA UINJILISTI WA NYUMBA KWA NYUMBA.
Advertisements
YALIYOMO:
01.NINI MAANA YA UINJILISTI.
02.AINA ZA UINJILISTI.
03.NAMNA YA KUINJILISHA NYUMBA KWA NYUMBA.
04.CHANGAMOTO KATIKA USHUHUDIAJI.
05.MASWALI CHOCHEZI.
06.KUUNDA VIONGOZI WA IDARA YA USHUHUDIAJI.
07.MISINGI YA KANISA LETU LA BEROYA BIBLE FELLOWSHIP CHURCH.
08. MASOMO MUHIMU YA KUFUNDISHA WAKATI WA KUSHUHUDIA.
09.MATUMIZI YA LUGHA NA SAUTI.
(Kwa ufupi)
01.NINI MAANA YA UINJILISTI WA NYUMBA KWA NYUMBA.
Uinjilisti wa nyumba kwa nyumba hujulikana kwa jina la “ ushuhudiaji” Neno hili linana maana kutangaza mambo yote ya kushangaza aliyokutendea Bwana. Kueleza namna ambavyo Bwana alivyokutembelea/alivyowatembelea,kueleza matendo makuu ya Mungu.Kushuhudia kuzuri ni kule kueleza hasa uzuri wa Mungu maishani mwako sawa sawa na neno la Mungu. Shuhuda zikae katika mpangilio wa neno la Mungu isiwe katika hali ya kujiinua. Hivyo basi tunashuhudia kwa sababu:
Kufuata kielelezo chake Bwana Yesu,kwa kuwa Yeye ndie mwanzilishi kushuhudia ( Luka 19:5-6, Luka 10:38-42,Mathayo 8:14. -Na mfano mwingine kwa Stephano Matendo 8:27-35,N.K)
Ni sehemu ya agizo kuu ( Mathayo 28:19)
Kuzivuna roho za watu waliopotea.
Kulitambulisha kanisa,ili watu wakapate mahali sahihi pa kuabudu.
Kuleta faraja ndani ya mioyo iliyoumizwa.
02.AINA ZA UINJILISTI/USHUHUDIAJI.
Zipo aina mbili kubwa za ushuhudiaji;
Nyumba kwa nyumba.
Kushuhudia nje ( barabarani,mtaani,sokoni,stendi ya bus,hospitalini. N.K)
KUMBUKA ; ( Uinjilisti wa jukwaani hujatajwa kwa kuwa wenyewe unajitegemea. Kumbuka tunaangalia uinjilisti haswa wa nyumba kwa nyumba)
I. Uinjilisti/ushuhudiaji wa nyumba kwa nyumba.
Ni aina ya ushuhudiaji ambao unatumika sana kuokoa roho za watu na kuwaelekeza mahali sahihi pa kuabudu. Madhumuni makubwa ya ushuhudiaji wa namna hii ni kuwafungua watu waliofungwa katika vifungo vya magonjwa,vifungo vya dini na kuwaelekeza mahali sahihi pa kuabudu. Kwa maana uinjilisti wa nyumba kwa nyumba unatoa fursa ya kipekee ya kuonana na mtu binafsi na kujua hasa ni eneo gani mtu huyo amekwama,na kwa jinsi gani waweza kumsaidia.
Mfano: Yesu naye aliinjilisha Luka 4:38-39
“Akatoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake.Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia.”
Wengine wanakuwa hawajui wafanyeje,wapo njia panda,wakihitaji mtu mmoja (mshuhudiaji) aje amkwamue kwa neno la Mungu lililo sahihi. Kwa sababu kuna watu majumbani hawahitaji vitu vingi bali wanahitaji ushauri wa kiimani tu waweze kuendelea.Ushuhudiaji wa nyumba kwa nyumba hauchagui nyumba za kushuhudia,bali unafanyika nyumba hadi nyumba sawa sawa na uchaguzi au mwongozo wa Roho mtakatifu. Kwa maana mshuhudiaji aweza kuzuiliwa na Roho kwamba nyumba fulani asiingie na Roho akampa ruhusa kuingia nyumba nyingine,kama vile Paulo alivyozuiliwa kushuhudia neno huko Asia kipindi walipotoka katika nchi ya Frigia na Galatia (Matendo 16:6)
Je ushuhudiaji unatakiwa kufanyika katika nyumba za wasioamini tu?
Ushuhudiaji unatakiwa kufanyika katika nyumba za wasioamini na nyumba za wanaoamini. Hakuna uchaguzi kwa kigezo cha kutokuamini kwao au kuamini kwao kwa sababu kitendo cha kushuhudia kikifanyika katika nyumba ya wasioamini kitaleta matunda na kuwafanya wamuamini Yesu,alikadhalika ushuhudiaji ukifanyika kwa waaminio kutaleta badiliko kwao waaminio wapokee kitu kipya kwa kuwa neno la Bwana li jipya kila siku iitwapo leo. Wapo waaminio wanaamini lakini hawana bidii katika maarifa ya Ki-Mungu,watu hawa wakiinjilishwa waweza kubadili kuamini kwao kwa kawaida na kuanza kuijua kweli,pia waweza kujua kanisa sahihi la kuabudu.
03.NAMNA YA KUSHUHUDIA.
Awali ya yote yapasa kufahamu kwamba kila mtu aliyeokoka afanyike shuhuda mahali alipo. Zifuatazo ni njia au namna mshuhudiaji atakavyoanza na kumaliza kazi yake.
Salimia na kujitambulisha. Mfano “ Bwana Yesu asifiwe… mmeshindaje wapendwa wa Mungu…,mimi/sisi ni watumishi -taja majina yako na unatoka wapi ukiwa umetulia vizuri, waweza kumuuliza pia jina lake kama akipenda kukuambia) Eleza Wp mpo
Eleza lengo lako. Mfano “ nimefurahi kuingia hapa,ni mahali pazuri,..basi nimekuja kuwashirikisha ujumbe mfupi wa Neno la Mungu….pia niweze kuomba na wewe….“
Omba kidogo ili ukabidhi eneo hilo mahali ulipo,pia omba kwamba ujumbe uliokuja nao ukapate kueleweka. (Maombi yatawaliwe na hekima ya Bwana,yasiwe marefu sana wala yasiwe mafupi sana. Omba kutoka rohoni katika uzuri na utaratibu)
Muulize kama hajaelewa mahali,au kama kuna mahali ambapo anaona kuna wasi wasi bado.
Eleza kiini cha ujumbe wako kwa ufupi kusiwepo na maneno mengi. Utumie biblia yako,pangilia maneno yako yawe machache yenye kukolea munyu.
Mtie moyo kwa kile ulichokihubiri. Mfano “ Mungu amesikia kilio chako,leo amekusudia kukuondolea hili teso,na usiwe na wasi wasi wewe ni mtu wake, Mungu wala hajakuacha…”
Mpe mwaliko wa kumpokea Yesu. Na umuongoze sala ya toba kisha umuombee tena ikiwa kama atakubali. La! Kama atakataa kumpokea Yesu basi usimuache vivyo hivyo waweza ukamkirisha sala ya imani kwa hekima kama sehemu ya maombi ya kawaida.
Msaidie katika swali,au hoja,au mashaka aliyokuwa nayo-ikiwa kama atakuuliza. Nawe mjibu kwa ufupi kwa kuchagua maneno ya kujibu.
Mualike katika ibada zenu na kumpa kipeperushi chenye kuonesha ratiba za ibada zenu.
Mpe kitabu cha hongera kwa kuokoka ikiwa kama kipo.
Mfunike kwa damu ya Yesu yeye na familia yake.
Urudipo kanisani,chukua hatua ya kumuombea tena huko huko aliko.
KUMBUKA MAMBO YAFUATAYO KUYAFANYA KABLA YA UINJILISTI.
Kumshukuru Bwana Mungu kwa kibali cha uinjilisti katika nyumba mnazoziendea.
Kujiandaa kwa maombi kwa kuomba neema ya kupokelewa katika nyumba hizo muziendeazo. Na maombi yote yafanyike,mfano maombi ya kuliteka anga za nyumba hizo.
Hakikisha unajipanga katika neno,namna ya kuanza na namna ya kumaliza. Katika hili muombe Roho mtakatifu aende nawe katika safari hiyo.
ANGALIZO WAKATI WA KUSHUHUDIA.
Zima simu zako kumruhusu Roho awe na nafasi.
Kuwa smart.
Ikiwa kama mpo wawili au zaidi,basi mnie mamoja na awe muongeaji mmoja kwa niaba ya wengine. Ikiwa mwingine anahitaji kunena basi mwingine na anyamaze ili muweze kusikilizana.
Msilinene vibaya kanisa,wala msinene vibaya mchungaji wenu kusudi watu wa nyumba wasije wakasikia wakawadharau au kuwakataa ninyi pale mnenapo.
Acha mizaha.
Ulenge kwenye kusudi isiwe unafika nyumba fulani basi badala ya kushuhudia unataka maji ya kunywa,au chakula,au unabweteka kwa mazingira( labda mazingira ni mazuri kisha waanza kumuomba mwenyeji akuwashie TV kidogo umalizie mpira unaoendelea katika TV N.K)
Usipendelee kwa kumuona mtu mazingira ya nje.
Usioneshe utofauti wa imani yako kwa kuwakashifu. N.K
HAKIKISHA:
Unawafuatilia wale wote uliowatembelea ( Wale waliokoka na hata wale wasiokoka.
A.CHANGAMOTO KATIKA USHUHUDIAJI.
Zipo changamoto nyingi katika kazi ya ushuhudiaji,baadhi ya changamoto hazina budi kuwepo kwa maana hazikwepeki,bali Roho mtakatifu umuwezesha mshuhudiaji kuzishughulikia na kusonga mbele. Zipo aina mbili za changamoto katika ushuhudiaji wa nyumba kwa nyumba nazo ni;
I)Changamoto upande wa washuhudiaji wenyewe.
II)Changamoto upande wa eneo la kushuhudia ( Nyumbani)
I).Changamoto za upande wa mshuhudiaji.
Kushindwa kujieleza vizuri. ( Mara nyingi ukianza vibaya katika kujieleza basi kunakufanya kupoteza lengo kamili la ushuhudiaji. Wengi hujikwaa kwa hofu namna ya kuanza)
Kuwa na neno la Mungu katika kiwango hafifu hususani pale unapokutana na maswali ya kujieleza ( Changamoto hii humsababisha mlengwa anayeshuhudiwa kukaa njia panda bila kuelewa akufuate huko kiimani au abakie pale pale alipo na imani yake.)
Maandalizi hafifu ya mshuhudiaji ( Changamoto hii imeonekana kwa baadhi ya washuhudiaji,pale wanapokuwa hawajajiandaa na kujipanga vizuri husababisha kukosa matokeo ya uvunaji mzuri. Maana hata mvuvi wa samaki sharti aandae vizuri nyavu zake,ajue majira mazuri ya upatikanaji wa samaki,ajue ni wapi alivua jana na wapi hajavua.N.K)
Kukosa upendo baina ya washuhudiaji. ( Ikiwa washuhudiaji wa siku wakikosa upendo basi hawawezi kutembea pamoja kwa maana watu wawili hawawezi kutembea pamoja wasipopatana Amosi 3:3-“ Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana? ” )
II.Changamoto upande wa eneo la kushuhudia.
Awali ya yote hatuna budi kuyajua makundi ya watu waliopo majumbani,pale tunapoenda kushuhudia. Kuna watu wa namna tofauti tofauti katika nyumba zanazokusudiwa kushuhudiwa. Utofauti huu wa watu upo katika Umri,ufahamu na akili,afya,itikadi za kidini na kiimani,makabila,rangi,jinsia,uwezo wa kiuchumi.N.K
Katika utofauti huo,basi ni vyema tukaangalia mgawanyo wa kiimani wa watu wote hao ambao hatuna budi kukutana nao majumbani tuendako. Mgawanyo wa makundi hayo ni kama ifuatavyo;
Wasioamini lakini ni wakristo wenye misingi ya sheria za dini zao.
Wasioamini kabisa ( Watu wenye imani nyingine mbali na ukristo)
Wanaoamini lakini wapo katika misingi ya manabii wa uongo.
Wanaoamini katika njia iliyo sawa na wewe mshuhudiaji.
Changamoto kubwa mbili zifuatazo zinaonekana sana katika eneo la ushuhudiaji kupitia makundi hayo ya watu.
Kushindwa kupokelewa. ( Baadhi ya watu majumbani hukataa kusikia kabisa,tena wengine kukejeri kwa maneno ya mizaha)
Kuulizwa maswali ( Makundi ya watu waliotajwa hapo juu yamejawa na maswali mengi kuhusu imani yako wewe mshuhudiaji. Wengine wanauliza kwa sababu hawajui,wengine wanauliza wanajua lakini wanataka kujua zaidi kwa nia nzuri,wengine wanauliza wakijua sivyo ndivyo lakini wakitaka kukupima utasemaje katika maswali hayo,watu hawa ndio wabishi sana kwa sababu lengo lao la kuuliza sio kujua bali ni kukupima imani yako~ Mfano mtu anakuuliza wapi palipoandikwa kwamba biblia ni neno la Mungu? )
B.MASWALI CHOCHEZI.
“ Maswali chochezi ” ni aina ya hoja zinazoibuliwa na watu huko majumbani. Ni aina ya maswali yanayoulizwa kuhusu imani ya kweli kushindana na imani ambayo si ya kweli. Mara nyingi maswali ya namna hii yana lengo baya la kumpima mshuhudiaji. Jambo hili tunaliona likitokea mara nyingi kwa Yesu mwenyewe kukutana na maswali ya kumpima kwamba atasemaje hali yeye aliyeuliza anaweza akawa anajua jibu lake. Mfano Yesu alipoingia Kapernaumu,wale watozao nusu shekeli walimuuliza juu ya kulipa kodi,hali wakijua kulipa kodi ni lazima sawa sawa na sheria ya nchi husika. ( Mathayo 17:24-27). Au mtazame pia Paulo alipowashuhudia watu wa Korintho,lakini hawakutaka kukubali ukweli hali wakiyajua mambo hayo ( Matendo 18 :4,5-6).
Hivyo basi kila mshuhudiaji anapaswa kujua namna ya kujibu maswali ya namni hii katika hekima yote pasipo kupaniki. Yafuatayo ni baadhi ya maswali au hoja zinazoulizwa sana kwa washuhudiaji pale wawapo nyumbani kwa watu wanaoshuhudiwa,maswali kama;
Je Yesu ni Mungu? Imeandikwa wapi?
Waberoya nini maana yake? Misingi yenu ya kanisa ipo wapi? Je ninyi ni wapentekoste? Au TAG,au EAGT mpo wapi haswa
Kuokoka ni nini maana yake?
Hoja juu ya ubatizo wa maji mengi.
Hoja juu ya udhihirisho wa Roho mtakatifu. Kwanza ni nani huyo Roho mtakatifu?
Suala la kuwa mtoto wa Mungu na kuwa mwana wa Mungu.
Suala la kula vyakula wanavyoviita najisi.
Maswala ya ndoa na mahusiano.
Dhambi ni nini? (Maswala ya makosa na msamaha)
N.K
Hivyo,ni lazima uwe na majibu sahihi kwa ufupi juu ya maswali kama hayo ambayo yaweza kuulizwa au kuombwa maelezo kutoka kwako mshuhudiaji. Ikiwa kama utaulizwa moja wapo la swali basi,jitahidi kujibu kwa ufupi sawa sawa na biblia isemavyo. Lah! Ikiwa hulijui jibu lake au ikiwa una wasi wasi basi mpe nafasi mwenzako ajibu. Na ikiwa mwenzako naye hajui na ikawa nyote hamjui basi tumieni hekima ya kumwambia mtarudi tena kesho au siku nyingine kujibu hizo hoja zao.
C.UONGOZI IDARA YA UINJILISTI.
IIfahamike kwamba umoja huu wa watu washuhudiao yafaa kuwa ni idara kamili ya ushuhudiaji inayojitegemea. Na kwa kuwa jambo lolote ili liweze kwenda vizuri katika mpangilio unaofaa linahitaji uongozi vivyo hivyo ushuhudiaji unahitaji viongozi watakao ongoza kundi kiroho na kiutendaji wakianzia hapa makao makuu yaani kanisani mpaka majumbani katika ushuhudiaji.
Lengo kubwa la viongozi wa ushuhudiaji ni kuliongoza kundi kiroho na kiutendaji sawa sawa na maono ya kanisa. Kwa kuwa itakuwa ni idara inayojitegemea,basi yafaa kuwe na viongozi wafuatao;
Mchungaji/Wachungaji.
Mwenyekiti
Katibu
Mwekahazina
Wajumbe watatu
Kazi ya kila kiongozi ni kama ifuatavyo;
a) Mchungaji.
Kusimamia shughuli nzima katika kushauri na kujibu maswali yote yanayohusu ushuhudiaji.
>Kufundisha washuhudiaji wawe kiroho zaidi.
>Aweza kuidhinisha eneo la kushuhudia akipata kibali cha baba apostle.
>Kuhakikisha roho za wongofu zinakabidhiwa kwa Apostle kwa ajili ya kuanza mara moja mafundisho ya kuukulia wokovu.
b) Mwenyekiti.
>Kupanga eneo la kushuhudia. (Lisiwe mbali sana na kanisa letu)
>Ni mwenyekiti wa vikao vyote vya ushuhudiaji.
>Kusimamia utekelezaji wa kuzifuata roho za watu zilizookolewa kipindi cha ushuhudiaji.
>Kutoa maelekezo sahihi ya mtaa husika kwa washuhudiaji wote kwa msaada wa mwenyeji wa eneo hilo,au kwa msaada wa mtu yeyote apajuaye vizuri.
>Kupokea taharifa muhimu kutoka kwa mchungaji au kutoka kwa apostle na kuwasilisha katika idara ya ushuhudiaji.
>Kubeba nembo na taswira halisi ya Beroya ndani na nje ya kanisa.( Awe kielelezo kizuri)
c) Katibu.
>Kuandaa vikao mbali mbali vya uinjilisti kwa idhini ya mwenyekiti.
>Kutunza kumbu kumbu za watu waliookoka pamoja na mawasiliano yao ya simu.
>Kuandaa minutes,agenda na kusoma katika vikao.
d) Mwekahazina.
>Kutunza pesa za uinjilisti katika mpangilio mzuri.
>Kutunza mapato na matumizi ya kifedha katika idara ya ushuhudiaji.
>Kutoa taharifa za mapato na matumizi.
>Kutoa pesa ya kutengeneza vipeperushi,au vijitabu vya hongera ya kuokoka.
>Kuwasilisha katika uongozi makusanyo yote ya sadaka yatakayopatikana wakati wa kushuhudia.
e) Wajumbe watatu.
>Watafanya kazi yoyote watakayopangiwa na viongozi wao.
NB.: Mchungaji aweza kuwa kiongozi wa nidhamu katika idara hii ya ushuhudiaji.
01.MSINGI WA KANISA ( BEROYA BIBLE FELLOWSHIP CHURCH )
Yafaa kufahamu msingi wa kanisa ili ikusaidie katika maelezo yako. Usipofahamu msingi wa kanisa la BBFC itakupa shida katika maelezo yako haswa pale utakapokuwa umeulizwa kwamba “ninyi mpo katika misingi gani?” Hivyo basi ni vyema ujue BBFC ni kanisa la namna gani.
Kanisa la Beroya bible fellowship ni kanisa la kipekee lenye huduma ya neno la Mungu katika uweza na nguvu za Roho mtakatifu. Jina la kanisa letu limetokana na watu waliokuwa waaungwana,wenye kulichunguza na kulitafakari neno la Mungu kila siku kwa uelekevu wa moyo na katika hekima yote kuona jinsi neno hilo lilivyo. Watu hawa walikuwa wakiishi Beroya ambao ulikuwa ni mji wa Makedonia uliopakana na Thesalonike mahali ambapo Paulo na Sila waliingia hapo na kuhubiri neno la Mungu. Soma MATENDO 17:10-11
Hivyo kanisa linaongozwa na Roho mtakatifu chini ya uongozi wa mtumishi wake Apostle Joe Mzuanda pamoja na mama Mzuanda. Kanisa letu lipo Kimara baruti tunapakana/nyuma ya PUMA petrol station (zamani bahama mama club).
Hivyo kila mshuhudiaji ni lazima ajue habari sahihi za kanisa lake,ajue pamoja na ratiba za kanisa.
02.MASOMO MUHIMU YA KUFUNDISHA KATIKA USHUHUDIAJI.
Yafuatayo ni baadhi ya masomo muhimu sana wakati wa ushuhudiaji sawa sawa na mkazo wa neno la Mungu linalohubiriwa hapa Beroya bible fellowship church;
Jinsi ya mkristo anapatikanaje.( Ukianzia uumbaji wa mwanadamu)
Kuokoka hasa ni nini? ( Tofauti ya dini na wokovu)
Kumuamini Mungu na kumtegemea katika hali yake yote.
Kuokoka na ushindi wa milele wa mwamini.
Urejesho wa ushirika kati ya mwamini na Mungu.
Ninawezaje kuwa mtakatifu?
Upendo wa Mungu juu ya maisha yetu na maisha ya msamaha ( Vile Mungu alivyotufia msalabani,akapigwa kwa ajili yako,na kwa kupigwa kwake umepona)
Thamani ya neno la Mungu.
Kuhesabiwa haki bure ( Hujakataliwa,)
Jinsi ya kuishi kiimani. ( Ushindi juu ya maisha ya kumtegemea Mungu)
Uponyaji ndani ya Jina na damu ya Yesu.
N.k
ZINGATIA:
Kila mshuhudiaji ni lazima aijue sala ya toba. Jifunze hapa kwa mfano huu ; ( utamuongoza sala ya toba kwa mfano wa sala hii)
“ Baba ninakushukuru kwa ajili ya siku hii ya leo,kwa maana u mwema katika maisha yangu,na sasa ninakata shauri kuachana na maisha ya dhambi, nanaamua kukufuata Mungu katika njia zako zote,futa jina langu katika kitabu cha hukumu,andika jina langu katika kitabu cha uzima,ninamkataa shetani na mambo yake yote,na hila zake zote,nakupokea Bwana Yesu,uwe Bwana na mwokozi wa maisha yangu, kuanzia sasa na hata milele,Ee Bwana unisaidie nipate kukuulia wokovu wangu,AMEN.” Kisha muombee.
A) MATUMIZI YA LUGHA NA SAUTI.
Ni vyema mshuhudiaji atumie lugha nyepesi kueleweka kwa wengi. Mfano ni vyema kutumia lugha ya kiswahili katika ushuhudiaji. Lakini endapo kama anayeshuhudiwa akitaka afundishwe kwa lugha nyingine mfano lugha ya kingereza basi mshuhudiaji ikiwa kama anaweza kushuhudia kwa lugha hiyo na ashuhudie. Na ikiwa hawezi basi ni vyema aombe kutumia lugha ya kiswahili anayoifahamu vizuri.
Ni vyema kutumia maneno yenye staha sawa sawa na neno la Mungu lisemavyo.
Ni vyema sauti yako wewe mshuhudiaji iwe ya chini,yaani ya kawaida. Isiwe kama unahubiri jukwaani wakati wa neno. Hekima itawale.
KUMBUKA YAFUATAYO:
Mshuhudiaji ni lazima awe mwombaji mzuri.
Mshuhudiaji awe pia ni msomaji na mwenye kulishika neno la Kristo Yesu.
Asiwe mtu wa kulaumiwa juu ya tabia yake huko mitaani./Awe na mahusiano mema na Mungu wake.
Aanze kujifunza kushuhudia nyumbani kwake au kanisani kabla ya kushuhudia nje.
Awe mberoya.
Ajitoe kidhabihu pasipo kuangalia kupata faida ya kimwili (Asiangalie malipo kwa maana kazi aifanyayo si ya Apostle bali ni ya Mungu)
Awe tayari kutoka na mtu yeyote aliyepangiwa,wala asichague chague wakuenda naye.Mwenyekiti wa kushuhudia awapange washuhudiaji wa siku husika kwa kuzingatia uiano wa jinsia pia ulinganifu wa mlengwa wa kushuhudiwa.
Ikiwa kundi la ushuhudiaji limemaliza maombi na kuanza safari,gafla kabla ya kufika nyumba yoyote pakaonekana baadhi yao wamekosa amani ya Kristo Yesu,basi rudini kwanza muombe tena kisha ndio mtoke tena.
Nyumba ya mchawi msiingie labda kama kuna msukumo mkubwa sana wa Roho mtakatifu juu yenu,ikiwa hakuna msiingie.
Muingiapo nyumbani mwa mtu na kama mmekataliwa,kunguteni mavumbi yenu na muondoke wala msiendelee kungangania hapo.
Ni vyema mnenaji akasomewa maandiko wakati wa kufundisha, la! ikiwa mnenaji anaweza kuongea na kusoma mwenyekuhubiri injili ni sehemu ya agizo kuu Mathayo 28:18-19.
Binafsi nimebarikiwa na semina hoi.Hebu juhudi ziendelee za kutia ukweli wa Mungu kwa njia hii ya mitandao.
JibuFuta