Jumapili, 7 Januari 2018

MALEZI YA WATOTO

 

“ mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee.”

Kumlea mtoto maana yake ni nini ?

Ni kumtunza na kumfundisha/kumuelimisha mpaka afikie mahali pa kujitegemea mwenyewe.

Ni kumtunza na kumfundisha kwa vitendo na maneno mpaka awe mzima, kiakili na kiutu kiasi cha kuweza kuendelea mwenyewe bila ya kukutegemea.

Njia ipasayo kumlea mtoto ni ipi?

Ni njia ile nzuri yenye maadili mema yanayokubaliwa na Neno la Mungu pamoja na jamii unayoishi katikati yake.


Mwenendo wenu ni fundisho kubwa kabisa mbele ya mtoto wenu. Njia ipasayo kumlea mtoto ni kuketi na mtoto na kumshauri maadili mema ya maisha (Kumb 6:7). Ni kumwelekeza kwenye mambo matakatifu, kabla hajaharibiwa na walimwengu.

Kwa mfano:-

Pale Nyumbani: Mlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hataatakapokuwa mzee.

– Ibada za nyumbani kwa wazazi pamoja na mtoto/watoto ni kitu muhimu sana.

– Mazungumzo yenu yanayohusu watu wengine, majirani, watumishi wenzako nk.

– Mnavyojibizana na mkeo/mumeo mbele ya watoto na hata sura yako ya kila siku mbele za watoto.

– Unavyowaelekeza watoto wako kuhusu maadili mazuri kwa waliomzidi umri.

– Adabu na heshima mezani mkiwa peke yenu na watoto au mbele ya wageni.

– Ikiwa wewe ni omba omba kila wakati hata watoto wako watakua hivyo.

Mahudhurio ya ibada: Mlee mtoto katika njia ipasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mzee.

– Unatarajia mtoto atachukua fundisho gani ukibaki nyumbani wakati wa ibada?

– Unatarajia mtoto atajifunza nini kama kila siku unachelewa ibada na kuwahi kutoka au kukaa nje ya kanisa saa ya mahubiri?

– Unatarajia mtoto atajifunza nini kama huchukui Biblia wala kitabu cha nyimbo unapoenda ibadani?

– Unatarajia kuelewekaje unapowaacha watoto nyuma wakati unapokwenda kuhudhuria vipindi mbali mbali vya ibada?

Tunapokuwa ibadani: Mlee mtoto katika njia ipasayo, naye hataiacha hata akiwa mzee.

– Usimwache mtoto acheze cheze na kutembea hovyo wakati wa ibada huku akipiga makelele.

– Sio vema wakati wa utoaji wa sadaka kumpa mtoto senti 20 au 50 wakati unazo pesa zaidi
Sio vizuri kupiga usingizi wakati ibada inaendelea. Au kutafuna pipi au “gum“ na kuchafua kanisa.

Kumbuka unayomfundisha mwanao kwa vitendo, yaweza kuwa picha nzuri au mbaya ambayo kwake itakuwa vigumu sana kuisahau au kuiacha hata atakapokuwa mzee!!!

Kwa nini?

Mzazi ni mwalimu wa kwanza kabisa kwa mtoto. Hivyo kila utakalomfundisha mwanao:-

– Atalizingatia na kulishika siku zote za maisha yake. Mfano: kama unapenda nyimbo za “dance“ au za kidunia yeye naye atazipenda hizo.

– Yale anayoyaona kwako anajifunza na kuyatendea kazi. Kwa mfano, kusema uongo, kuahidi bila kutimiza ahadi, kutukana nk

– Ukifanya kazi au kuishi katika hali ya uvivu usishangae mtoto wako akiwa mvivu.

– Ukiwa na bidii au ulegevu katika mambo ya Mungu, mtoto wako atakuwa hivyo.

– Ukiwa na hali ya usengenyaji na kuwadharau wengine mtoto wako atayaiga hayo.

– Kama una kiburi na majivuno au hali ya kutokumtii mumeo au kumpenda mkeo mtoto atajifunza hali hiyo.

– Kama una hali ya kutokuwa na ibada za nyumbani na uvivu wa kushiriki vipindi kanisani, mtoto atayaiga hayo.

– Kama unashabikia ya dunia na kuweka kando mambo ya kiroho mtoto atakuwa hivyo.

Hivyo mlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mzee.
TUWE VIELELELEZO VIZURI KWA WATOTO WETU NAO WATAKUA HIVYO.

               MALEZI YA WATOTO

Tabia ya mtu mzima inachangiwa kwa kiasi kikubwa na malezi ya utotoni mwake. Wanasaikolojia za watoto wanaeleza kuwa binadamu anajifunza vitu vingi sana katika kipindi cha utotoni kati ya mwaka 1 mpaka miaka 7 pengine kuliko kipindi kingine katika maisha yake hivyo kufanya malezi ya watoto kuwa jambo muhimu sana la kuzingatiwa na wazazi au walezi.

Mamabo anayojifunza katika kipindi hiki ndiyo yanayomtengeneza kuwa vile ambavyo anakuwa katika utu uzima wake. Hivyo basi hiki ni kipindi muhimu sana katika malezi na ukuaji wa mtoto.

Katika kipindi hiki mtoto anajifunza kwa haraka sana. Ni wakati ambao anajifunza kipi ni kizuri na kipi ni kibaya kutokana na jinsi walezi na jamii anayoishi inatafsiri na kufanya.

Inashauriwa katika kipindi hiki watoto kuwa pamoja na wazazi wao kama mazingira yake ni mazuri na yanachangia kujifunza kuzuri kwa mtoto.

Familia ambayo ina upendo na amani inamfundisha mtoto kuwa hivyo. Mtoto anajifunza kupenda kwa sababu anaona upendo katika familia yake,anajifunza kupenda amani na kutengeneza amani kama anaona wazazi wake au ndugu katika familia wanafanya hivyo.

Kinyume chake ni kuwa kama familia inakosa amani na upendo kati yao basi vivyo hivyo inamfundisha mtoto mambo mabaya. Mtoto anajifunza kutopenda au kutojua kupenda na hivyo kumjenga vibaya. Familia za aina hii zinajenga mazingira mabaya kwa mtoto wao.

Pia Soma:Madhara ya Kupongeza Watoto-Kama unafikiri umekuwa ukifanya vyema basi fikiri tena.
Changamoto za Kulea Watoto wa “Dijitali” kwa Wazazi wa “Analojia”
Familia zilizotengana wakati mwingine zinaleta uafadhali kwa upande mmoja wa kumfanya mtoto asione maisha yasiyo na upendo toka kwa wazazi wake; japo kwa upande mwingine kuna madhara kwa mtoto kwani hatajua umuhimu wa kuwa na mwenza wa maisha.

Watoto wengi ambao wamelelewa na mzazi mmoja au wazazi wakiwa mbalimbali wanapata shida kuishi na wenza katika maisha yao ya ukubwani.

Kwa ujumla ni muhimu sana kwa wazazi kupanga na kutekeleza aina ya malezi ya watoto ambayo yatawafanya wawe na maadili na tabia njema wakiwa watu wazima.

Tabia ya Kuomba:
Kumfundisha mtoto kuomba pale anapohitaji kitu inamfundisha kuwa mnyenyekevu kwa watu wengine hasa anapohitaji msaada.

Inamfundisha pia kuwa kupata kitu kisichokuwa chako inahitaji hiari toka kwa mmiliki. Mtoto ambaye hajui kuomba na kupewa anajengwa katika hatari ya kuwa mnyang’anyi na mbakaji siku za mbele.

Lakini pia kwa kuwa unapoomba kuna matokeo mawili,kukubaliwa au kukataliwa. Mtoto anajifunza hayo na anakuwa tayari kukubali hapana kama mojawapo ya majibu. Mtoto ambaye hajui kukataliwa kila anapoomba ni hatari pia.

Tabia ya Kulilia Vitu:
Tabia hii ni mbaya na ni lazima kwa wazazi kutoiendekeza kwani ina madhara makubwa kwa watoto na hatimaye hata wakiwa watu wazima.

Mtoto anayelilia vitu ni yule ambaye kwanza hajui kuomba na hata akiomba hajui kuwa kuna matokeo mawili,yaani “ndiyo” na “hapana”.

Watoto wanatakiwa kujua kuwa kuna wakati si kila kitu kinapatikana na katika hali hiyo kunahitajika uvumilivu. Kwani hii ndiyo hali halisi ya maisha kwa walio wengi duniani. Lakini pia mtoto anafundishwa kuwa si kila kitu ni kizuri kwake. Mtoto anaweza akalilia bia kama anamwona mama au baba anakunywa, ni vyema akaambiwa na akaelewa kuwa bia hairuhusiwi kwa watoto na hivyo hatapewa.

Kama mtoto yuko katika umri ambao anaweza akaambiwa na akaelewa sababu basi ni vizuri akaambiwa.

Hapana ni muhimu sana kwa mtoto,neno hili linatengeneza mipaka ya mahitaji ya binadamu mtoto. Inasaidia kujenga adabu katika maisha ya utu uzima.  Anajenga tabia ya kujizuia vile ambavyo anajua si vyema kwake.  Aidha kwa kujifundisha mwenyewe au kwa kuambiwa na wazazi wake au walezi na walimu toka akiwa mtoto.

Tabia ya Kusemea:
Utasikia mtoto anamwabia mama yake baada ya kuadhibiwa “Nitakusemea kwa Baba akirudi”.Hii ni tabia mbaya kwa mtoto. Kwasababu inamtengenezea kuamini kuwa hakutendewa haki na mama yake au mtu mwingine yeyote. Hii ina maana hata kama alifanya kosa hakiri kuwa ni kosa na hivyo ni ngumu kujirekebisha. Falsafa ya madiliko ya tabia inasema kuwa “Kukiri kosa ni nusu ya safari ya kujirekebisha”.

Tabia hii ikemewe kwa mtoto. Mtoto akija kwangu na kesi kama hii huwa namuuliza kwanini alifanyiwa hivyo alivyofanyiwa?. Jaribu kuuliza swali hilo kwa mtoto kila anapoleta kesi ya hivi na sikia majibu yake. Akikuambia sababu,ambayo mara nyingi inakuwa kosa lake mweleze kuwa hilo ni kosa na asirudie tena.

Hapo unampa mafunzo mawili,kwanza umemweleza kuwa amekosa kwa mara nyingine na hivyo kumfanya aamini na kukiri kosa na hivyo kujenga mazingira mazuri kuelekea kujirekebisha. Pili unamfundisha kuwa si kila anapoaadhibiwa anaonewa na akimbilie kuomba msaada.

Pia inamsaidia kujifunza kuwa aliyemwazibu alikuwa sahihi na inamsaidia kumheshimu na kumsikiliza siku za mbele.

Tabia ya Kumpongeza Mtoto na Kumuadhibu:
Pongezi ni muhimu katika kujenga tabia nzuri ya mtoto na hata akiwa mtu mzima kama ambavyo ni muhimu katika kuadhibu.

Mtoto anajifunza kuwa akifanya kitu vizuri au akifanya vitu vizuri anapata zawadi na kinyume chake anaadhibiwa. Hii ni kweli hata katika utu uzima.

Japo pongezi isizidi mipaka na kumuharibu mtoto (soma jinsi pongezi zinvyoharibu watoto) ni vyema mtoto akajua kuwa kunamatokeo chanya na hasi kwenye kila anachokifanya na pale anaposhindwa kufikia malengo basi aongeze bidii zaidi na atafanikiwa.
Pongezi inaweza ikawa ni makofi tu au maneno ya kumtia moyo kama “Hakika wewe ni mtoto mzuri, ninajivunia”. Pongezi zinamfanya mtoto kupenda kufanya vitu vizuri tena siku nyingine.

Adhabu ni muhimu pia,hasa pale ambapo mtoto ameelezwa mara kadhaa na haoneshi mabadiliko yoyote.  Adhabu ni kitu hasi chenye nia ya kukuongoza katika njia chanya.

Maisha ya binadamu yanaongozwa na sheria,sheria ziko kila mahali,nyumbani,kazini,barabarani na sehemu nyingine nyingi kwa madhumuni ya kuleta utaratibu fulani wa kuishi. Adhabu inamjenga mtoto kufahamu kuwa kunasheia na ni budi kuzifuata vinginevyo utaingia matatani.

Tabia ya Uchoyo,Ulafi na Ubinfsi:
Unajua mafisadi na majambazi wanatengenezwa wapi? Ni katika familia zetu. Tunamuona mtoto hataki kula na wenzake na ananyang’anya wenzake kile walichonacho hata kama hana kazi navyo na tunakaa kimya. Unategemea nini mtoto huyu akiwa waziri au raisi wa nchi?

Wazazi wanatakiwa kukemea tabia za uchoyo na ulafi kwa watoto. Mfundishe mtoto kucheza,kula na kupeana vitu na wenzake. Mjengee moyo wa kutoa na kuwa na kiasi kwani hivi vina mchango mkubwa katika kumjenga kuwa mtu mzima mwenye haiba.

MALEZI YA WATOTO

                            Utangulizi
                    Nini maana ya malezi
Malezi ni uangalizi wa karibu wa wazazi kwa mtoto wake kiroho, kiafya, kiakili, kitabia, Mungu ndie mwanzilishi wa watoto. Mungu alipomumba adamu, akamfanyia msaidizi wake Hawa, akasema zaeni mkaongezeke. Mwanzo 1.8.
Katika somo hili tutajifunza namna ya kulea watoto wetu tuliopewa na Mungu. Malezi haya yatagusa maisha ya watoto ya kiroho na kimwili. Tutaangalia haki na wajibu wa mtoto kama Neno la Mungu linavyofundisha, yaani Biblia Takatifu. Kwa njia ya somo hili wazazi tunaweza kuutimiza mpango wa Mungu kupitia malezi bora ya kiroho na kimwili kwa watoto wetu, kwa kufanya kazi pamoja na Mungu. Katika Rum. 8:28 tunasoma: “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema………” Hii ni pamoja na kazi ya kulea watoto; Mungu hufanya kazi hiyo pamoja na sisi.
Malezi ya mtoto yanaanza lini?
a) Kimwili - malezi ya matoto yananza akiwa bado tumboni. Yeremia 1.4,5. mama huyu inabidi kuzingatia kanuni zote za afya ikiwa ni pamoja na kula mlo kamili kuishi katika hali ya usafi wa mazingira, chakula na malazi, pia maombi yanaitajika sana kwa mama huyu, hivyo mama huyu anatakiwa amlinde sana mtoto huyu aliye tumboni ikiwa ni pamoja na baba huyu kumsaidia mama huyu aweze kujifungua salama mama huyu ajiepushe na madawa ambayo yanaweza kumuathiri mtoto pia aepuke misukosuko na kazi nzito.
Kuna sehemu kuu tano za ukuaji wa mtoto
Kimwili, kiakili, kihisia, kijamii.na kiroho.
Kimwili , watoto hukua kwa viwango tofauti, lakini utaratibu wao wa ukuaji kimwili karibu wote hufanana. Watoto hujifunza kwa kurudia rudia, hivyo mzazi anatakiwa amfundishe mtoto kwa kurudiarudia ili mtoto aweze kushika.
Kiakili watoto wadogo wengi ni wadadisi, hujifunza kwa kuiga
Kihisia watoto wadogo huonesha hisia zenye nguvu sana na hisia zao hutawala matendo.
Kijamii, watoto wote wanahitaji maongozo ya kibiblia na mifano ya kuiga. Hali tabia huathiri jinsi watoto wanapojifunza na jinsi wanavyohusia na wengine
Kiroho — mtoto huyu anahitaji kuombewa, kupendwa na kuambiwa maneno ya kutia moyo. Vinywa vya wazazi vitamke maneno ya baraka kwa mtoto huyo na sio ya laana au majuto. Kama wazazi watazungumza maneno mabaya kwa mtoto kipindi hiki ni rahisi sana shetani kuyachukua na kuyatumia kwa mtoto akishazaliwa au hata kabla hajazaliwa. Neno la Mungu linasema katika Mit. 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi………” Utapata matunda mazuri utanena vizuri juu ya mtoto wako aliye tumboni. Maneno yatafanyika mtego kama ukinena vibaya, shetani atayatumia kuumba jambo baya kwa mtoto, hivyo kwa hiyo unategwa na kukamatwa kwa maneno ya kinywa chako. (Mit. 6:2).
Mambo ya kuzingatia
Nena maneno ya baraka kwa mtoto. Muombee kila wakati na maombi yaguse ulinzi na uponyaji huku ukikemea na kuharibu laana zote za shetani ikiwa ni pamoja na zile za kiukoo au kikabila ili anapozaliwa zisiwe na nguvu kwake. Wengine wanaamini ukoo wao ni wa kimaskini, aidha wana historia ya uchawi, au magonjwa mbalimbali na kadhalika. Yakatae kwa imani hayo yote, yasiingie na kuwa urithi kwa watoto wako. Vile vile omba neema ya wokovu kwa ajili yake.
Mtoto akishazaliwa bado atahitaji lishe bora ili akue sawasawa. Chakula bora kwa mtoto anapozaliwa ni maziwa ya mama yake ambayo yana virutubisho vingi kuliko chakula kingine chochote na yanasaidia kuimarisha kinga ya mwili wa mtoto.Wanawake wengine hawapendi kunyonyesha kwani wanadai kuwa maziwa yao yanaweza kuwa makubwa na hivyo kuharibu maumbile yao, yaani ya mama. Mtoto anapokosa kunyonya ipasavyo anaathirika, anaweza kupata mashambulizi ya maradhi mara kwa mara. Mungu ameweka mfumo huo ili mtoto anyonye. Mungu hatapendezwa kabisa na kitendo cha mama kumnyima mtoto maziwa hayo, kwani ni kumnyanyasa na kumwonea mtoto huyo. Tabia ya mama kumnyima mtoto haki yake ya msingi ni sawa na tendo la uuaji kwa mtoto. Kwa upande wa kiroho wazazi wadumu kumwombea mtoto hata baada ya kuzaliwa pamoja na kumsemea maneno ya baraka.
SABABU ZA KUWAELEA WATOTO
a) Watoto ni thawabu
Katika Zab. 127:3 Biblia inasema “Tazama wana ndio urithi wa Bwana uzao wa tumbo ni thawabu.” Mungu hatupi watoto ili tuwahifadhi kwa matumizi yetu wenyewe. Yeye anatupa watoto ili tuwalee kwa utukufu wake. Watoto wetu ni wa Mungu.
Mungu anatoa baraka ya uzao. Naye anasema “Zaeni mkaongezeke mkaijaze nchi. (Mwa. 1:28,9:1,7) Tena anasema katika Law. 26:9 “Nami nitawaelekezea uso wangu na kuwapa uzazi mwingi na kuwaongeza nami nitalithibitisha agano langu pamoja nanyi.” Katika Kum. 28:4 anasema “Utabarikiwa uzao wa tumbo lako”. Katika kitabu cha Mwa. 48:9 “Yusufu akamwambia babaye, hawa ni wanangu Mungu aliyonipa hapa. ”Pia katika Isa. 8:18 inasema “Angalieni mimi na watoto hawa niliyopewa na Bwana tu ishara na ajabu katika Israel.” kumb 5.29,33
Biblia inatudhihirishia kuwa uzao au watoto wanatoka kwa Mungu mwenyewe. Mungu ameweka uhai katika mbegu na yai ili kwa pamoja vifanyike kuwa kiumbe hai, yaani mtu-mtoto. Bila uhai kuwepo mbegu na yai havina uzima.
Kwa sababu hii Mungu anataka tuwe na makusudi haya kwa ajili ya watoto wetu:-
Watoto wetu wafikie hatua ya kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wao na kufuata mpango wa Mungu kwa ajili ya maisha yao. Mungu anatazamia wazazi wawaelekeze watoto kwake, kwa njia ya Neno lake yaani maandiko matakatifu, Biblia.
b) Mungu ameagiza tuwafundishe watoto wetu
Mungu mwenyewe ametoa maelekezo, ya namna ya kuwafundisha watoto wetu. Katika Kum. 6:6-7 Biblia inasema “Na maneno haya ninayokuamuru leo yatakuwa katika moyo wako, nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako na utembeapo njiani na ulalapo na uondokapo. ”Tukisoma katika Mwanzo 18:19 Neno la Mungu linasema “Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe na nyumba yake baada yake waishike njia ya Bwana, wafanye haki na hukumu……..” Tunaona Mungu alipomwita Ibrahimu alikusudia awe kiongozi wa kiroho nyumbani na kuwafundisha wanawe njia ya Bwana.
Kwa wito wa Ibrahimu Mungu aliwaweka akina baba kuwa wawajibikaji katika kuwafundisha watoto wao waishike njia ya Bwana wafanye haki na hukumu. Kuwafundisha watoto wetu kanuni za Mungu na njia za neno lake ni jambo la kwanza, muhimu, na la lazima katika familia. Hii ni amri Mungu aliyowapa watu wake. Katika Zab. 78:5-7 anasema “……Aliyowaamuru baba zetu wawajulishe wana wao…..” Kile Mungu anachoamuru hutoa neema ya kutusaidia kutimiza. Moja ya njia kuu ya kuonyesha upendo kwa Mungu ni kujishughulisha na maendeleo ya kiroho ya watoto wetu na kujitahidi kuwaleta katika ushirikiano wa uaminifu kwa Mungu.
Mafundisho ya kiroho yanapaswa kuanzia nyumbani, wote baba na mama wayasimamie vyema. Kumwabudu Bwana ni lazima katika familia, na hii ni amri ya moja kwa moja kutoka kwa Bwana. (Kum. 6:7-9, 21:18-21, Kut. 20:12). Mwumini anapaswa awape watoto wake elimu yenye kiini katika Mungu kwa bidii, ambayo inawaonyesha ushirikiano wake na Mungu katika njia zake. Malezi haya yatamwandaa mtoto kuishi maisha ya kumpendeza Mungu.
Mafunzo ya kiroho na ya kibiblia kwa mtoto, kimsingi yanatoka katika familia na siyo kanisani au shule ya Jumapili. Katika maeneo haya mtoto huwa anao muda mchache sana, hivyo anahitaji kupata mengi zaidi kutoka kwa wazazi. Kanisa na shule ya Jumapili husaidia tu katika mafunzo ambayo msingi wake umekwishawekwa na wazazi wenyewe. Kwa sababu hii basi moyo wa baba ni lazima uugeukie moyo wa mtoto ili kuulea na kuuleta kwenye moyo wa Mwokozi Yesu. (Lk. 1:7)
c> Huathiri kizazi kijacho cha jamii wazazi ni lazima wakabidhi imani yao kwa wale watakao piga mbio baada yao ni lazima tupange mapema na tusiipuze mafunzo na mandalizi kwa kizazi kinachofuata kumtumikia bwana. zab 78. 2,7 wamuzi 2.10,11.
Hatua za kufuata ili kuwaongoza watoto katika maisha ya utauwa katika Kristo
Hatua za kufuata ili kuwaongoza watoto katika maisha ya utauwa katika Kristo
a) Waweke watoto wakfu kwa Mungu mwanzoni mwa maisha yao.
Kama tuliivyoona katika utangulizi wa somo hili kwamba ni vyema kumkabidhi mtoto mbele za Mungu mwanzoni kabisa. Katika 1Sam. 1: 28 Biblia inasema “Kwa sababu hiyo mimi nami nimempa Bwana mtoto huyu wakati wote atakaokuwa hai amepewa Bwana” mark 10.13.
b) Wafundishe watoto kumcha Bwana na kuukataa uovu.
Watoto wapende haki na kuchukia dhambi. Ingiza ndani yao ufahamu wa mtazamo wa Mungu na hukumu kwa dhambi. Katika Ebr. 1:9 Biblia inasema “Umependa haki umechukia maasi kwa hiyo Mungu, Mungu wako amekutia mafuta, mafuta ya shangwe kupita wenzio.”
Kazi hii ya kuwafundisha watoto ndio muhimu zaidi kuliko:
- Kupata mshahara mkubwa
- Kuheshimiwa na watu wengine
- Kuwa kiongozi kati ya watu
- Kutumikia kanisa.
Kazi ya kufundisha watoto ni wajibu wa wazazi wote wawili - yaani baba na mama. Baba na mama lazima watenge muda wa kuwafundisha watoto, kukaa na kuongea nao pamoja. Kwa njia hii watoto wanakuwa karibu zaidi na wanaweza kuelewa hisia zao kirahisi. Kama wazazi yaani baba na mama hawana muda na watoto, basi itakuwa vigumu kuelewa shida na matatizo yao. Hii inaweza kusababisha hatari, kwa mfano tu, ukakuta watoto wanaeleza shida zao kwa watu wengine maana wazazi hawapatikani kirahisi. Hii husababisha watoto kupokea ushauri na maelekezo yasiyo sahihi ambayo yanaweza kumpotosha mtoto. Wazazi wapange muda wa ibada ya pamoja na watoto wao.
c) Wafundishe watoto wako kutii na kuheshimu wazazi kupitia nidhamu ya Biblia.
Kumrudi mtoto kwa maonyo ya neno la Mungu. Ili watoto waweze kuelewa ni muhimu wafundishwe kwa neno na kwa mfano. Wazazi wanapaswa kumtii Kristo na kumfuata ili watoto wapate mfano halisi kutoka kwa wazazi wao. Wafilipi 4:9 Biblia inasema “Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea na kuyasikia na kuyaona kwangu yatendeni hayo…”
Njia za kuwafundisha watoto wetu
- Tahadhari ya hatari.
Wazazi wawe makini na kujihadhari na mambo ambayo yanaweza kuwaondoa watoto wao kwa Mungu. Macho ya wazazi yawe wazi katika kuona mambo wanayoyafaa watoto wao na kuwasaidia. Hii haina maana kukasirika na kuwa mkali, bali kuonyesha upendo na kushikilia yaliyo mema. Mambo yanapobadilika kwa watoto wazazi wanatakiwa kujua ili watoto wasiwazunguke kwa kutokujua kwao, na hatimaye kuwasababishia kutoka nje ya msimamo wa neno la Mungu. Mambo yote yapimwe kwa Neno la Mungu na kwa maombi ili watoto wapone.
- Fundisha kweli za Biblia wanazohitaji.
Wazazi wanapokuwa karibu na watoto katika kuzungumza nao ikiwa ni pamoja na kuwapa nafasi ya kujieleza ni rahisi kuyafahamu mahitaji yao na kujua changamoto wanazokutana nazo. Basi, uwe tayari kuzungumza na kuwasaidia watoto katika sehemu mbalimbali za maisha yao kutegemea umri na jinsia kama ni wa kiume au wa kike.
- Wasaidie watoto kutii.
Mzazi anawajibika kumsaidia mtoto kuwa mtii katika yale anayomuagiza kuyafanya na yale anayomfundishwa. Jinsi ya kumsaidia mtoto kutii: mfano unapomtuma kwenda kuchukua kitu fulani akakataa, basi wewe mzazi hutakiwi kwenda yeye badala yake, bali inabidi utafute njia ya kumfanya mtoto atimize kufanya ulichomtuma, ikibidi hata kwa adhabu, ili kumsaidia kuwa mtii kwa lile wasemalo wazazi. mith 22 15, mith23.14
Kama utamtuma naye akakataa na baadaye kisha aone unafanya mwenyewe; basi, tabia hiyo itajengeka na hata asiweze kukusikia kwa lolote utakaloagiza. Maana amejifunza kwako kuwa anapokataa kufanya kile ulichomtuma hatima yake utafanya mwenyewe. Kiburi kinamwingia mtoto.
Tunaona Mungu anatusaidia sisi kama watoto wake kutii neno lake kwa kutuonya ya kwamba tukikaidi tutaangamizwa. Isaya 1:18-20 anasema, “Haya njooni tusemezane asema Bwana… Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi, bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga…” Hapa Mungu anasema “Njoo” kinachotakiwa kwa mwanadamu ni kutii, vinginevyo, au kwenda kinyume cha hapo, ni uasi utakaofuatiwa na adhabu.
d) Walinde watoto wako na vishawishi viovu.
Ujue nia ya shetani siku zote ni kutaka kuwaangamiza watoto, iwe kiroho au hata kimwili kwa kufanya kuwavuta katika mambo ya ulimwengu. Kuna mambo kadha wa kadha ambayo watoto wanakutana nayo maishani na haya yanaweza kusababisha au kuwaondoa kabisa wasimfuate Mungu sawasawa. Kwa mfano:
- Majaribu ya dunia.
Neno la Mungu linasema “Msiipende dunia wala mambo yaliyomo katika dunia… na dunia inapita pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele”. (1Yoh. 2:15-17).
- Marafiki wabaya.
Kitabu cha Mithali 13:20 kinasema “… Bali rafiki wa wapumbavu ataumia. ”Pia Zab. 1:1 inasema: “Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki; wala hakusimama katika njia ya wakosaji; wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.”
- Tamaa zao wenyewe
Katika Waraka wa Yakobo 1:14 anasema, “Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa zake mwenyewe, huku akivutwa na kudanganywa.” Vishawishi vinavyotokana na yeye mwenyewe, kwa njia ya kuona, kusikia, kugusa, kuonja kisha anajisikia hamu ya kuviendea badala ya kuviepuka au kukimbia mbali navyo. Hatimaye mtoto anajikuta amejitumbukiza mwenyewe katika uovu.
- Uongo huletwao na shetani.
Shetani ni mwongo na baba wa waongo. Katika Yoh. 8:44 Biblia inasema: “ … Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa sababu yeye ni mwongo na baba wa waongo.” Mungu amempa kila mtoto watu wawili wa kumtunza kwa kusaidiana. Mtoto anaishi nyumbani kwao miaka mingi na anawategemea wazazi. Mungu alipanga hivyo ili wazazi waweze kuwafundisha watoto wao na kuwajibika.
- Wafahamishe watoto kuwa Mungu wakati wote anawaangalia na kuthamini yale wanayoyafanya, kwa kufikiria, kusema na kutenda. Zaburi 139:2,4,7,12 inasema: “Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu. Umelifahamu wazo langu tokea mbali. Maana hamna neno ulimini mwangu usilolijua kabisa Bwana …. Niende wapi niukimbie uso wako? … Giza nalo halikufichi kitu, bali usiku huangaza kama mchana. Giza na mwanga kwako ni sawasawa”
_ Wafundishwe kuhusu mabadiliko ya miili yao hasa kipindi cha kubalee
e) Waongoze watoto wako mapema juu ya kuipokea imani binafsi katika maisha yao, toba na ubatizo katika Kristo na nguvu za Roho mtakatifu. Wasiwe watoto tegemezi kiimani, bali wafikie kumfahamu na kumkiri binafsi Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wao. Hii itawajengea msimamo imara katika Imani hata wawapo mbali na nyumbani kwa wazazi. warum 10. 9
f) Wazoeze watoto wako kwenda kwenye kanisa la kiroho ambako Neno la Mungu linahubiriwa na nguvu za Roho Mtakatifu zinadhihirishwa. Wafundishe usemi usemao “Mimi ni mwenzao watu wote wakuchao, na wale wayatiio mausia yako”. (Zab 119:63)
g) Watie moyo watoto wako kuendelea kujitenga na mambo ya ulimwengu pia waweze kushuhudia na kumtumikia Mungu. Yakobo 4:4 anasema, “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu?.” Wafundishe ya kuwa wao ni wageni na wasafiri juu ya uso wa nchi, siku moja wataondoka. (Ebr.11:13-16). Ni kwamba nyumbani kwao hasa na uenyeji wao uko mbinguni huko ndiko Kristo katuandalia makao ya milele (Kol 3:1-3, Yoh 14:1-3). Pia katika Wafilipi 3:20 Biblia inasema, “Kwa maana sisi wenyeji wetu uko mbinguni kutoka huko tena tunamtazamia mwokozi Bwana wetu Yesu Kristo.”
h) Wafundishe watoto wako kwamba Mungu anawapenda na kuwa ana makusudi maalumu kwa ajili ya maisha yao. (Luka 1:13-17, 1Pet 1:3-9) Katika Rumi 8:30 anasema, “Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki, hao akawatukuza”. Kwenye mstari wa 28 anasema, “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani wale walioitwa kwa kusudi lake”.
j) Waeleze watoto wako kila siku kwa kutumia neno la Mungu na kwa kufanya mazungumzo, ibada na maombi ya pamoja kwa familia. 1 Timotheo 3:15 anasema: “… Tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu”.
Katika kitabu cha Kumbukumbu 6:6,7,9 Mungu anasema: “Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe wafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena katika nyumba yako, utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo… Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako”. Watie moyo watoto wako, ili waishi maisha ya kudumu katika maombi, kwa njia ya kuwa kielelezo na wosia. Mzazi uwe kielelezo. Efeso 6:18: ”Kwa sala zote na maombi, mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo, na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote”.
k) Waandae watoto wako kuteseka na kustahimili mateso kwa sababu ya haki. Wanatakiwa wajue ya kuwa imeandikwa: “Wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa”. (2Timotheo 3:12). Maudhi ni sehemu ya maisha kwa mtu wa Mungu yeyote anayeishi kwa kumpendeza Mungu kwa maana yuko kinyume na shetani pia na matakwa ya ulimwengu. Yoh. 17:14-15 Yesu anasema: “Mimi nimewapa neno lako, na ulimwengu umewachukia, kwa kuwa wao si wa ulimwengu, mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu bali uwalinde na yule mwovu”. Rumi 8:18: “Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu”. (Soma pia Rumi 8:31-39)
l) Wainue watoto wako mbele za Mungu kwa bidii siku zote (Efeso 6:18). Zingatia juu ya maombi ya Bwana Yesu kwa ajili ya wanafunzi wake kuwa kama mfano wa maombi ya mzazi kwa ajili ya watoto wake. (Yohana 17:8-15)
m) Uwe na upendo kwa watoto wako na kuwajali, kiasi kwamba unakuwa tayari kuyamimina maisha yako yawe kama dhabihu kwa Bwana ili kufanya imani yao ikue na kuyafanya maisha yao yawe iwapasavyo kuwa kwa Mungu wao. Katika Wafilipi 2:17: “Naam, hata nikimiminwa juu ya dhabihu na ibada ya imani yenu, nafurahi…” Hapa inaonyesha upendo na kujali kwake mtume Paulo na anavyowajali watoto wake wa kiroho huko Filipi, kiasi kwamba, alikuwa tayari kutoa uhai wake kwa ajili yao. Ikiwa mtume Paulo alikuwa tayari kujitoa hivyo, kwa ajili ya watoto wa kiroho! Je, haingetupasa kufanya hivyo zaidi hasa kujitoa kwa ajili ya watoto wetu wenyewe?
Gharama ya kujitoa kwa ajili ya watoto wako yawezekana ni ule muda wako wa kukaa nao, kutoa mali zako kwa kuwapa elimu au mtaji wa maisha, kufanya maombi ya kufunga kwa ajili yao, lakini pia kujinyima starehe, na kuteseka ili tu watoto wafikie kiwango kizuri katika kumjua Mungu na pia maisha yao ya kiroho na kimwili yampendeze Bwana na kanisa.
Ikumbukwe kuwa mali pekee sio jibu kamili la kuwajali watoto, maana kizazi hiki starehe na anasa zimekuwa chambo cha kuwapoteza watoto. Ni vizuri mzazi akafanya yote katika uwiano mzuri, ili kwa kila jambo aoneshe kujitoa kwake kwa ajili ya watoto wake. Kwa kufanya hivyo Mungu atapata utukufu na kufanya ya watoto yawe mema na yenye baraka.
Hatua zote hizi zinalenga kumfundisha mtoto kwa njia ya nadharia na vitendo au kwa mfano/ kielelezo. Kuna Mithali inasema “Maneno matupu hayavunji mfupa”. Hivyo basi, katika kusema na kuonyesha kwa vitendo au kutoa mfano halisi, anayefundishwa anaweza kushika vizuri zaidi somo husika, kuliko kutoa nadharia au maneno matupu peke yake.
Mazazi lazima umuwekee mtoto wako mazingira mazuri ya maisha kwa mfano elimu ni muhimu, akiba, urithi. mith 4.13
Mambo yanayozuia mafundisho ya wazazi kwa watoto
Matendo yasiyo na hekima
Maandiko yanasema katika kitabu cha Yakobo 1:5: “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima na aombe…” Ili watoto wenu wapokee mafundisho ni muhimu kumwomba Mungu atupe hekima ya kuwalea hawa watoto. Matendo yasiyo ya hekima ni kama yafuatayo:-
- Kuwaaibisha watoto mbele ya wengine. Mara nyingi wazazi wanawaadhibu watoto mbele ya wenzao, jambo hilo siyo zuri. Mtoto anakosa ujasiri mbele ya wenzake. Hata kama mtoto ni mdogo ni vyema kumchukua mahali pa faragha na kumweleza kosa, kisha ukamwadhibu. Inawezekana siyo adhabu tu inayomfanya ajisikie kudhalilika mbele ya wenzake, lakini wapo pia wazazi wanaopenda kuwaogesha watoto wao nje au mbele ya wenzake wakimwangalia; si tendo la busara. Lazima tukumbuke kuwa watoto nao ni watu kamili walio na hisia, utashi, aibu nk. Hivyo tuwaheshimu.
- Adhabu kali kupita kiasi. Wazazi ni lazima wapime adhabu wanazotoa kwa watoto wao kulingana na kosa, jinsia, umri na mazingira pia. Vilevile adhabu isitolewe kwa hasira, vinginevyo mtoto hataelewa kosa na anaweza akarudia kama hakuelewa. Biblia inatufundisha jinsi ya kutoa adhabu kwa watoto wetu, hivyo tunahitaji uongozi wa Mungu ili tusiwe sababu ya kuwapoteza watoto wetu kwa adhabu zilizo kali kupindukia.
- Kumwambia kuwa kazi yake haifai au kuidharau kwa kuona si kitu. Jambo hili linatendeka hasa kwa watoto wenye umri mdogo, pale wanapoanza kujifunza kutengeneza vitu vya kuchezea, hutengeneza vijisanamu vya udongo, maboksi, au miti kwa maumbile mbalimbali. Wakati huyu mtoto hubeba kila anachodhani kinafaa kwa kuchezea na kufanyia kazi yake. Vitu vyao wanaweza hata kuviingiza ndani, sebuleni au wakaenda navyo kitandani mwao wanamolala bila wasiwasi. Wazazi huchukia na kuona kama ni uchafu na kuwafokea ovyo, watoto wanajisikia vibaya na kuona wameonewa na wazazi, wanajiona hawana haki. Njia nzuri hapa ni kumuelekeza kwa upendo na kumpa eneo maalumu la kufanyia shughuli zake huku ukimtia moyo kwa kazi anayofanya na kumsifu au kumsaidia kufanya vizuri zaidi ikiwezekana. Kwa njia hii, mtoto anajengeka katika ubunifu na atakapoanza shule atakuwa na akili nyingi na kujiamini. Kama anajisomea, usimlaumu pale anapokosea, mwelekeze kwa upendo. Tena usimwambie mtoto wako kuwa “wewe huna akili, utakuwa ni wa mwisho tu!!” Maneno hayo na mengineyo yanamharibu mtoto kiufahamu na kumvunja moyo kabisa hivyo, hayafai.
- Kumkemea bila kuchukua hatua yeyote. Mara nyingi utasikia kwa mama au baba akimwambia mtoto, kwa mfano, “acha!!, nitakupiga wewe.” Mtoto anaendelea tu kufanya anachofanya na mzazi wala hamchapi. Hali hii inamjengea mtoto kuona kuwa mzazi ana tabia ya kusema au kufoka tu, wala hafanyi chochote. Kufanya hivyo ni mbaya sana kwa mtoto. Ni vizuri mzazi akimwambia mtoto “acha” au “njoo” au “nenda” na mtoto asipotii kufanya, basi, mtoto anatakiwa asaidiwe kutekeleza aliloambiwa ili aumbike tabia ya kutii.
- Kuwa na mtoto mmoja unayempenda kuliko wengine miongoni mwao. Hii ni tabia mbaya itakayomfanya huyo mtoto asipokee mafundisho ya mzazi. Mtoto asiyependwa anaona mafundisho yako hayamhusu, bali ni ya yule anayependwa. Moyoni mtoto anafunga mlango wa kupokea utakalomwelekeza, kwa ajili ya upendeleo unaofanya. Mwanzo 37.3.
- Kutokusikiliza matatizo au haja zao. Wakati mwingine wazazi wanapokuwa katika hali isiyo nzuri kiuchumi; fedha hakuna, mambo hayaendi vizuri, wanakuwa wakali bila sababu na kutokusikiliza haja za watoto wao. Njia nzuri ya kusikiliza na kuongea nao ni maneno ya Mungu, na kuwafundisha jinsi ya kumwomba Mungu ili aweze kufungua milango na kuwapatia haja zao. Itawajengea imani kwa Mungu. Pia unahitaji kuwaombea watoto wako; Mungu anaweza kufanya kazi katika mioyo yao. Tunaamini Mungu anaweza kuwabadilisha watoto wetu katika yale tunayoyaona kwa akili zetu ni magumu kuwasaidia kwa njia za kawaida.
Kuwalea watoto wetu
(i) Kuwasaidia kutenda Mema.
Biblia katika kitabu cha Mithali 22:6 inasema, “Mlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mzee”. Ni wajibu wetu wazazi kujitoa nafsi zetu kuwafundisha mambo ya kimungu pamoja na adabu njema. Neno “fundisha “ kwa kiebrania lina maana “weka wakfu”. Hivyo mafundisho ya kikristo yana makusudi ya kuwaweka wakfu watoto wetu kwa Mungu na katika mapenzi yake, na kuwafanya wajitenge mbali na mambo maovu; hivyo kuwa katika mwenendo wa kumcha Mungu. Wazazi wawatie moyo watoto wao kumtafuta Mungu wao wenyewe ili kuwafanya wafurahie mambo halisi ya kiroho ambayo Mungu anawatendea; hawataweza kuyasahau kabisa hata wajapo wakubwa au watu wazima. “Naye hataiacha”. Kwa kanuni hii, mtoto aliyefundishwa sawasawa na wazazi wake hawezi kuziacha njia alizoelekezwa na Mungu.
Tunahitajika kuwarithisha watoto imani tuliyo nayo, kama vile tunavyosoma katika 2Timotheo 1:5 “ Imani ..ambayo ilikaa kwanza kwa bibi yako Loisi na katika mama yako Eunike …” Tunaona Timotheo alifundishwa maadili ya kimungu kupitia bibi yake na mama yake na hatimaye akawa mtumishi mzuri wa Mungu. Licha ya baba yake alikuwa myunani, mama yake alifanya bidii kumfundisha na kumlea katika Mungu, hata akafanikiwa. Haleluya! Mama usikate tamaa, endelea kufanya bidii, Mungu atakutendea.!!
Hata hivyo wapo baadhi ya watoto wenye wazazi waliomwacha Mungu au wanaoshindwa kuendelea na Mungu wao. Kutokana na kuishi kwao kwenye jamii yenye uovu, au hata kwa kuona baadhi ya watu wa Mungu wakiishi maisha yasiyokuwa na uaminifu, watoto hawa nao wanaweza kuambukizwa tabia hizo. Mengine ni kama yale niliyoandika kwenye kurasa za nyuma juu ya “Mambo yanayozuia mafundisho yetu kwa watoto”, kwa ufafanuzi zaidi.

(ii) Mbinu za kuwasaidia watoto kutenda mema.
Wazazi wanapaswa kutunga sheria zenye hekima ili kuwasaidia watoto watende mema. Sheria hizo zianze kutumika mapema wangali watoto wachanga. Sheria zinawasaidia watoto wajue mambo ambayo wazazi wanataka wafanye na yale wasiyopenda yafanyike.
Ili kuzisimamia sheria hizo kwa bidii na sheria hizo ziweze kufanikiwa basi:-
a) Lazima wazazi wote wawili wakubaliane juu ya sheria hizo.
Wazazi wawe kitu kimoja katika kila sheria waliojiwekea. Isitokee labda baba anatunga sheria ambayo mama hakubaliani nayo au mama anatunga sheria ambayo baba hakubaliani nayo, kwani hali kama hii ni hatari sana kwa watoto. Jambo hili ni baya sana, na linaweza kuwachanganya watoto na kusababisha uasi mwingi ndani yao. Wazazi wanaposhindwa kukubaliana katika sheria juu ya watoto wao, basi, kunaweza kutokea matatizo yafuatayo:-
(i) Watoto wanaona mfarakano wa dhahiri au hali ya kutofautiana kwa wazazi wao, hawajifunzi umoja na upendo kati ya baba na mama.
(ii) Itatokea wazazi kukasirikiana katika utekelezaji wa sheria hasa pale ambapo moja haijafuatwa.
(iii) Watoto wanaacha kuzitii sheria hizo.
(iv) Watoto wanakimbilia kwa mzazi mmojawapo au mwengine kuliko na upendeleo.
(b) Lazima watoto wazielewe sheria hizo.
Wazazi wanapotunga sheria ni muhimu wawaeleze watoto kwa uangalifu. Wawaeleze jinsi watoto watakavyotii na ieleweke na kutekelezeka. Kama haieleweki ni rahisi kuvunjwa.
(c) Lazima wazitii sheria hizo kila siku.
Wazazi wawe wavumilivu kuwakumbusha watoto sheri hizo. Wakati mwingine watoto wanaasi, pale wanapogundua kuwa wazazi wamesahau sheria walizoweka. Sheria ziwe sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Wakati mwingine sheria zinakuwa nzuri na zinaeleweka, lakini wazazi wanapokuwa na shughuli nyingi, kuchoka na kutokuwa na muda na watoto, basi, wanashindwa kutunza na kusimamia sheria hizo nzuri walizozit
Kuonya na kuwaadhibu watoto wetu.
Hii ni sehemu muhimu kabisa kabisa katika malezi ya watoto. Pamoja na kwamba katika ulimwengu wa sasa wazazi wanapuuzia kuonya na kuadhibu watoto wao kwa madai kuwa ni kuwanyanyasa, bado wanasahau kuwa Mungu mwenyewe ameagiza tufanye hivyo, ili watoto wetu wasipotee.
Kuonya na kuadhibu ni upendo wa mzazi kwa mtoto. Katika kitabu cha Mithali 3:11,12 anasema, “Mwanangu usidharau kuadhibiwa na Bwana …. kwa kuwa Bwana ampendaye humrudi …”. Hivyo basi, Mungu anapotuonya na kutuadhibu sisi watoto wake anasema anafanya hivyo kwa sababu anatupenda. Vivyo hivyo ni muhimu wazazi watoe maonyo na adhabu kwa watoto kwa sababu wanawapenda.
Wakati mwingine watoto wanaasi hata kama wanazijua sheria. Inawapasa wazazi kuwaadhibu, ijapokuwa adhabu inapotolewa huwa si wakati wa furaha, lakini inahitajika.

Sababu za kuwaadhibu watoto wetu:-
i) Tunawaadhibu kwa sababu tunawapenda.
ii) Tunawaadhibu ili kuwarudi waweze kutenda matendo mema.
iii) Tunawaadhibu ili kuondoa ujinga uliofungwa ndani ya mtoto.
Kabla ya kutoa adhabu ni muhimu kumkumbusha mtoto sheria na kumwelemisha kosa lake. Huu sio wakati wa kujadili bali wa kutenda. Ni vibaya sana kumwadhibu mtoto wakati mzazi bado una hasira, kwani hutaweza kumwelewesha kosa sawasawa na kwa sababu hiyo mtoto atajisikia umemwonea. Ukiwa na hasira huwezi kufanya jambo zuri. Biblia inasema “Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu.” (Yakobo 1:20)
Aina ya adhabu:-
Adhabu ziko za namna mbalimbali kutegemeana na umri wa mtoto, mazingira anayoishi na wakati mwingine jinsia yake. Adhabu inaweza kuwa ni kumchapa kwa fimbo, kumyima marupurupu fulani ambayo pengine anayapenda sana n.k.
Kuchapa kwa fimbo Biblia imefundisha sana ijapokuwa kizazi hiki watu wanapindua mambo na kusema watoto wasichapwe kwa fimbo. Hii ni ajabu sana na hatari kubwa! Mungu anasema “mchape mtoto”. Mwanadamu anasema “usimchape mtoto”, hivi ni nani asikilizwe?
Mithali 13:24: “Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanaye …”. Maandiko yanaagiza wazazi wawarudi watoto wao kwa kutumia “fimbo”. Kuchapa kufanywe kwa upendo pale tu mtoto anapokuwa amefanya kosa kwa makusudi au kwa kutokujali. Usitumie fimbo kwa kumuumiza au kumpa majeraha. Nia au lengo ni kuondoa ujinga kama maandiko anenavyo.
Mithali 22:15: “Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto, lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali.” Mtoto asiposaidiwa mapema angali mdogo huleta matokeo mabaya baadaye na inaweza yakawa mateso kwake na kwa familia.
Mithali 29:15 inasema “Fimbo na maonyo hutia hekima bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye”. Adibisho hili ni muhimu kumsaidia mtoto asiwe na tabia mbaya ambayo baadaye inaweza kumfanya kuwa na maisha mabaya, yasiyokubalika kwa jamii husika, kuwa mharibifu, na hata kusababisha kifo. Katika Mithalli 19:18 Biblia inasema: “Mrudi mwanao kwa maana liko tumaini”. Mithali 23:13,14 inasema: ”Usimnyime mtoto mapigo, maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa… Na utamwokoa nafsi yake na kuzimu” na Mithali 29:17 inasema: ”Mrudi mwanao naye atakustarehesha, naam, atakufurahisha nafsi yako”. Mithali 10:17 inasema: “Akubalie kurudiwa huwa katika njia ya uzima..”
Tunahitaji msaada wa Mungu ili kuweza kufanya mambo haya, kama vile Yesu alivyosema katika Injili ya Yohana 15:5b kuwa, ”Maana pasipo mimi, ninyi hamwezi kufanya neno lolote”. Tuwaombee watoto wetu na kujiombea sisi wenyewe wazazi ili Mungu atupe hekima yake na jinsi ya kuwalea watoto ipasavyo.

Wajibu katika familia.
WAZAZI.
Wazazi wa Kikristo wana wajibu kwa watoto wao ili kuwapa malezi bora yanayowasaidia kimwili, kiakili na kiroho.
i) Kuwalea kiroho.
Ni muhimu wazazi wakaanzisha ibada ya familia nyumbani. Hii ni ibada inayojumuisha jamii nzima nyumbani yenye lengo la kuisaidia familia kuwa na mawasiliano mema na Mungu. Ibada hii isimamiwe na baba na mama au kama yupo mtoto mkubwa nyumbani anayeweza kuongoza. Lakini ni muhimu sana wazazi au walezi wakawepo katika ibada hiyo, na wala sio kuwaachia watoto peke yao. Mungu aliumba jamii na aliazimu baba na mama au walezi wa watoto waishi pamoja. Ibada hii isiwe ya muda mrefu, na ni vema wote waweze kushiriki vizuri, bila wadogo kuiona ni kero na kulala usingizi. Inasaidia kuleta umoja wa familia kiroho na Mungu anakuwepo katikati yao. Mathayo 18:20 Yesu anasema: “Kwa kuwa walipo wawili, watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao”.
ii) Kuwalea kiakili.
Wazazi wajitahidi kuwapa msingi mzuri wa elimu watoto wao inavyostahili, wasiwanyime watoto fursa ya kusoma pale inapowezekana kwa jinsia zote na bila ubaguzi, kwani kuwanyima huko kutawajengea mazingira magumu ya kuishi hapo baadaye. Elimu itawasaidia kuwafungua kifikra na ujuzi. Pili, Wazazi wawashirikishe watoto wao katika mipango ya familia. Watakapokuwa wakubwa watakuwa wamezoea kazi, miradi na majukumu mbalimbali ya familia na hivyo kushirikishwa katika mipango mbalimbali ya wazazi, na kisha utekelezaji wake kuwa rahisi. Watoto wajue huduma, utumishi na maono ya wazazi wao, na wazazi wawatie moyo katika kumtumikia Mungu na kujiendeleza kielimu kwani Mungu anawahitaji watu kama hao katika kazi yake.
iii). Kuwalea Kimwili.
Wazazi wana wajibu wa kuwatimizia watoto wao katika mambo ya mwili, ikiwa ni pamoja na chakula, mavazi, malazi, matibabu, elimu na mengineyo. Ni jambo la aibu mtoto wa Kikristo kuonekana anazurura ovyo mitaani, na kuwa ombaomba, ati, amekosa mahitaji muhimu. Kitendo hicho kinamhuzunisha sana Mungu. Mungu anahitaji kila mzazi kufanya kazi kwa mikono yake, ndimo alimo amuru baraka zitakazokuwezesha kuitunza familia yako.
“Utabarikiwa mjini utabarikiwa na mashambani …” (Kum. 28:3). Pia amekuahidi kuwa “… Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa …”. (Ebr.13:5) “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? … Kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Basi utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa”. (MT. 6:31-33)
“Tena mjitahidi kutulia, na kutenda shughuli zenu,na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe, kama tulivyowaagiza, ili mwenende kwa adabu mbele yao walio nje, wala msiwe na haja ya kitu cho chote”. (1The. 4:11,12)
1Timotheo 5:8: “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini”.
Na katika Mithali 21:25 inasema: “Matakwa yake mtu mvivu humfisha, kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi”. Pia wazazi wanatakiwa kujua kuwa wao ni washauri na wapatanishi, Waalimu, na Viongozi katika familia zao hivyo basi:-
a) Kama washauri na wapatanishi
Biblia inatufundisha katika Mathayo 5:9: “Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu”. Neno la Mungu linatufundisha kuwa Mungu ameweka huduma ya upatanisho ndani yetu. (2Kor. 5:18). Ni jambo la aibu mzazi kufitinisha watoto wake na kuonyesha upendeleo wa dhahiri. Watoto hawa katika maisha yao yote utakuwa umewajengea chuki na fitina baina yao, na kufanya kikwazo katika jamii yako.
Zab 64:6-8: “ Hutunga maovu, husema tumefanya shauri kamili; Na mawazo ya ndani ya kila mmoja wao, na moyo wake huwa siri kabisa; Kwa hiyo Mungu atawapiga shabaha, kwa mshale mara watapigwa; Ndivyo watakavyokwazwa, Ulimi wao wenyewe ukishindana nao. Wote wawaonao watatikisa kichwa”. Na katika Mithali 11:14 Neno la Mungu linasema: “Pasipo mashauri taifa huanguka, bali kwa wingi wa washauri huja wokovu”.
b). Kama Walimu
Wazazi wajijue kuwa wao ni walimu wa msingi kabisa kuliko mwalimu yeyote yule. Wao hawahitaji kugharimia fedha yoyote ili kufikisha mafundisho yao kwa watoto wao, kwa maana wanaye mtoto tangu anapozaliwa na hivyo ni vema kuanza mara moja kumpatia mafundisho na malezi yanayohitajika. Wanayo nafasi nzuri katika kumshirikisha imani yao, maadili yao na mengine wanayoyapenda. Hivyo lazima wawe walimu wa neno na mfano au kielelezo bora katika kuwakilisha mafundisho yao mema kwa watoto na yanayompendeza Mungu. Pia kwa kuonyesha heshima, lugha nzuri ya mawasiliano na wengine, upendo na mwenendo mwema kwa ujumla.
(1Timotheo 4:12).
c) Kama wenye mamlaka na Viongozi
Kwamba wazazi wajue wana mamlaka na ni viongozi katika familia. Hivyo ni lazima kuwa na maamuzi yanayohusu familia juu ya watoto wao wakati wote. Maamuzi yanaweza kuwa katika sura mbili. Kwanza, mtoto afanyapo vizuri anastahili pongezi na kutiwa moyo na ikiwa amekosa anastahili adhabu. Mzazi asisite kuchukua hatua inayostahili, na kuwa na uamuzi wa kufanya hivyo. Pili, mtoto anapokabiliwa na maadui wenye kumpotosha au kumdhuru aidha kiroho, kimwili na kiakili, basi mzazi kama kiongozi anawajibika kuliangalia jambo hilo kwa makini na kulitafutia ufumbuzi wa makini katika kulitatua.
Ikumbukwe kuwa mtoto anamtegemea mzazi kwa uamuzi wake katika kila jambo. Mzazi anapoonyesha ulegevu wa maamuzi katika mambo yanayomkabili, basi, yeye huchukua njia yeyote ile atakayoiona, kuwa ni nzuri au hata yenye kuweza kumletea madhara na kisha matokeo yake yakaigusa familia nzima kwa namna moja au ingine. Hivyo wazazi waonyeshe upendo wa kweli na kuwapa ulinzi katika mazingira ya kiroho, kiakili na kimwili pia.
B WATOTO
Watoto wanawajibika katika :-
i) Tabia njema na Utii.
Ni wajibu wa watoto kuonyesha tabia njema na utii kwa wazazi wao. Katika Efeso 6:1-3 Nenoneno la Mungu linasema: “Enyi watoto watiini wazazi wenu katika Bwana ….. Waheshimu baba yako na mama yako, amri hii ndiyo amri yenye ahadi …” Pia soma katika Kolosai 3:20, na Kutoka 20:12
ii) Kutunza maadili ya nyumbani.
- Kuonyesha heshima kwa wakubwa katika kushika na kuyafanya mambo anayoelekezwa na wakubwa.
- Kuwa na mwelekeo thabiti katika elimu.
- Kufanya kazi kwa bidii katika yale yanayomhusu mwenyewe na pia wengine, kama kuwasaidia wazazi kazi mbalimbali zilizopo nyumbani na kulingana na mazingira, umri na uwezo wa mtoto: kama vile kuosha vyombo, usafi wa ndani na nje ya nyumba, kupamba na kadhalika, ili kuipa hadhi njema familia.
- Kuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri katika familia na kuhifadhi umoja huo kwa gharama yoyote.
Kujua kuomba msamaha kwa wengine pale anapokosea na kusamehe anapokosewa. Wajue kuwa watoto ni baraka katika familia na magomvi hayabariki.
Kama watoto hawatatambua na kufanya wajibu wao kama neno linavyofundisha, basi, tatizo la mmomonyoko wa maadili katika jamii bado litakuwa kubwa. Watoto wakifanya wajibu wao ni haki yao kabisa, tena ni HAKI YA MTOTO na ni wazi kulingana na maandiko yaani Biblia. Kama hawautimizi wajibu huo, ni wazi kuwa wanaipoteza haki yao kimsingi ambayo Mungu aliwapa ili wawe taifa takatifu linalompendeza.
Na wazazi tukishindwa kusimamia wajibu wetu ili kumsaidia mtoto katika njia njema, haki itakosekana, na tutawaletea watoto wetu laana katika kizazi chao. Kumbuka usemi usemao “Unayoyaona leo ni matokeo ya waliotutangulia”. Katika Kutoka 20:5,6, neno lasema: “… Mimi, Bwana, Mungu wako ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu”.
Watoto huasi
Wazazi wasishangae kuona watoto wanaasi. Hata wale watoto wanaoonekana wema wakati mwingine nao huasi. Hii ni kwa sababu sote tumezaliwa katika hali ya dhambi. Neno linasema katika Zaburi 14:13: “Wote wamepotoka wameoza wote, pia hakuna atendaye mema la! Hata mmoja”. Hata kama wangalifungiwa katika chumba cha ndani peke yao, na kutunzwa humo wenyewe, wakiendelea kukua humo; utashangaa, kuona bado tabia ya uasi ikijionyesha! Mfano, hasira, chuki, ugomvi, tamaa mbaya na mengineyo.
Hiyo ni asili ya mwanadamu baada ya anguko, dhambi ikamtawala. Anahitaji kusaidiwa katika neema ya Yesu Kristo chini ya uangalizi wa wazazi wake. Kama tulivyosoma katika Mithali 29:15,17: “Fimbo na maonyo hutia hekima, bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye”. Pia Mithali 29:17: “Mrudi mwanao naye atakustarehesha …”. Na Mithali 22:6 anasema: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”.
Mzazi asimtetee mtoto pale anaposhutumiwa kufanya maovu na kumkingia kifua bila kufanya utafiti wa kutosha. Mara nyingi mtoto anaweza kuonyesha wema machoni pa wazazi lakini anapotoka nje shuleni au mitaani hubadili tabia, usishangae kuwa mambo anayoyafanya yakawa tofauti kabisa na mwonekano mbele yako. Hivyo mzazi lazima uwe makini sana. Maana kwa kumtetea mtoto kwa yale mabaya anayoyafanya kunaweza kumharibu mtoto na pia kusababisha mahusiano mabaya kwenu wenyewe kama familia na hata kwa majirani pia.
Watoto wanapoasi huwa ni wakati mgumu kwa wazazi, lakini sheria zisibadilike, wazazi wawe thabiti, wema na wapole. Wanapaswa kujaribu kumwelewa mtoto huyo na mabadiliko yake kimwili, kiroho na kiakili. Wajitahidi kuzuia njia au mambo yanayompelekea mtoto kubadili mwelekeo au tabia. Wamsaidie kumwepusha na vishawishi pale inapowezekana. Baadhi ya vishawishi hivyo ni kama vile kupewa na fedha nyingi za matumizi kuliko uhitaji wa lazima, kusoma magazeti mabaya, kuangalia mambo ya ngono, kuzurura ovyo bila kupewa kazi nyumbani n.k. Tukumbuke kuwa wazazi nasi tuko duniani, tunaweza kuelewa ni nini mtoto anakabiriwa kama jaribu kwake? Kwa wakati huo tukatafuta namna ya kumsaidia. Tusijaribu kujifanya hatuelewi au tuko sahihi wakati wote, bali tufahamu kwamba Mungu ndiye msaada wetu na nguvu yetu, na mwenye kutushindia katika mambo yote. 
Rum. 8:37, Filipi 4:13: “Lakini katika mambo yote tunashinda na zaidi ya kushinda kwa yeye aliyetupenda” na tena: “Nayaweza mambo yote katika yeye (Mungu) anitiaye nguvu”.
Tunaishi katika dunia iliyoharibika na adui anatafuta kila njia ili kuharibu watoto na kukandamiza mawazo na matendo yao kuelekea kwenye upotovu. Tuzijue nyakati za mwisho, ambapo Neno la Mungu linasema: “Siku za mwisho, kutakuwepo nyakati za hatari. Watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu …” (2Timotheo 3:1-5)
Tusiwaache watoto wetu wakaangamia na mambo ya nyakati hizi za mwisho kama vile hatuhusiki. Mungu ametuweka kwa makusudi maalumu na yuko tayari kufanya kazi pamoja nasi katika hali hii, ili watoto wetu wanusurike na janga hili, wapone, na twende nao mbinguni. Hivyo lipo tumaini.
Neno lasema katika Warumi 8:28: “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake”. Na tena asema katika 1Petro 2:9: “Ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu … Ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu, mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema”.
Katika Isaya 54:13,14 Bwana asema hivi: “Na watoto wako wote watafundishwa na Bwana; amani ya watoto wako itakuwa nyingi. Utathibitika katika haki, utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa, na mbali na hofu, kwa maana haitakukukaribia”. Mungu anasema: “Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, nisije nikaipiga dunia kwa laana”. (Malaki 4:6)
Hivyo basi, tusiruhusu watoto wetu wafanye mambo tu wanayojisikia, ati kwa sababu jamii inayotuzunguka inafanya hivyo, lakini tujijue tuna wajibu mkubwa mbele za Mungu juu yao, na Mungu anathamini mchango wetu kwa watoto na anaangalia kwa karibu sana jinsi tunavyowatendea maana ni mali yake nasi tu mawakili wake tu.
“Bwana akasema, ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu (watoto) posho kwa wakati wake? Heri mtumwa (Mzazi) yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo”. (Luka 12:42,43)
“Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu, roho ile itendayo dhambi itakufa”. (Eze.18:4)
“Wana wetu na wawe kama miche waliokua ujanani. Binti zetu kama nguzo za pembeni zilizonakishwa kwa kupamba hekalu”. (Zaburi 144:12).

BAADHI YA MAKOSA 11 YANAYO FANYWA NA WAZAZI KATIKA MALEZI YA WATOTO 


1. Upendeleo kwa watoto. Upendeleo huwa unawagawa watoto katika familia. Kwa mfano, mzazi anasema kwa kuwa wewe unafanya vizuri darasani wewe ndio wanangu na wengine ni watoto wa nani? Au kwa kuwa wewe ni mtoto wa kiume basi wewe ni wa kwangu na watoto wa kike ni wa mama. Upendeleo unaanza kuwaathiri watoto kisaikolojia wanakufa taratibu na kuanza kuona duniani siyo sehemu salama ya kuishi. Kuna watoto wale wanaolelewa na ndugu au walezi wengine wanakuwa wanachukuliwa kama siyo sehemu ya familia ya watoto hivyo wanawanyima haki ya malezi bora. Wazazi mnatakiwa kuamka juu ya hili na kuoka vilio vya watoto.
2. Kuwatukana hovyo watoto; yaani kuna watoto wanapitia wakati mgumu katika maisha sana wazazi wao kabisa wanawatukana matusi ya kila aina ambayo hata mtoto hastahili kuyasikia. Watoto wanatukanwa matusi ya ajabu hatimaye anakua na kuona matusi ni sehemu ya maisha yake hivyo anakwenda naye kujenga jamii iliyo mbovu. Tokea mtoto yuko tumboni anasikia tu matusi jinsi mama yake anavyotukana bila hata ya kuona soni. Kwa mfano matusi kama mbwa,paka wewe, kichwa kama cha shangazi yako na mengine mengi tu. Jamani wazazi hayo matusi hayawajengi watoto bali yanawabomoa tumia muda huo kumfundisha mtoto au hata kumwambia mwanangu Fulani nakupenda huwenda mtoto akafarijika kuliko matusi.
3. Kuwapiga watoto kwa hasira. Kama tunavyojua kuwa falsafa ya hasira ni hasara. Mzazi unakuta amekwazika katika shughuli zake basi anaona hasira zake azimalizie katika kumpa mtoto mapigo yasiyostahili na hatimaye kumuumiza vibaya. Epuka kumpiga mtoto unapokua na hasira zako bali pumua kwanza hata kwa dakika tano kwani hutojutia maamuzi yako.
4. Kutowajali na kuwathamini. Imekuwa ni desturi watoto wa familia zingine wazazi hawawajali watoto kabisa yeye anajijali yeye kwanza. Kwa mfano, mtoto anaweza kudaiwa ada shuleni lakini mzazi anaona ni bora atoe hata ada nusu ili apate hela ya kunywa pombe. Au wengine wanakula ada za watoto na hatimaye wanafukuzwa shule. Ni bora kutokuzaa kuliko kuzaa na kuja kuwapa watoto shida duniani. Mzazi ni haki yako kumpatia mtoto mahitaji yake yote ya msingi. Mthamini mtoto kwa kumjali hata kuvaa mavazi nadhifu nay a kupendeza.
5. Kumwachia jukumu la malezi msaidizi wakazi. Hili ni tatizo katika zama hizi mzazi anajua kuzaa na kumwacha mtoto akilelewa na dada wa kazi. Kwa namna hii mtoto atawezaje kupata upendo wa mama? Kwanini unamlea mtoto kama watoto wa chupa? Hata kama una kazi hakikisha unapangilia muda wa kukaa na mtoto au watoto na kuwapa malezi bora. Acha tabia ya kumwaachia dada wa kazi kila kitu. Mtoto akiharibika unaanza kulalamika bila kujua wewe ndio kiini cha kosa.
6. Kutowafundisha watoto falsafa ya imani ya kidini. Katika karni hii 21 wazazi wengi wanaiga kuwalea watoto malezi ya kidigitali yaani malezi ya kwenye mitandao ya kijamii na kwenye tamthilia nakadhalika. Mzazi anakumbatia mambo ya kidunia na kusahau kumfundisha mtoto falsafa ya dini. Dini ni falsfa nzuri ya kiimani katika malezi ya watoto. Mtoto ukimlea katika misingi ya kidini ni faida kubwa kwako na kwa jamii nzima. Kumlea mtoto kidunia ni hasara kubwa kama vile unafuga nyoka siku yoyote atakung’ata tu.
7. Kutowasimamia katika masomo yao. Watoto wanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wazazi wao ili kuweza kufika pale wanapotaka. Wazazi mnatakiwa kuacha tabia ya kuwaachia walimu kila kila katika mambo ya darasani. Kuwa mwalimu wa kwanza kwa mtoto wako hakikisha unamkagua na kujua nini amajifunza kila siku na kumsaidia kazi za nyumbani. Wasimamie siyo kuwaua watoto kwa kuwaachia uhuru wa kuangalia tv na kusahau masomo yake muhimu.
8. Kutowapa watoto muda. Hakuna zawadi kama muda ambayo unaweza kumpatia mtoto na akahisi unampenda. Kisaikolojia mtoto anafurahi mzazi anapokua naye anahisi unampenda na unamjali. Changamoto ya watoto siku hizi ni wazazi kutowapatia watoto muda wa kukaa nao. Mzazi anawahi kuondoka na kuchelewa kurudi. Hata kama kuna kitu anataka kukuambia na kugundua kipaji kwa mtoto unashindwa kabisa. Acha kuua kipaji cha mtoto na kutompatia muda wa kukaa naye.
9. Kuwakosoa na kutowasikiliza. Kukosolewa ni kwa mtoto ni kumdoofisha kiakili kabisa. Mtoto anatakiwa kusikilizwa na kutiwa moyo na kumpa faraja katika kitu alichofanya. Kukosea siyo kushindw bali kufanya makosa ndio mwanzo wa kujifunza. Usimkosoe mtoto vibaya bali mtie moyo na kumuonesha njia sahihi ya kupita ni ipi ili aweze kufika. Huwezi kuwa mtaalamu wa kitu Fulani bila kufanya makosa. Makosa ni sehemu ya kujifunza.
10. Kuwalaani watoto. Wazazi wageuka kuwa laana kwa watoto wao na siyo Baraka. Mzazi anamlaani mtoto wewe huwezi kufanikiwa. Wewe huwezi kufanya chochote yaani anamjengea mtoto vizuizi vya kutotimiza ndoto yake. Kwa mfano, wewe utaweza wapi wewe ni wa kufeli tu, kama Fulani alifeli wewe ndio utaweza? Maneno ni mabaya sana yanamuuza mtoto moyo kabisa na kumkatisha tamaa na kumjengea hofu ya maisha.
11. Kuwalalamikia na kuwalaumu watoto. Watoto wanalaumiwa na wazazi wao na kulalamikiwa badala ya kuoneshwa njia ya kupita. Mzazi ni mtu wa kulalamika na kulaumu tu juu mtoto. Hakuna hata siku mzazi aliwahi kusema badala ya kwenda kule pita njia hii ndio sahihi. Huwezi kuwajenga watoto kwa kuwajengea msingi wa kulaumu na kulalamika kila wakati. Unamlamikia mimi nahangaika na kusomesha na kulisha sasa kumsomesha na kulisha ni haki ya nani kama siyo mzazi? Usilalamike katika kutimiza wajibu wako bali furahia majukumu. Watoto wanataka kupatiwa kama wewe ulivyopatiwa siyo kueleza changamoto zako


Makosa 15 ya Kuepuka Katika Malezi ya Watoto



Swala la malezi ya watoto ni swala nyeti, pana, gumu, na lenye changamoto nyingi; hivyo linahitaji umakini mkubwa na maarifa stahiki.
Kutokana na umuhimu huu basi, ni wazi kuwa changamoto au matatizo mengi ya kimalezi yanayotokea kwenye maisha ya watoto yanatokana na makosa yanayofanywa na wazazi katika malezi.
Pamoja na kwamba hakuna kanuni ya malezi, lakini yapo makosa ambayo wazazi wanapaswa kuyaepuka katika swala la malezi ili kuhakikisha watoto wao wanakuwa katika maadili na misingi sahihi.
Karibu nikufahamishe makosa 15 ambayo kila mzazi au mlezi anatakiwa kuyaepuka katika malezi ya kilasiku ya watoto.

1. Kumfurahisha mtoto

Kumfurahisha mtoto ni muhimu kufanywa na kila mzazi au mlezi, lakini ni lazima kuwe na kiasi. Wazazi wengi wamekuwa wakifanya kosa la kutaka kuwafanya watoto wao wafurahi kwa kila kitu. Mtoto akitaka hiki anapewa au akitaka kufanya hivi anaruhusiwa alimradi tu awe na furaha.
Kwa kosa hili unatengeneza mtoto ambaye hatokuja kuambilika mbeleni; atakuwa huku akifahamu kuwa kila anachokitaka ni lazima akipate na kikubaliwe.

2. Kumwabudu mtoto

Watoto wameumbwa na Mungu kupendwa na si kuabudiwa. Mtoto akifahamu kuwa unamwabudu, atakuendesha na kamwe hatokutii kwani anafahamu kuwa yeye ndiye anayetawala moyo wako.
Pia si vyema kumwabudu mtoto kwani mara apatapo shida kama vile kifo, utakuwa kwenye hali mbaya kwani imani na moyo wako wote uliuweka kwake.

3. Kujadili na kudharau wazazi na watoto wengine

Kuna wazazi wana tabia ya kuwajadili na kuwadharau wazazi na watoto wengine mbele ya watoto wao. Hili ni jambo baya sana kwani linawajengea watoto tabia ya dharau na kuwasengenya watu wengine.
Tambua mtoto ni sawa na karatasi nyeupe inayoandika mambo mbalimbali; hivyo unapoonyesha tabia mbaya mbele ya mtoto ataishika moja kwa moja.

4. Kuwafundisha kuishi kwa sheria

Kuna familia nyingine ukifika utafikiri ni kambi ya jeshi; watoto wanaishi kwa sheria kali na ngumu. Kuwalea watoto kwa sheria hakuwafanyi kuwa bora bali huwafanya waigize nidhamu na pindi wawapo nje ya nyumbani watavunja sheria zote.
Nimeshuhudia watoto waliowekewa sheria ya kutokunywa pombe au kuvaa nguo za ovyo nyumbani, lakini wawapo nje ya nyumbani huvunja sheria hizo hadi kupitiliza.
Ni muhimu ukamsaidia mtoto kutambua yeye mwenyewe umuhimu wa kuishi katika maadili kwa ajili ya badaye yake na si kumlazimisha kuishi kwa sheria.

5. Kuwalazimisha kushika imani kwa nguvu

Hakuna mzazi asiyependa mtoto wake awe mtu wa imani. Lakini tatizo linakuja juu ya ni kwa njia gani wazazi wanawawezesha watoto wao kushika imani.
Mzazi anapomlazimisha mtoto kushika imani, moja kwa moja mtoto ataiacha imani hiyo atakapokuwa mbali na mzazi; ni muhimu kumfanya mtoto atambue umuhimu wa imani yeye wenyewe na si kwa kumlazimisha. Hata hivyo unaweza kufanya haya yafuatayo kama mzazi:
  • Kuwa mfano wa kuigwa katika imani. Usimlazimishie imani ambayo wewe mwenyewe huna.
  • Mwonyeshe faida za kuishi kwenye imani.
  • Mwonyeshe athari za kuishi bila imani.
  • Mpe rasilimali zote zinazohitajika katika imani.
  • Fanyeni matendo ya kiimani pamoja katika familia (Kuomba, kusoma maandiko ya imani yenu, kujadili kwa pamoja maswala ya imani n.k.).
  • Mpongeze pale anapofanya jambo zuri la kiimani.
Kwa njia hii mtoto wako atakuwa katika misingi bora ya imani ambayo hataiacha.

6. Kutokuwa na muda wa kuwasikiliza

Wazazi wa leo kwa lugha ya mtaani wako “bize” kutafuta pesa na hawana muda na watoto. Ikumbukwe kuwa watoto nao wanahitaji kusikilizwa.
Mara kadhaa umewahi kusikia watoto waliojiua au kujidhuru kutokana na kuwa na matatizo ambayo walikosa mtu wa kumweleza. Hakikisha hata kama una shughuli nyingi kiasi gani hukosi muda wa kukaa na kumsikiliza mtoto wako.

8. Kugombana mbele ya watoto

Kuna wazazi wasiokuwa na staha kabisa, wao hutukanana na hata kupigana mbele ya watoto wao. Mtoto anapoona wazazi wakitukanana na kupigana, huiga tabia hiyo na kwenda kuifanya kwa wenzake na hata kwenye ndoa yake ya baadaye.
Ukiwa kama mzazi unayempenda mtoto wako, basi hakikisha tofauti zenu mnazimaliza kwa hekima na busara, tena ikibidi chumbani kwenu ili watoto wasipate mbegu mbaya kutoka kwenu.

9. Kuruhusu utamaduni wa kimagharibi uwatawale

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameingia mpaka kwenye swala la malezi. Wazazi wengi wa karne ya 21 wameruhusu watoto wao  kutawaliwa na utamaduni wa kimagharibi.
Kwa mfano unamwekea mtoto televisheni yenye chaneli za kiasasa ua unamruhusu kutumia intaneti ya kawaida ambayo haijachujwa kwa ajili ya watoto. Ni wazi kuwa mtoto atajifunza tabia za ajabu ajabu kutoka kwenye tamaduni za kimagharibi zilizoporomoka.
Hata hivyo unaweza kufanya haya yafuatayo:
  • Usiruhusu mtoto wako kutumia televisheni au mtandao kwa muda mrefu.
  • Tawala chaneli na vipindi ambavyo mtoto wako anavitazama.
  • Tawala intaneti ya mtoto. Unaweza kumfungulia mtoto injini pekuzi (search engines) kama vile http://www.kidrex.org/ na https://www.kiddle.co/ ambazo zinachuja maudhui salama kwa watoto.

10. Kuwa mkatili kwa mtoto

Naamini mara kadhaa umewahi kusikia mzazi amempiga mtoto hadi kufa au kumfanyia ukatili mwingine kwa kigezo tu kuwa mtoto amekosea.
Ni vizuri ukafahamu kuwa mtoto huonywa kwa hekima na upendo ili atambue kosa lake na afahamu kwanini ameadhibiwa ili asirudie kosa tena.
Kumfanyia mtoto ukatili kama vile kumchoma, kumkata, kumkanyagakanyaga, kumnyima chakula n.k. Humfanya akue katika hali ya kuwa mkatili au mwenye utu wa ndani ulioathirika.

11. Kumfanyia mtoto kila kitu

Wazazi wengi hufanya kosa la kumfanyia mtoto kila kitu kwa kuamini kuwa ndiko kumhudumia vyema. Watoto huwekewa wahudumu au waangalizi hata zaidi ya mmoja, ili tu wasipate shida.
Ni muhimu mtoto akajifunza kufanya baadhi ya vitu hata kama kuna mwangalizi; mtoto ajifunze vitu kama vile kuoga, kufua, kufagia na hata kupanga vitu katika chumba chake. Kwa njia hii utalea mtoto anayewajibika.

12. Kutokumfundisha mtoto kujiandaa kwa baadaye

Ni lazima mtoto afahamu kwanini anatakiwa kusoma, kulinda afya yake, kutumia pesa vizuri n.k. Wazazi wengi wanafikiri kuwa watoto watajua tu mambo haya wenyewe moja kwa moja siku za mbeleni.
Hili ni kosa ambalo huwafanya watoto wa wazazi wengi hasa wenye pesa kutokuandaa baadaye zao. Wao hufikiri wamezaliwa kutunzwa na baba na mama hadi mwisho wa maisha yao.

13. Kutokutawala ulaji wa mtoto

Ni jambo la kusikitisha kuona mtoto anapata maradhi ya shinikizo la damu kutokana na ulaji mbaya. Wazazi wengi wenye pesa huwapa watoto wao mlo bora kupita kiasi, jambo ambalo huathiri afya za watoto.
Pia wazazi wengine huwazoesha watoto wao vitu kama vile biskuti na pipi ili kuwafurahisha. Jambo hili limewasababishia watoto wengi kuoza meno au hata kuwa wezi wa fedha ili wanunue vitu hivyo.

14. Kutokumfundisha mtoto elimu ya jinsia

Swala la jinsia lipo na haliepukiki; mtu anayeweza kufahamu vyema maswala ya kijinsia ya mtoto ni mzazi. Watoto wengi hufundishwa elimu ya jinsia na marafiki zao shuleni, jambo linalowafanya wapate elimu potofu.
Hivyo ukiwa kama mzazi unayejali baadaye ya mtoto wako, ni vyema ukatenga muda ukazungumza naye kuhusu maswala ya kijinsia.

15. Kutokuheshimu hisia na utu wake

Mtoto ni binadamu kamili mwenye utu na hisia ambavyo vyote vinatakiwa kuheshimiwa. Wazazi wengi hufanya kosa la kutokujali kuwa watoto wao wamechoka, hawana furaha au hata kujali wanapokuwa na changamoto mbalimbali.
Ni muhimu pia wazazi waepuke kuwakaripia au kuwakemea watoto wao mbele ya watoto wengine, kwani kwa kufanya hivyo huwafanya wajisikie duni.
Hitimisho
Naamini umeona wazi jinsi suala la malezi lilivyo pana na gumu. Lakini naamini kwa kuepuka makosa tajwa hapo juu, moja kwa moja wewe kama mzazi utaweza kumlea mtoto wako vyema.

Hakikisha unahusisha imani na juhudi zako zote katika malezi, kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

HUDUMA ZA MAZISHI

Huduma ya Mazishi  (Mchungaji, mzee wa kanisa, au shemasi anaweza kufanya huduma hii). Ushauri umetolewa kwamba, kadiri inavyowezekana, maz...