Jumapili, 28 Januari 2018

KAYA NA FAMILIA



KUWAACHA WAZAZI NA KUWA MWILI MMOJA



NENO LA LEO: Mwanzo 2:24

“Kwa hiyo mwanamume atamwacha Baba yake na Mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja”

TAFAKARI:

Kati ya matatizo yanayochangia Ndoa nyingi kutokuwa na AMANI ni swala la Wanandoa kutowaacha wazazi wao. Ni kweli damu ni nzito kuliko maji, lakini Mungu anatoa agizo la wanandoa kuanzisha himaya yao. Magomvi tunayoyashuhudia kati ya – Mawifi, Mama mkwe, wakamwana, Mashemeji na Baadhi ya wanandoa, yanatokana na kutoelewa agizo hili. Agizo la kuwaacha wazazi lina maana kubwa, baadhi ni hizi:





1. Wanandoa wasianzie maisha kwenye kaya za wazazi wao, yaani wasiishi na Familia za wazazi wao. Wanapaswa kuanzisha himaya yao, yenye uhuru kamili wa maamuzi juu ya maisha yao.





2. Ndugu wasaidiwe, lakini wasipewe nafasi ya kiutawala, kuna mashemeji wanatoa Amri utafikiri ni nyumbani kwao. Mke ameolewa na mmoja, athaminiwe, mara nyingi akina Dada (Mawifi), wanaona wivu kwa kila kitu anachofanyiwa wifi yao, wanaume wanatakiwa kuwa na Msimamo juu ya wake zao, Mke ni Ubavu na ni mwili mmoja.




3. Siri za Mke na Mume zisitoke kwenda kwa Ndugu, labda kwa makubaliano inapobidi. Kuna wanandoa hawatulii, kila jambo lazima liende kwa Ndugu. Mara nyingi Dharau zinaanza kwa kutotunza Siri.


4. Inapolazimu kukaa na Wazee- mfano. Mama Mkwe, ni wajibu wa mwanamume kumlinda mke wake, mara nyingi akina Mama wakiwa kwa watoto wao wa kiume wanajitwalia Madaraka, na kujiona ni wa muhimu kuliko wakwe zao, atataka apatiwe mahitaji zaidi au sawa na mkwe wake. Wengine wanataka kufanana hadi nguo za Ndani.


5. Kama mtakaa na Ndugu wa upande wowote, hakikisheni hawaingilii uhuru wenu wa faragha.


6. Endapo kumetokea kutoelewana kati ya wanandoa, usipeleke mashitaka kwa wazazi wako, peleka mashitaka kwa wazazi wa mwenzio. Wazazi wako mara nyingi hawataona kosa lako, hivyo ni rahisi tatizo kutopata ufumbuzi.


Mawifi, Mashemeji, Akina Mama na Baba Mkwe, na wakamwana – Tafadhalini sana waachieni wanandoa nafasi na Uhuru, hao ni mwili mmoja. Wanandoa msiogope mawimbi yakiwapata, Mungu yupo atawashindia Daima, anao uwezo wa kutuliza DHORUBA.



ADUI ANAYETESA FAMILIA



Ujumbe unatoka: Mathayo 5:27-28

Mmesikia kwamba imenenwa, USIZINI; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kutamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.

tAFAKARI:

Wiki mbili zilizopita, Familia mbili ziliingia kwenye misiba ya kusikitisha baada ya Baba wa familia moja na Mama wa familia nyingine kupata ajali ya gari na kufa papohapo wakiwa wanatoka kupeana mapenzi. Mama (marehemu) alikuja likizo, mume na watoto aliwaacha ulaya, na Baba (Marehemu) alikuwa anaishi hapa Dar na familia yake, siku hiyo marehemu hawa walikutana, na wakakubaliana kukumbushia mapenzi waliyokuwa wakipeana wakiwa marafiki kabla ya Ndoa. Shetani hakuwaachia Pumzi, siku hiyohiyo ikawa ya RAHA na mara kugeuka kuwa ya HUZUNI NA MAUTI, “One mistake one Goal”.





Marafiki zangu, kama kuna adui mkubwa anayetesa familia katika vizazi vyote ni Dhambi ya UZINZI, yaani Tendo la Ndoa kati ya watu wawili wasio katika NDOA Halali.Familia nyingi zimesambaratishwa, watoto wanahangaika utafikiri baba kafariki kumbe amesombwa na Kahaba, Familia hazina Furaha wala Amani, Upendo umehamia kwa wenye kunyanyua Chuchu na Makalio ya Mchina. Familia zinapata shida za pesa, huku akina baba wanaitwa mapedeshee, mala ATM, Mabuzi na kila aina ya sifa, bila kusahau Mashugamamiii wanaojituliza kwa vijana.



Kwa bahati mbaya sana, Kila kunapokucha ndivyo Adui huyu mkubwa “ZINAA” anazidi kupata umaarufu katika Jamii, anashabikiwa na kila Mtu, kuanzia watoto hadi vikongwe, maskini hadi wafalme, wapagani hadi kwa manabii na Mitume feki. Ni mara ngapi tumesikia vituko vya kwenye Ma “Guest House” vizito kuibiwa na Machangu Doa, Makanisani wachungaji kula kondoo wao, mashuleni walimu na wanafunzi, na vyuoni ndiyo usiseme, maofisini mabosi na wafanyakazi wao, na zaidi hata kwenye mabasi (daladala) wanavyobanana, unashangaa mwanaume tayariiii (Eti Mfadhaiko). HILO NI PEPO LA NGONO.


Amri ya Saba katika zile Amri kumi inasema “USIZINI” Kutoka 20:14, pamoja na kuhalalishwa na watu wengi, Mungu anasema “Ikimbieni ZINAA. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye ZINAA hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa MWILI wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu akaaye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu” 1Korintho 6:18-20. Kizazi cha NUHU na Sodoma Mungu aliwaangamiza kwa sababu ya huyu adui Mtesaji na Muuaji “ZINAA”.


Wapendwa tendo la Zinaa ni sawa na Kulamba Sukari iliyotiwa SUMU, na wengi hawajui hilo, hatimaye wanaishia kwenye maisha ya Majuto na Kukata tamaa kama sio kifo, na hatimaye Jehanamu ya Moto. Wengi wanadai huwezi kuishinda Zinaa, ni kweli, hata Yesu alisema “Mimi ni Mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; MAANA PASIPO MIMI NINYI HAMWEZI KUFANYA NENO LO LOTE” Yohana 15:5.Ushindi wa dhambi hii ya Zinaa, ni kwa, kuruhusu Roho Mtakatifu akaye ndani yetu, ambaye anaua chembechembe za Virusi vya Dhambi (Tamaa ya mwili) na Kutupatia tabia ya Mungu ndani ya MIOYO YETU, na huku ndiko kuzaliwa UPYA. 




SWALI limeulizwa; je na wewe imepitiwa na huyu adui anayetesa familia? Jibu kwa asilimia kubwa ni Ndiyo, hata kama wewe hujawahi kuanguka kwenye Zinaa, kwa namna moja au nyingine umeyaonja madhara yake, kupitia familia tunazoishi nazo. Wito wangu ni huu, wote walioathirika na jambo hili, Mlango bado uko wazi, Rehema za Mungu bado zipo kutusaidia Kushinda na Kutuvusha salama.




MUME MWEMA

Neno la leo linatoka: 1Petro 3:7
“Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa AKILI; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe”
TAFAKARI:
Kwa asilimia kubwa matatizo yanayotokea katika ndoa chanzo chake ni mwanaume kutojua kuishi kwa akili na Mke wake. Ni kweli kuna wanawake wajinga ambao biblia inasema wanavunja nyumba zao kwa mikono yao wenyewe, pamoja na hayo kama mwanaume ataomba Mungu ampatie Hekima au akili Ndoa inadumu. Kumbuka kila unalotenda kwa mwenzio linazaa tendo la kutendewa likiwa baya au jema. Tatizo likitokea katika ndoa, kaeni chini mtafute chanzo cha tatizo, Mume ana sehemu ya kutumia akili aliyopewa na Mungu kurudisha mahusiano. Hebu tuangalie baadhi tu ya mambo anayotakiwa mwanaume kumtendea mkewe:




MUME AMHESHIMU MKE WAKE: Kuna wanaume wanadharau wake zao, utakuta mke anatukanwa, kupigwa, anakosolewa mbele ya watoto au hata mbele ya watu kama house girl. Mara ngapi tunasikia wanaume wakigomba “Mama Fulani chakula gani hiki mbona ugali haujaiva vizuri?”, lawama hizo mbele za watu au mabinti wa kazi – ni kumuaibisha mkeo, na kwake ni tatizo kubwa. Mke ni tofauti kabisa na watoto au wasichana wa kazi, anatakiwa kupewa Heshima, huyo ni mwenzi wako na mshauri wako. Kufanya Mapenzi na wanawake wengine ni kumdhalilisha mkeo na kwa sababu mapenzi hayagawanyiki lazima matatizo yataanza.




MUME AMJALI NA KUONYESHA UPENDO KWA MKE: Mwanamke ana hisia kali za mahusiano, anabadilika kulingana na anavyotendewa, wakati mwingine wanakuwa kama watoto, unaweza kumdanganya hata kwa kitu kidogo ili mradi kiashirie kumpenda. Siku moja jaribu kununua Pipi, halafu mwambie “sweet” au “Darling” nimekuletea zawadi kubwa, twende nikakupe chumbani, halafu toa pipi huku ukimtazama usoni, utashangaa yatayotokea. Onyesha kuwa unamjali, unamthamini, unampenda na unafurahia ukiwa nae. Hata kama ana kazi yake, Mnunulie nguo rasmi kama zawadi. Neno Pole Mpenzi, Samahani, Umependeza n.k. yana maana sana kwa Mwanamke. Mume awe na muda wa kuongea na Mke wake, kushinda kwenye Mabaa hadi usiku, kuwa busy na TV au Kompyuta muda wa usiku ni tatizo kwa mwanamke. Wanaume wengi wanacheka na kupiga porojo na wanawake wengine maofisini, lakini akifika nyumbani utafikiri ameambiwa yuko mahakamani penye amri ya usipige kelele. 




MUME NI KICHWA CHA NYUMBA: Tangia mwamzo Majukumu ya kutunza familia ni ya Baba, mwanamke ni msaidizi, siku hizi mambo yamegeuka, akina mama ndio wanaachiwa mizigo ya kulea familia, Mke akiwa na kazi au biashara ndio usiseme, Nguo za watoto, chakula, ada n.k. yote anaachiwa Mama. Baba hakikisha unaacha fedha za kutosha nyumbani, wengi wanapenda chakula kizuri huku wanaacha fedha za fungu moja la mchicha, na wengine wanakula vizuri wakiwa kazini – Supu, Biliani, Pilau mbuzi, Juice – familia nyumbani ni maharage wakibadilisha Mchicha.




MPATIE HAKI YAKE YA NDOA: Ni wajibu wa Mume kumtimizia mkewe hitaji la Ndoa, jambo hili siku hizi limekuwa tatizo kubwa. Wanaume wengi WANABAKA wake zao, kwa maneno rahisi ni kwamba wanafanya tendo la ndoa kutimiza wajibu sio kwa ajili kupeana mapenzi. Utakuta mwanaume anaparamia tu wala hakuna maandalizi, siku nzima wameshinda hawaongei, usiku ukifika ni Amri za Jeshi “SIMAMA JUU, KULIAAAA GEUKA, MGUU PANDE, MWILI LEGEZA” hizo kwa mwanamke ni Karaha au Adha badala ya Raha. Wanaume wengi ni wabinafsi katika swala hilo, wanajali kutimiza haja zao, kuna akina mama hawajawahi kufikishwa mwisho wa Raha, japo kila siku wanatoa huduma. Hili jambo linahitaji elimu ili kila mmoja aone furaha ya Ndoa.



UPENDO NA UTII KATI YA WANANDOA



Neno la leo linatoka: Waefeso 5:25
“Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake”
TAFAKARI:
Mara nyingi wanandoa wanapofarakana utasikia Mume anasema mke wake hamtii, na mwanamke anadai mume wake hampendi, sasa nani anatakiwa kuanza? Kutii au kupenda! Kabla sijaanza kuongea juu ya sifa za Mume mwema, nitaanza kueleza falsafa ya Maneno haya mawili “Kupenda na Kutii” yanavyohitaka kutumika katika Ndoa.


UPENDO WA MWANAUME: Upendo wa kweli kwa mwanaume juu ya mke wake, ni ule tu unaojengwa na Mungu, wengine wanasema, hauna sababu, ndio maana utakuta watu wanaulizana hivi huyu mume amempendea nini?. Adam alipatiwa mke na Mungu, alichukuwa ubavu wake akamfanya Hawa, alipopelekewa AKAMPENDA. Hivyo upendo wa kweli wa Mume kwa Mke wake, huanzishwa na Mungu, ndiyo maana Paulo anamfananisha Mwanaume, kama Kristo alivyolipenda Kanisa. Wanaume wengi siku hizi hawapendi ila wanatamani au kupenda vitu Fulani. Mfano: Wengine wanapenda Makalio bila kujua kuna ya Mchina, wengine “Figure eight”, wengine Maziwa yaliyosimama – mama akianza kunyonyesha Upendo kwisha, upendo wa namna hiyo ni wa kitambo, ndoa nyingi zinaanza na upendo huo, baada ya muda mfupi Ndoa inakuwa Karaha.


UTII WA MWANAMKE: Watu wengi kwa kutokuwa na elimu ya Biblia, wametafsiri neno hili vibaya hasa wanaume. Ukisoma biblia ya lugha ya Kiingereza na lugha zingine za asili ya waandishi wa Biblia, utii wa mke kwa mume ni tofauti na utii wa Mtoto kwa wazazi au watumishi kwa Bwana zao. Utii wa Mke kwa Mume unaitwa “SUBMIT” wakati Utii wa Mtoto au watumishi unaitwa “OBEY”. Soma biblia ya kiingereza – KJV “Waefeso 5:22, 6:1, 6:5”. Wives are supposed to SUBMIT themselves to their Husbands, while children are supposed to OBEY to their parents. Mwanamke anatakiwa KUJISALIMISHA kwa Mumewe kwa UPENDO akiamini juu ya UPENDO wa mume wake, anakubali kuwa ubavu au msaidizi wa mumewe. Wanakuwa mwili mmoja. Ukiona mwanamke kawekewa Sheria nyumbani na anatakiwa kutii kama mtoto, huo sio mpango wa Mungu, na ndoa lazima itaishia kuwa Jela Ndogo – Jambo hili ni pan asana linahitaji hekima ya Mungu kulielewa na kulitenda.


Ukielewa falsafa hiyo, mwanaume hatadai mwanamke amtii kwanza ndipo ampende, Mungu angefanya hivyo, Kristo asingekuja kutukomboa tungali wenye dhambi, alitupenda tungali wabaya. MUME MPENDE MKEO, MLEJEZE KWA UPENDO KAMA KRISTO ANAVYOTUTENDEA.



MKE MWEMA



NENO LA LEO LINATOKA: Mithali 14:1
“Kila mwanamke aliye na Hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu hibomoa kwa mikono yake mwenyewe”
TAFAKARI:
Kuna mithali isemayo “MAJUTO MJUKUU”, ni kawaida kwa wanandoa kuangalia na kulaumiana juu ya matatizo yanayojitokeza, badala ya kutafakari chanzo cha matatizo. Matatizo mengi ya ndoa yanatokana na wanandoa kutokuwa na elimu ya ndoa na kutofuata ushauri wa Mungu aliyeanzisha Ndoa. Baadhi ya sifa za Mwanamke mwenye Hekima – Pia Soma Mithali 31:10-31.


1. Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema I katika ulimi wake (31:26). Wanawake wengi hawajui kuutumia ulimi vizuri – Ukali, maneno ya mikato, matusi, ukaidi n.k. kwao ni mambo ya kawaida. Wengi wanatawaliwa na HASIRA na WIVU, akiona mumewe anacheka na mwanamke ni Kosa la jinai, mwanamke anafura wala hata hawezi kuongea, hali ya hewa inabadilika hata paka nyumbani wanatambua kuwa hali ni Mbaya.


2. Hufanya kazi kwa Moyo na Huamka alfajiri na mapema
Kuna wanawake ambao ni wavivu kupindukia, inafika wakati hata kutandika kitanda anamtuma House Girl, wanaume ni rahisi sana kuvutwa na anayemhudumia kwa ukaribu, House girl akiandaa chakula, mara kitanda, mara maji ya kuoga, mara apige deki chumbani n.k. Haichelewi mwanaume kulipa fadhila kwa wema anaotendewa.


3. Ni msafi na anajua kuandaa mavazi yanayofaa kwa familia yake
Kuna wanawake ambao ni wachafu – usishangae kukuta sufuria kwenye makochi, chumba cha kulala ni stoo ya nepi za mikojo na nguo chafu, wengine kuoga ni anasa. Mwanamke ni MAJI, sharti mwanamke awe msafi muda wote. Wanaume wote wanapenda Usafi, marashi hata ya mchina yasikose, Mwanamke hakikisha “Reception” inakuwa Safi na kuwa katika hali ya kumfanya Mume ajisikie kujipumzisha kwa Raha mstarehe.


4. Jali na timiza Mahitaji ya NDOA kwa mume wako
Sulemani anasema mwanamke mwema “Taa yake haizimiki usiku”, kuna wanawake wavivu kwa swala hili, pia kuna wanaopenda kulipa visasi kwa kuwanyima waume zao huduma, utakuta wiki nzima mama apanda kitandani huku amevaa “KOMBATI” utafikiri ni askari anaenda vitani. Wanaume ni sawa na Mbuzi ambao hawachelewi kukata kamba wakikosa majani walipofungiwa. Fanya makosa yote, lakini usijefanya ujinga wa kumkomoa mume kwa kumnyima huduma ya Ndoa, hilo ni kosa la Jinai. Hakikisha huduma hizo zinaboreshwa, nenda na wakati ili mradi isiwe kinyume na taratibu za Mungu.


5. Mwanamke anatakiwa kujua kupika chakula kitamu, ambacho familia itafurahia.
Wanawake wengi hasa wa siku hizi hawajui kupika, ndio maana utakuta wanaume wengi wanaishia kula hotelini au kwa mama ntilie, kama umetoka bara basi usione aibu kujifunza kwa watu wa pwani namna ya kuunga NAZI kwenye chakula. Akina mama ni wajibu wao kujifunza Mapishi, Mchicha peke yake unaweza kuwa na mapishi zaidi ya 10, wanaume wanapenda chakula chenye ladha “Test”, mfanye mume akumbuke chakula cha nyumbani.


6. Mwamini Mume wako, wivu na hisia mbaya ni adui wa ndoa yako. Usitoe siri za ndoa yenu kwa mashoga au ndugu zako. Muda wote muombe Mungu akupatie hekima ya kuongea pindi tatizo linapotokea, Muombee mume wako ili Mungu amsaidie pia awe na Hekima ya kutunza Ndoa kwa Uadilifu na Upendo. 


Mungu awajalie hekima katika maisha ya Ndoa ili Furaha, Amani na Upendo vipate kudumu daima.




MAANA HALISI YA NDOA







NENO LA LEO: Mathayo 19:4-6
“Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe”.


TAFAKARI:
Nikawaida kusikia; heri nisingeolewa au nisingeoa, na wengine hata kama hawasemi kwa maneno lakini mioyoni wanajuta kwanini waliingia kwenye Ndoa, wanatamani kutoka lakini hawawezi. Kitu cha kushangaza ni hiki; wakati wengine wanatamani kutoka katika ndoa, wengi wanatamani kuingia ili na wao wajionee. Na wengine bila aibu wanawaambia vijana "Ndoa ni ngumu mtaiweza?". Kimsingi NDOA sio NGUMU ila wanadamu wanaingia katika NDOA bila kuwa na Elimu ya NDOA.


Leo hebu tuanze kuangalia kuwa, Je! ni mpango wa Mungu Ndoa ziwe na hali ya kukatisha tamaa namna hiyo? kama sivyo, matatizo yanatoka wapi? make utaona vijana wakati wa uchumba walikuwa wanabembelezana zaidi ya Mtoto na Mama, wananyweshana juice huku mmoja amempakata mwenzie, akiwa anamwangalia usoni kwa tabasamu lisilo na mfano, utafikiri wako peponi. Unashangaa baada ya kuoana na kuishi takribani mwaka mmoja, na wengine hata miezi mitatu haipiti, MAMBO YANAANZA KUBADILIKA TARATIBU LAKINI KWA UHAKIKA.


Majibu ya mikato unaanza kuyasikia, makelele na kununiana vinaanza kujitokeza, hata kwenye uwanja wa mpira, mambo yanaanza kuharibika, AMRI kama za jeshi zinaanza kutumika kwenye chumba cha faragha, ni "Mguu pande - Mguu sawa, nyumaaaaaa geuka! mwiliiii legeza !!!!!".Wapendwa! sehemu za kutuliza mawazo zinageuka kuwa KARAHA!. Hali kama hizo zinatoka wapi? na tufanye nini kuepukana na hali hizo? 


Tatizo kubwa ni kukosa elimu juu ya Ndoa na Kutomruhusu Mungu aliyemwanzilishi wa Ndoa kutawala maisha ya wanadoa. Leo naomba uelewe jambo hili: NDOA ni muunganiko wa WATU WAWILI WENYE MAPUNGUFU walioamua kuungana kuwa mwili mmoja. Kwakuwa wengi wanaingia kwenye ndoa bila kujua jambo hili wanapata shida wanapoanza kuona tabia za wapenzi wao zikibadilika. Mara nyingi TABIA huwa hazibadiliki, ila ni Tabia za ASILI ambazo Zilikuwa sio rahisi kuonekana wakati wa uchumba, ni Mungu peke yake aliyekuwa anajua madhaifu hayo. Zingatia kuwa Hujaoa au hujaolewa na Malaika, kila binadamu aliyezaliwa katika ulimwengu wa Dhambi ana Mapungufu ambayo - Ni Mungu pekee anayeweza kuwafanya wana NDOA kuchukuliana, ndani ya UPENDO wa KWELI unaotokana na Mungu mwenyewe. 


Hesabu ya 1 + 1 = 1, Ni ngumu kuielewa kibinadamu, hesabu hiyo ukifanya kibinadamu lazima utatoa jibu ambalo ni 2, kwa upande wa Mungu jibu hilo ni KOSA. Hiyo ndiyo shida Mambo ya Mungu tunataka kuyatolea Majibu kwa kutia akili zetu, tutakwama tu. Hebu Mungu atusaidie kutupatia uwezo wa kutambua maana ya NDOA, ili ndoa zipone. Kwa leo naishia na utangulizi huu mfupi - Tutaendelea siku zijazo, usije ukakosa mada hizi, kwani MUNGU yupo kwa ajili ya kutusaidia.



NDOA IHESHIMIWE



 Ebrania 13:4
“Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu”
TAFAKARI:
Kama kuna bidhaa adimu katika maisha ya siku hizi, ni HESHIMA KATIKA NDOA. Wana ndoa asilimia kubwa hawaheshimiani, lakini pia hata watu wa nje hawaheshimu Ndoa za wenzao.


Utasikia matusi ya nguoni yakirushwa kati ya wanandoa mbele za watoto, magomvi ya usiku yasiyokoma, kunyanyasana, dharau, maneno ya mikato, kununiana n.k. yote hayo ni kukosa heshima katika ndoa.


Mawifi, mashemeji, akina mama mkwe n.k. tunashuhudia wakianzisha tafrani katika ndoa za ndugu zao. Bila kuwasahau wanaowasha mapenzi kwa waume au wake za watu. Hayo yote ni kuvunja heshima ya ndoa. Mithali 5:15 inasema “Unywe maji ya Birika lako Mwenyewe”. Uliona wapi watu wanapokezana vijiko wakati wa kula? Huo sio ustaarabu na kukosa HESHIMA.


Sehemu nyingine inayopaswa heshima ni chumbani, sehemu pekee ya kupumzisha akili na kupata furaha ni wakati wa faragha. Wapendwa leo kuna kesi nyingi na matatizo mengi ya wanandoa, hata magonjwa, yanayotokana hapo chumbani. Wengi vyumba vyao vimegeuka kuwa KARAHA, ni amri kama jeshini, ndio maana hata madereva wa magari wanalazimika kwenda Shule, angalia madereva taxi wengi wako “very rough” na gari zao hazidumu.
Pia sharti wanandoa wakumbuke kuwa kila kiungo cha mwili kiliumbwa kwa kazi maalumu, ndio maana hatujawahi kuona wanyama wanafanya tendo la ndoa kinyume na maumbile, mambo hayo athari zake ni kubwa. Hebu, UPENDO NA AMANI vitawale katika viwanja vya FARAGHA. 



HASIRA HASARA - KATIKA NDOA

Ujumbe unatoka: Waefeso 4:16 
“Muwe na HASIRA, ila msitende dhambi; Jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka”
TAFAKARI:
Asilimia kubwa ya NDOA za siku hizi hazina AMANI, utasikia mama anasema heri nisingeolewa, na wakati mwingine Baba anafikiri alikosea, huenda huyo mwanamke halikuwa chaguo sahihi. Wanasahau kuwa wakati wa uchumba na hatimaye “honey moon” (Fungate), walikuwa wakipakatana wakilishana na kunyweshana Juice. Lakini leo watu wanalala huku wanaomba usiku uishe haraka.


Leo tunatafakari juu ya HASIRA na Kuwa na machungu moyoni, Kuna watu wanahasira za Kijinga, utakuta mtu amefura hawezi hata kuongea. Lakini ukifuatilia utakuta KOSA ni dogo, mfano: Mwanamke anamuona mume wake anacheka na mdada anayefanya naye kazi. Moja kwa moja wazo linamtuma kuwa anaibiwa, Mara mama anaanza kununa, inafika usiku Mama anapanda kitandani na NGUO utafikiri ameambiwa ajiandae kukimbiza mwizi usiku. Na mwanaume akiona adhabu inazidi, siku ya kwanza, ya pili, ya tatu, wiki - anaanza kuzungusha macho barabarani utafikiri “WIPER” za Isuzu. Unashangaa Mama anaanza kuvaa kanga za Mafumbo “Utazunguka kila Bucha Nyama ni ileile” na utakuta Baba wala hana habari ya Kusoma maneno ya Kanga. Mwisho wa yote NDOA inaishia kuwa Jera ndogo ambayo, Upendo, Furaha na Amani vinabaki kuwa historia.


Wapendwa, hasa wenye ndoa changa, jueni kuwa, Ndoa ni Muungano wa watu wawili waliodhaifu, walioazimia kuishi wakichukuliana na kusaidiana. Tatizo sio kukosewa au kukwazwa, shida kubwa ni namna ya kuchukuliana hasa mwenzio anapokukosea. Kumbuka mwanadamu yeyote sio mkamilifu “SIO MALAIKA”, hivyo kukoseana lazima kutatokea, na SHETANI anaitumia hali ya kukoseana vizuri, atakuletea hisia mbaya na kukujaza hasira na Machungu Moyoni ambayo madhara yake ni SUMU YA NDOA. Katika hali zozote unapoona umekosewa, omba hekima kwa MUNGU atakupatia njia nzuri ya kulitatua tatizo kwa AMANI, waswahili walisema “HASIRA - HASARA”. Mungu anasema "Hasira hukaa kufuani mwa wapumbavu" Mhubiri 7:9 


ADUI WA NDOA YAKO



UJUMBE UNATOKA: Warumi 16:19-20
“Maana UTII wenu umewafikilia watu wote; basi nafurahi kwa ajili yenu, lakini nataka ninyi kuwa wenye HEKIMA katika mambo MEMA, na wajinga katika mambo mabaya. NAYE MUNGU WA AMANI ATAMSETA SHETANI CHINI YA MIGUU YENU UPESI…..”
AFAKARI:
Baada ya kufanya uchunguzi, imebainika kuwa kadri tunavyoendelea kuishi, kati ya ndoa 100, ndoa 95 zinapitia changamoto za Migogoro ambayo mwisho wake ni kuachana, na hata kama hawajapeana talaka, basi wanaishi kwa matumaini. Yaani wanaomba lolote litokee ili waondokane na Adha ya maisha ya Ndoa. Utakuta watu wanatembea Barabarani wanaongea peke yao, au wanafika maofisini wakiwa na MALUWELUWE “Upset Minded”.


Wapendwa kuna adui wa Ndoa yako, anayekuonea wivu unapokula Maraha na mpenzi wako, kila wakati anapanga njama namna ya kulihujumu Penzi lenu – naye ni SHETANI. Hata kama ndoa yako haijawahi kupitia migogoro, jua huyu adui anaipigia mahesabu, siku moja utashangaa mambo yamebadilika, Kitanda cha futi sita kitakuwa kama Mahabusu. Mwingine utasikia ansema, mume wangu siku hizi ni USINIGUSE. Hii ndiyo kazi ya Huyu adui, kuleta huzuni sehemu ya Furaha, kama alivyoleta kwa wazazi wetu wa Kale ADAM na HAWA. Ukiona tatizo limeingia, usihangaike kutafuta mchawi au kumuona mwenzio ni Mbaya, wala usitafute kulipa kisasi – Dawa ni kupeleka shitaka kwa Mungu, Mwenye uwezo wa KUMSETA (TO CRUSH) yaani kumharibu Shetani.


Mama mmoja alikuja analia, macho mekundu, nikamuuliza nini kimemsibu, kumbe mume wake anatembea na shoga yake, na mwishowe akaamua kuhamia kabisa. Nilimpa Dawa ambayo hadi sasa anaisifia, Mume amerudi nyumabani. Nilimwambia – Kwanza amsamehe mume wake, kwani kuna adui aliyesababisha hayo yote – Pili amuombe Mungu Aharibu kazi hizo za Shetani. Baada ya Maombi – Mwanaume kila akienda kucheza MECHI na nyumba ndogo hafanyi kazi, akafikiri amelogwa, akaenda kwa wanganga hadi WAMASAI, nguvu za KI - hazikurudi, akienda kwa mkewe anakuwa na Nguvu kama Simba. Mwishowe akaona hana jinsi, akarudisha majeshi nyumbani, na Mama sasa anakula kwa Raha zake.


Rafiki usitumie nguvu na akili zako kutatua matatizo ya Ndoa yako, salimisha maisha yako kwa Mungu, halafu Mtwishe yeye Fadhaha zako, ana njia maelfu za kukushindia. Shetani si chochote si lolote, ndiyo maana anafanya kila mbinu kututenga na Mungu, anajua tukiwa na Mungu hana uwezo wa nasi – MUNGU WA AMANI ATAMSETA CHINI YA MIGUU YETU 

NDOA NA MATUMIZI YA FEDHA



Ujumbe wa Leo unatoka: 1 Timotheo 6:10
Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda FEDHA; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani na kujichoma kwa maumivu mengi”
TAFAKARI:a
Kama tunavyoshuhudia, matukio mengi ya kutisha mfano: Mauaji hadi ya Albino, Ujambazi, Ukahaba, Ufisadi, Wizi n.k. huchangiwa na kupenda Fedha. Pia Ndoa nyingi leo zinaathirika na swala hili la Pesa, leo kwa ufupi tunaangalia njia za kutatua matatizo ya NDOA yanayotokana na fedha.


1. Ubinafsi katika Vipato: Hili ni tatizo kubwa, kwenye ndoa hakuna neno changu, kuna neno CHETU, hivyo vipato vinatakiwa viwekwe wazi, ili vipangiwe matumizi kwa pamoja. Mifumo Dume haitakiwi, na wengine wanasema kipato cha baba ni cha Familia na kipato cha Mama ni Chake Mwenyewe – Huo ni Ubinafsi.


2. Matumizi ya Fedha yapangwe na wanandoa wote, yakizingatia pia matumizi binafsi “Pocket Money”. Kama mama hana kipato, fedha kiasi itengwe kwa ajili ya matumizi yake binafsi. Kununua vitu vya thamani bila kumshirikisha mwenzio tayari ni tatizo – mwenzio atajua una pesa nyingi umemficha. Moja kwa moja Imani inapotea na wakati wote atafikiri una Mapesa na kuna mambo ya siri unayafanya bila ya yeye kujua.


3. Familia iwe na Vipaumbele, hapa inahitajika hekima, make watu wanatofautiana mitazamo: Mwanaume utakuta anapenda music system ya Kisasa wakati Mama anataka Jiko kubwa la gesi, na fedha haitoshi, hilo ni tatizo tayari.


4. Kutokana na hali ya maisha kwa wengi kuwa Ngumu na Vipato kuwa vidogo – inahitajika Busara na kuwa na KIASI juu ya kupanga matumizi. Inahitaji Upendo wa Kweli ambao utawaunganisha nia zenu kuwa kitu kimoja. Amueni kuishi kulingana na Kipato chenu.


Ushauri kwa wanaume: Acheni kutumia fedha ovyo kwa mambo ya Starehe huku akina Mama wakibeba mizigo mizito ya kuhangaika na familia, ulevi na machangudoa ni sumu ya Maisha ya Ndoa.
Ushauri kwa wanawake wenye Vipato Vikubwa kuzidi waume zao:Kuweni na Busara, wapeni waume zenu heshima ya kuwa Baba wa Familia, kuweni na kiasi katika kuvaa, sio kila toleo kitenge uwe nalo.







































































































































Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

HUDUMA ZA MAZISHI

Huduma ya Mazishi  (Mchungaji, mzee wa kanisa, au shemasi anaweza kufanya huduma hii). Ushauri umetolewa kwamba, kadiri inavyowezekana, maz...