SEMINA YA WAZEE WA KANISA
KIONGOZI WA KIROHO
Kiongozi wa kiroho ni tofauti na kiongozi asiye wa kiroho kwa kuwa kiongozi wa kiroho ni mtumishi anayewatumikia anaowaongoza wakati huyu kiongozi mwingine hutumikiwa na wale anaowaongoza. Yesu ni mfano kamili wa kiongozi wa kiroho.
- (Marko 10:45) Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
- (Yohana 13:4-5) aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga
- (Marko 10:43) Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu. Na kwahiyo sifa kuu ya kiongozi wa kiroho ni kuwa mnyenyekevu na kuwa na huruma.
- (Luka 7:12-13) Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie.
Mzee wa kanisa ili atimize vyema wajibu wake ni lazima pia aijue taasisi anayoitwa kuiongoza. Kanisa ni mali ya Mungu aliyoinunua kwa damu ya mwanae Yesu Kristo na kuiweka chini ya usimamizi wa Roho Mtakatifu ili itumike hapa duniani kama chombo cha wokovu kwa wanadamu wote. (Matendo ya Mitume 20:28) Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.
Kanisa ndicho kitu cha thamani sana hapa duniani kwani kilinunuliwa kwa damu ya thamani ya Yesu. (Matendo ya Mitume 20:28) Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. (Waefeso 5:25) Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake. Ingawa shetani kwa karne nyingi amejaribu kuliharibu kanisa hili, Yesu ameendelea kutimiza ahadi yake ya kulilinda na nguvu za kuzimu.(Mathayo 16:18) Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu;wala milango ya kuzimu haitalishinda. Mwamba unaotajwa hapa si Petro bali ni Yesu mwenyewe. (1 Wakorintho 10:4) Wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Yeye ndiye aliyekuwa katika kanisa jangwani pamoja na yule malaika aliyesema naye katika mlima wa Sinai, tena pamoja na baba zetu; ndiye aliyepokea maneno ya uzima atupe sisi. (Matendo ya Mitume 7:38). Kristo ndiye kichwa cha kanisa. (Waefeso 5:23) Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Mzee wa kanisa asiruhusu watu kugeuza kanisa kuwa mahali pa kupimania ubavu, ubabe na kutambiana juu ya nani aliye bora kuliko mwingine. Wala asiruhusu kanisa kugawika kwa misingi ya watu wenye ushawishi au ukabila kwa kuwa si Paulo wala Kefa aliyelinunua hili kanisa. (1 Wakorintho 1:12, 13) Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo?
Yesu alikuja duniani kuondoa ukuta uliokuwa umetugawa sisi tuliokuwa wamataifa na Wayahudi. (Waefeso 3:6) Ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili. Ukuta huo aliubomoa kwa kutoa kafara ya upatanisho iliyotuwezesha sisi tuliokuwa wamataifa pamoja na wale waliokuwa warithi wa ahadi za kimwili zilizotolewa kwa Abrahamu kuhesabiwa haki ya kuwa warithi wa Agano Jipya. Yesu anawathamini wale walioko nje ya zizi hili kama anavyotuthamini sisi. Yeye huwaita wale walio kwenye zizi lile ni kondoo wake. (Yohana 10:16) Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja (Wagalatia 3:27-28). Hili hututangazia kuwa sisi tulio kanisani hatupaswi kujigawa makundi makundi ya kubaguana. Kuta hizo Yesu alikwisha kuzivunja. (Wagalatia 3:27 – 29) Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Moja ya wajibu mkubwa wa kanisa leo ni kuifanya hekima hii ijulikane kwa ulimwengu wote.
Kuitwa kuwa mzee wa kanisa ni kupewa heshima kubwa kwa kuwa anayestahili heshima hiyo ni Yesu mwenyewe. Wazee wa kanisa ndiyo viongozi wa kwanza kabisa kuwekwa ili kulilinda na kulichunga kanisa lake Mungu. (Matendo ya Mitume 14:23) Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini. Paulo alikutana nao wazee hawa mara kwa mara na kuwapa maelekezo muhimu ya usimamizi wa kanisa la Mungu kama tufanyavyo leo. (Matendo ya Mitume 20:17) Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa. Hawa ndiyo waifanyao kazi pamoja na Kristo kulisafisha kanisa lake ili lisiwe na kunyanzi. (Waefeso 5:27) Apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.
SIFA YA MZEE WA KANISA
Sifa za wazee zimetajwa katika Agano la Kale na Agano jipya kwa mafungu yafuatayo:
“Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi.” (Kutoka 18:21)
“Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi.” 1 Timotheo 3:1-7
MAJUKUMU YA MZEE WA KANISA
Majukumu ya Mzee wa Kanisa yamegawanyika katika Nyanja tatu: Kuchunga, Kusimamia, na Kuongoza (kuwa kielelezo au kuonesha njia). (1 Petro 5:1-4) Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.
KUCHUNGA:
Mtu huchungwa kwa kuhakikisha amekula chakula anachokihitaji na kwa kiasi atakachoshiba. Utafiti unaonesha kuwa miongoni mwa sababu zinazowafanya watu waasi na kuacha kutembea na watu wa Mungu, ni mafundisho potofu wanayopewa na waasi wenzao. Ili kuzuia ongezeko hilo mzee wa kanisa atahakikisha washiriki wake anawapatia mafundisho ya misingi ishirini na nane kwa ukamilifu na kuchukua muda wa kujibu hoja za kisera zinazotolewa na waenezao mafundisho ya uongo. Kuchunga pia kutahusisha kutembelea washiriki majumbani na kutembelea kwenye makundi mara kwa mara akiyaimarisha ili yaweze kukua na kuwa kanisa. Kuhubiri kila Sabato na kuhakikisha waliopangwa kwa mahubiri wanakidhi hitaji. Kuhakikisha watu walio kwenye eneo lake wanafikiwa na injili ya Yesu na hivyo kuongeza idadi ya washiriki wake kila mwaka angalao kwa 25% ya washiriki waliopo. Kuona kuwa washiriki wananunua Biblia, Miongozo ya kujifunza Biblia na kitabu cha Tumaini Kuu kwa ajili yao wenyewe na kwa kugawia wasiofikiwa na injili yetu. Kuona kuwa kila idara inajihusisha na shughuli za uinjilisti. Kuona kuwa jengo la ibada linaboreshwa ili lifanane na heshima ya Mungu tunayemwabudu.
KUSIMAMIA:
Mchungaji asipokuwepo mzee wa kanisa atasimamia baraza la Kanisa na kushughulikia kujaza nafasi zilizo wazi, kutoa adhabu kwa waumini, kwa kadri atakavyoelekezwa na mchungaji, ataendesha meza ya Bwana, atatoa matangazo, atatoa semina kwa watenda kazi, atapitisha wanaohama na wanaohamia, ataendesha huduma ya mazishi, atahudhuria semina, atakaribisha wageni na kuwaandalia huduma za malazi na chakula, atatuma taarifa kunakohusika, atakuwa msemaji wa kanisa. Atasimamia ratiba za vipindi na kuona kuwa wahusika wanazingatia muda uliopangwa na ya kwamba vipindi vinaendeshwa kwa kuzingatia miongozo na maelekezo yaliyopo. Kuhakikisha kanisa lina dira na mpango wa muda mfupi na wa muda mrefu unaofafanua namna mtakavyofikia viwango vya juu vya ukuaji katika siku za usoni. Wazee watumie madaraka waliyopewa kukemea wale wenye mazoea ya kulisumbua kanisa na kuyumbisha washiriki ikiwa baada ya kupewa semina bado wameendelea kukaza shingo. (1 Timotheo 5:20) Wale wadumuo kutenda dhambi uwakemee mbele ya wote, ili na wengine waogope.
KUONGOZA:
Mchungaji ataongoza kwa kuonesha kielelezo kwa mwonekano, vitendo, na kauli. Ataonyesha uongozi wa utumishi kwa kuwavuta anaowaongoza na kamwe hatafanya kazi kwa kulazimisha au kwa manung’uniko. Atafungua milango kwa washiriki ili wamfikie kwa matatizo yao, atashauri na kusuluhisha migogoro, atakuwa mwaminifu na mwadilifu, ataimarisha umoja na kupiga vita ubaguzi wa namna yoyote. Atawahimiza na kuwatia shime washiriki wake kutumia fursa zilizopo na uwezo walio nao kujiletea maendeleo ya kiuchumi, kiakili, kijamii, na kiroho na hivyo kuboresha maisha yao nay a kanisa. Atawahimiza kutimiza wajibu wao kwa lugha ya kiungwana na staha huku akiwaelekeza kwa Kristo
MIPAKA YA MZEE WA KANISA
Wazee wa kanisa watawekeana zamu ili kutoa fursa kwa asiye zamu kushiriki huduma za makundini au huduma zingine. Mzee kiongozi ndiye atakayehusika kuendesha vikao vya baraza la Kanisa mchungaji asipokuwepo, pamoja na matangazo, lakini anaweza kukasimu madaraka hayo kwa wengine akitaka. Kila idara itapewa mzee mmoja atakayeisimamia kwenye vikao vyake na kuihimiza itekeleze majuku yake. Mzee wa kanisa ni mzee hadi kundini hivyo ataweka kwenye ratiba yake siku za kutembelea kundini kwa semina na kusalimu washiriki. Mzee wa kanisa hatahudumu katika kanisa amabalo halijamchagua isipokuwa kwa kibali cha mchungaji wa mtaa. Kipindi cha mzee kukaa madarakani ni mwaka mmoja au miwili kutegemeana na maamuzi yaliyopitishwa na mashauri ya kanisa. Ikiwa baada ya muda huo mzee ataonekana bado anahitajika katika utumishi wake, na ikiwa watu wengine wenye sifa kama ya kwake hawapatikani, kanisa linaweza kumchagua tena.
WASAIDIZI WA MZEE WA KANISA
Mzee wa kanisa atatakiwa awape uzoefu na kuwapa shime watendaji walio chini yake akiwaelekeza namna ya kufanya kazi zao kwa ufanisi. Asiwalaumu wanapokosea bali awaonye kwa unyenyekevu akiwakumbuka kwenye maombi yake ili roho awasaidie kubadilika. Mzee awashirikishe wenzake katika maamuzi wala asipende kufanya maamuzi peke yake. Awathamini watendaji wenzake akitambua kuwa kazi inayofanywa kwa ushirikiano kama timu ndiyo inayofaulu. Mara kwa mara awapongeze na kuwashukuru wale wanaofanya vema ili wapate nguvu ya kuendelea kufanya vizuri. Asiruhusu wasaidizi wake kuchukua nafasi yake kwa kuwa mambo yatakapoharibika ni yeye atakayewajibika. Akubali kuwajibika kwa makosa ya wasaidizi wake.
MIIKO YA MZEE WA KANISA:
Ni mwiko kwa mzee wa kanisa kutoa siri za Baraza au za washiriki anaowatembelea kwa watu wasiohusika. Ni mwiko pia kwa mzee kutembelea washiriki akiandamana na mtenda kazi wa jinsia tofauti na kuwa na ukaribu unaokaribisha maswali na mashaka. Ni mwiko kwa mzee wa kanisa kutumia fedha za kanisa bila idhini ya baraza la kanisa. Ni mwiko kwa mzee wa kanisa kumsimamisha kazi au kumpa adhabu mshiriki bila idhini ya baraza la kanisa na mashauri ya kanisa. Ni mwiko kwa mzee wa kanisa kumzuia mchungaji wa mtaa wake kuhudumu kwenye kanisa au kundi alilopo. Ni mwiko kwa mzee wa kanisa kugomea maagizo yaliyotoka ngazi za juu kwa utashi wake mwenyewe au kwa kushinikizwa na kanisa lake. Ni mwiko kwa mzee wa kanisa kuruhusu kikundi chochote cha kanisa kutoka nje ya kanisa lake au kikundi cha kanisa lanje kutembelea kanisa lake bila taarifa na idhini ya mchungaji. Ni mwiko kwa mzee wa kanisa kuruhusu kutumia mimbari watu waliokatazwa na uongozi wa juu kutumika kanisani. Ni mwiko kwa mzee wa kanisa kutompokea na kumwandalia malazi na chakula mgeni wa kanisa aliyewatembelea. Ni mwiko kwa mzee wa kanisa kugomesha kanisa kutokuja mkutanoni au kwenye makambi kwa sababu yoyote ile.
WAJIBU WA WASHIRIKI KWA MZEE WA KANISA
Mzee wa kanisa anafanya kazi nyingi za kanisa kwa kutumia muda wake na wakati mwingine kwa kutumia mali zake na hivyo kanisa linapaswa kuonesha kutambua ukweli huo kwa kumpa heshima anayostahili. (1 Petro 2:17-18) Waheshimuni watu wote. Wapendeni ndugu. Mcheni Mungu. Mpeni heshima mfalme. Enyi watumishi, watiini bwana zenu kwa hofu nyingi, sio wao walio wema na wenye upole tu, bali nao walio wakali. Tena mahali pengine mtumishi wa Mungu amesisitiza akisema. (Waebrania 13:17) Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.
MKUU WA HUDUMA
MKUU WA HUDUMA
CHIMBUKO LA HUDUMA ZA WASHIRIKI:
Idara katika kanisa la Mungu huanzishwa kutegemeana na mahitaji yanayojitokeza katika kipindi husika. Uanzishwaji wa Idara unakusudia kuliweka jukumu fulani muhimu mikononi mwa watu wachache watakaolishughulikia kwa umakini zaidi badala ya jukumu hilo kusimamiwa na kanisa lote kwa ujumla. Kabla idara ya mashemasi haijaanzishwa inaelekea kanisa zima lilisimamia shughuli za kulihubiri Neno au shughuli ya uinjilisti. Baada ya kuoneka haja ya kuwepo kitengo kinachojishughulisha na utatuzi wa migogoro yaani mashemasi ndipo na watu wengine maalumu wakawekwa kusimamia shughuli za uenezaji wa Neno au Uinjilisti.
“Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno”. (Matendo 6: 1-4)
SIFA ZA VIONGOZI WA HUDUMA ZA WASHIRIKI
Kiongozi wa huduma za washiriki ni mtu anayetwishwa jukumu la kusimamia mipango ya Uinjilisti ya kanisa katika mwaka husika na katika eneo lote la kanisa husika. Mtu huyu ni lazima awe ameshuhudiwa kuwa na karama za uinjilisti, kuwa na shauku ya kuona roho nyingi zikiokolewa, na mwenye juhudi na moyo usiokata tamaa.
WAJIBU WA VIONGOZI WA HUDUMA ZA WASHIRIKI
Idara ya huduma za washiriki huhusisha idara zote zilizopo kanisani isipokuwa idara ya mashemasi. Idara hii ina viongozi wakuu wawili. Mmoja huitwa Kiongozi wa Huduma na mwingine huitwa Katibu wa huduma. Viongozi hawa wote ni wajumbe wa Baraza la Kanisa.
MAJUKUMU YA IDARA YA HUDUMA
Kama nilivyosema awali idara hii hushughulikia kuona kama idara na washiriki wote wameingizwa katika shughuli za uinjilisti katika mwaka husika. Jambo la kwanza wanapoanza kazi mwanzo wa mwaka ni kuitisha kikao kitakachojadili idadi ya roho zilizolengwa kuongolewa katika mwaka husika, watakaohusika kuzileta roho hizo, mbinu zitakazotumika kuzileta roho hizo, maeneo mapya yatakayopewa kipaumbele, tarehe na mahali ambapo matukio mbalimbali ya uinjilisti yatafanyika, upatikanaji wa vyombo vya kuhubiria, chakula, wanatimu, vibali vya mikutano na Bima, wahubiri, Kwaya, nyumba za kulala wanatimu, vijizuu na masomo ya sauti ya Unabii, Biblia, Zawadi mbalimbali na matangazo yatakayohitajika. Mbinu kuu zinazotumika kupata roho makanisani kwa sasa ni Mikutano ya hadhara (Effort), Huduma za Utabibu, Shule na Vyuo vyetu, Vitabu vyetu kupitia wainjilisti wa vitabu, Radio na Sabato za Wageni. Njia hizi kwa kawaida hutumika kama hatua ya kuvuna kile kilichopatikana kutokana na madarasa ya Biblia Yasema yaliyokuwa yanaendelea kipindi chote cha mwaka, vijizuu, vilivyokuwa vikigawanywa kwa nyakati mbalimbali, mahusiano ya kifamilia, kirafiki na kiukoo, kiujirani, kikazi na pia kama matokeo ya kusikiliza hotuba za mikutano iliyopita iliyofanyika sehemu mbalimbali. Ili kufanikisha shughuli zake idara hii inapaswa kufanya yafuatayo:
KUCHUKUA TAKWIMU MUHIMU ZA WATU ZA ENEO LA KANISA ANALOLISHUGHULIKIA:
Takwimu hizi ni zile zinazoonesha eneo lake lina vijiji na vitongoji vingapi, idadi ya wakazi wote wa eneo hilo kwa mujibu wa sense iliyopita ni wangapi, kati ya wakazi hao wanaume, wanawake na watoto ni idadi gani, waadventista na wasio waadventista ni kiasi gani. Takwimu hizo zitamsaidia kujua ukubwa wa jukumu lake la kupeleka injili lilivyo. Lengo la idara ya huduma ni kuona wote walioko kwenye eneo lake wanafikiwa na ujumbe wa malaika watatu na wanaupokea.
MKAKATI WA KULIFIKIA ENEO LOTE KWA INJILI:
Mkuu wa Idara na msaidizi wake wataweka mipango ya muda mfupi, muda wa kati, na muda mrefu wa namna ya kulifikia eneo lote la kanisa lake na Injili ya Milele. Ataainisha maeneo yaliyofikiwa na injili na yale mapya, na kila mwaka ataonesha mipango aliyonayo kwa ajili ya maeneo mapaya na ya zamani. Kila mwaka atachagua eneo moja kwenye maeneo mapya na eneo jingine kwenye maeneo ya zamani ambako kanisa litaweka msisitizo wake wa uinjilisti.
KUZIGAWIA IDARA MAJUKUMU YA KIUINJILISTI KWA MWAKA HUSIKA:
Viongozi wa idara hii watazigawia idara zilizopo kanisani maeneo ya kufanyia kazi na roho wanazotakiwa kuzivuna kama matokeo ya kazi yao ya uinjilisti kwa mwaka husika. Idara hizo katika vikao vyao zitatakiwa zioneshe mbinu mbalimbali watakazotumia kufikia lengo hilo na kuwaridhisha viongozi wa idara ya huduma kama kweli mbinu hizo pekee zinatosha kufikia malengo hayo. Mchana wa Sabato ya kwanza ya mwezi kwa kawaida hutumika kwa ushuhudiaji na kutoa taarifa ya kazi. Kama katika mbinu zilizopendekezwa kuna Effort na Sabato za Wageni, uongozi wa idara utaratibu ili kuhakikisha shughuli hizo haziingliani na shughuli zingine za aina hiyo hiyo za idara au kanisa zinazofanywa wakati huo huo na mahali hapo hapo.
BARAZA LA MALENGO YA UINJILISTI YA MWAKA:
Idara ya Huduma za washiriki itafanya kikao chake cha pili kitakachopokea mipango yote ya kiuinjilisti ya maidara kwa mwaka na kuifanyia marekebisho pale yanapohitajika na kisha watayaunganisha pamoja ili kuyawasilisha kwenye baraza la kanisa. Mipango hiyo itaonesha kinachokusudiwa kufanyika, tarehe kitakapofanyika, wahusika wa tukio, gharama zitakazotumika, na zitakavyopatikana gharama hizo. Vyanzo vya mapato kwa kawaida ni Bajeti ya Kanisa, michango ya washiriki, Harambee, Wafadhili wa ndani na nje, na Miradi.
VITENDEA KAZI VYA INJILI:
Idara ya huduma inatakiwa kujua mahitaji ya vitendea kazi vya kanisa vinavyohitajika kwa ajili ya shughuli za uinjilisti na kuhakikisha vitendea kazi hivyo vinapatikana kwa wakati ama kwa kuvinunua ama kwa kuviazima. Vitendea kazi hivi vimegawanyika katika makundi mbalimbali kama ifuatavyo;
Vyombo vya electronic vya kuhubiria ambavyo ni Generator, Projector, Amplifier, Mixer, Speakers (box na horn), Microphone za nyaya, Microphone zisizo na waya (Wireless Microphone) na receiver zake, Stabilizer, Extension cables na nyaya za umeme na za spika, DVD au Video Receiver, Laptop n.k.
Vitendea kazi vya mfumo wa karatasiambavyo ni Biblia Yasema, Masomo ya sauti ya Unabii, Masomo ya mgunduzi, Masomo ya Sauti ya Unabii, Vijizuu, Matangazo ya kubandika na ya kugawa, Kadi za mialiko, magazeti, vitabu, Picture rolls, Biblia, Vibali vya mkutano, Bima n.k.
Vitendea kazi vya mfumo wa samaniambavyo ni Jukwaa la wahubiri na waimbaji, jukwaa la box na horn speaker, Viti vya wahudumu na vya mkutano, Vibanda vya kukaa wasikilizaji kuwakinga na mvua au jua na gharama zote za ujenzi.
Huduma za Malazi na chakula ni eneo jingine ambalo linahitaji kuwekewa mipango kamili. Ni lazima ijulikane idadi ya watu watakaohitaji chakula, malazi na huduma zingine muhimu. Ni jukumu la wakuu wa idara husika wakishirikiana na viongozi wa huduma kuona kuwa chakula cha kutosha kinakusanywa mapema kabla ya tukio na malazi ya wanatimu, kwaya na mhubiri vinajulikana mapema. Washiriki binafsi waombwe kusaidia wawezavyo kwenye eneo hili ili kupunguza gharama.
MAFUNZO
Jukumu lingine la idara ya huduma za washiriki ni kutoa mafunzo ya namna ya kufanya uinjilisti. Mafunzo haya yamegawanyika katika maeneo mbalimbali. Eneo la kwanza ni mafunzo ya namna ya kuhubiri kwenye mikutano ya hadhara na mikutano ndani ya kanisa. Mafunzo haya hutolewa kwa washiriki wote na baada ya kupimwa wale watakaooneka wamemudu wataorodheshwa ili kutumika katika maeneo husika. Eneo jingine la mafunzo ni mafunzo ya kuingia nyumba kwa nyumba yatakayofuatiwa na mafunzo ya kuendesha madarasa ya Biblia Yasema na mbinu za kukatisha shauri. Wakuu wa idara pia wataendesha mafunzo ya Walei na Wamishionari ili kuongeza idadi yao maana ni watu muhimu kwa kazi ya uinjilisti. Pamoja na mafunzo haya viongozi wa idara wanaweza kuendesha semina ya kujadili mafungu tata na kuyapatia ufumbuzi.
HUDUMA KWA JAMII
Idara ya huduma za washiriki itawahamasisha washiriki kufanya huduma mbalimbali za kusaidia wenye mahitaji wanaopatikana kwenye jamii wanayokusudia kuipelekea injili. Huduma hizo ni pamoja kutoa nguo, fedha, chakula, matibabu, ushauri wa afya, ndoa, na msuala ya uchumi, kujenga au kukarabati nyumba, choo, visima, kulima shamba, kushona nguo zilizotatuka, kuunga kandambili, kurepea viatu, majembe, sufuria, miavuli, kunoa majembe, mapanga, na mashoka, kufundisha tuition watoto n.k. Shughuli hizi hujenga mahusiano mema na kufungua njia kwa ajili ya Injili.
WALEI KABLA NA BAADA YA MKUTANO:
Viongozi wa idara hii wataorodhesha Walei na Wamishionari waliopo kwenye kanisa lao ili kuwatumia kwa ajili ya maeneo mapya yaliyokusudiwa kufanywa mikutano ya injili mwaka huo. Walei wapelekwe kwenye eneo la tukio miezi mitatu kabla na waendelee kubaki angalau miezi mitatu baada ya mkutano kwisha. Gharama za walei na wamishionari hawa zitolewe na kanisa au wafadhili wa ndani na nje. Washiriki wote wahimizwe kutoa vyakula, samani, na nguo kwa ajili ya walei watakaojitolea kulea waumini wapya.
TAARIFA YA SHUGHULI ZA KUONGOA ROHO
Kila baada ya mkutano wa Injili kwisha na mwishoni mwa robo katibu wa Huduma ataandika taarifa inayoonesha mikutano ya injili iliyofanyika, watu waliosikia ujumbe huo (utafanya makisio kulingana na umbali ambao vyombo vyenu vilimudu kurusha mahubiri na idadi halisi waliohudhuria), waliopokea Ujumbe (hapa utachukua jumla ya watu walijitoa kutaka kuendelea kujifunza), na idadi ya waliojitoa kwa ubatizo. Taarifa itaonesha pia gharama zilizotumika na kama makdirio mliyojiwekea yalifikiwa au hayakufikiwa na utapendekeza kwa nini yalifikiwa na kwa nini hayakufikiwa.
MIIKO YA VIONGOZI WA HUDUMA ZA WASHIRIKI
Viongozi wa idara ya huduma hawaruhusiwi kuwatumia kwa kazi ya Injili watu waliozuiwa na uongozi wa Konferensi au wenye msimamo unaokwenda kinyume na kanisa. Hawaruhusiwi kualika mhubiri au kwaya yoyote bila taarifa na idhini ya mchungaji. Mialiko yoyote kutoka au kwenda nje ya mtaa ni lazima ipitie kwa mchungaji na kasha Konferensi na bima ya dola moja (sawa na Tshs 1,700/= kwa sasa) kwa mtu mmoja ni lazima ilipwe kwa ofisi ya Konferensi majuma mawili kabla ya safari. Ni mwiko kwa mikutano yetu kuvuka muda tuliopangiwa au kukiuka masharti tuliyopewa isipokuwa kama kuna haja hiyo basi viongozi waonane na uongozi wa mahali pale mapema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni