MAFUTA YA UPAKO
Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake. (Zaburi 133:1, 2)
Mafuta yaliyotumika kuwapaka makuhani yalikuwa ni ishara ya Roho Mtakatifu. Tunahitaji Roho Mtakatifu, ndiye pekee anayeweza kuleta umoja katika kanisa letu ili tuweze kufanikiwa katika jitihada zetu za kimisionari.
Maisha yetu ni lazima yafichwe ndani ya Mungu kupitia kwa Yesu Kristo. Ni lazima tuwe na uelewa binafsi wa Mungu, ndipo tunapoweza kumwakilisha kwa namna iliyo sahihi kwa ulimwengu. Ni lazima nuru yetu iangaze popote tulipo ikionesha utukufu wa Mungu kwa matendo yetu mema. Hii ndiyo kazi iliyo kubwa na muhimu katika maisha yetu. Wale ambao watakuwa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu, watadhihirisha uwezo wake kwa kuweka katika uzoefu kanuni za kweli za milele. Wataonesha kwamba yale mafuta matakatifu yametolewa katika ile mizeituni miwili kuingia katika vyumba vya hekalu la nafsi. Maneno yao yatakuwa yamejawa na nguvu ya Roho Mtakatifu ili kulainisha na kutawala moyo. Itadhihirika kwamba maneno yanayosemwa ni roho tena ni uzima. (Reflecting Christ, uk. 130)
Yeye anayehisi udhaifu wake na akamenyana na Mungu kama Yakobo alivyofanya, kwa kulia kwamba, “Sitakuachia hata utakaponibariki,” ndipo patakuwepo na kupakwa upya kwa mafuta ya Roho Mtakatifu. Ndipo angahewa ya mbinguni itamzunguka, na mvuto na mguso wake utakuwa chanya sawa sawa na dini ya Kristo. (Medical Ministry, uk. 203)
Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. (Yohana 16:13)
Hebu na tuongezeke katika elimu ya kweli tukimsifu na kumtukuza yeye ambaye ni mmoja pamoja na Baba. Hebu na tutafute kwa dhati kupakwa mafuta ya mbinguni ambayo ni Roho Mtakatifu. Hebu tuwe na Ukristo safi unaokua, ili mwishowe kule katika vyumba vya mbinguni tupate kutamkwa wakamilifu katika Kristo. (Reflecting Christ, uk. 219)
Ni lazima pawepo na namna ya kubadilisha, kwa kuchukua na kuachia, kwa kupokea na kutoa. Kwa kufanya hivi, tunaunganishwa kama watumishi pamoja na Mungu. Hayo ndiyo yanatakiwa kuwa ni maisha ya utendaji ya Mkristo, “yeye atakayeipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.”
Uwezo wa kupokea hayo mafuta matakatifu kutoka katika ile mizeituni miwili unaongezeka kadiri mpokeaji wa hayo mafuta anavoyatoa kutoka kwake kwenda kwa wengine kwa namna ya maneno au matendo ya kuwezesha roho zenye uhitaji. Kazi, yenye thamani, inayoridhisha itakayofanyika kwa kudumu kupokea na kutoa.
Tunahitaji, na ni lazima tupate mafuta mapya kila siku. Kwa kufanya hivi unadhani ni roho ngapi tunaweza kuzisaidia kwa kuwasiliana nazo? Mbingu yote inasubiri mifereji ambayo itatumika kupitishia mafuta ili kuleta furaha na mibaraka kwa wengine. Nina uhakika kwamba hakuna atakayefanya makosa ikiwa tu atakuwa mmoja pamoja na Kristo. Akiwa ndani yetu, tutafanya kazi bila kukoma kwa ukamilifu ili kazi hiyo tunayofanya ipate kudumu. Utimilifu wa kimbingu utamiminika kupitia kwa mawakala wa kibinadamu waliojitoa wakfu kuwafikia wengine. (Testimonies for the Church, vol.6 pp. 116, 117)
Roho Mtakatifu anapotawala fikra za washiriki wa kanisa letu, panakuwa na viwango vya juu sana vya hotuba, na huduma za kiroho kuliko inavyoonekana sasa. Washiriki watahuishwa na maji ya uzima, na watenda kazi wanaofanya kazi chini ya kiongozi ambaye ndiye kichwa yaani Yesu Kristo watamdhihirisha Bwana wao katika roho, katika maneno, matendo, na watatiana moyo wakisonga mbele katika kazi kubwa hii ya mwisho ambayo wameianza. Patakuwa na ongezeko la umoja na upendo lililo na afya, ambalo litakuwa na ushuhuda kwa ulimwengu kwamba Mungu alimtuma Mwana wake wa pekee ili afe kwa ajili ya ukombozi wa wenye dhambi. Ukweli wa kimbingu utainuliwa na kadiri unavyoangaza kama taa inayowaka, tutauelewa zaidi na kwa uwazi zaidi. (Counsels for the Church, uk. 100)
Tunakaribia mwisho wa historia ya ulimwengu huu, na Mungu anatuita wote kuinua viwango vyenye uvuvio. “Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” Anawaita watu wote wafanye kazi kwa upatanifu ulio kamili. Anawaita wale walio katika fani ya tiba kuunganika katika huduma; anaita huduma zote kushirikiana na huduma ya wamisionari wa kitabibu na analiita kanisa kutimiza wajibu wake, likiinua viwango vya matengenezo ya ukweli katika maeneo yao wakiwaacha wataalam na wenye uzoefu kuingia katika maeneo mapya. Tuepuke kutamka maneno yatakayowakatisha tamaa, kwani kwa kufanya hivi tunauhuzunisha moyo wa Kristo na kumfurahisha adui kwa sehemu kubwa. Wote wanatakiwa kubatizwa kwa Roho Mtakatifu, wote tunatakiwa kuepuka kuawaona wengine kama hawafai kwa kutoa kauli zinazokatisha tamaa na kuwafanya washindwe kumsogelea Kristo ili wapate kutambua uzito wa wajibu walio nao watendakazi pamoja naye.
MTAKATIFU KWA BWANA
Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi Bwana ni mtakatifu nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu. (Mambo ya Walawi 20:26)
“Mtakatifu kwa Bwana” ndiyo chapa iliyokuwa katika kofia aliyovaa Kuhani Mkuu. Bwana anatutaka sisi, kama alivyowataka makuhani wa wakati ule wa kale kuishi maisha yaliyotengwa, maisha matakatifu. Maisha yetu yanatakiwa kumshuhudia yeye.
“Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, ‘Mvueni nguo hizi zenye uchafu.’ Kisha akamwambia yeye, ‘Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi.’ Nikasema, ‘Na wampige kilemba kizuri kichwani pake.’ Basi, wakampiga kilemba kizuri kichwani pake, wakamvika mavazi; naye malaika wa Bwana akasimama karibu (Zakaria 3:4, 5)
Bwana hakukana mashtaka yaliyoletwa kuhusu kutokustahili kwa Yoshua, lakini alionesha kuwa amemnunua kwa thamani kubwa. Alimvika vazi lake la haki, sio kwamba alimvika vazi hilo juu ya mavazi yake machafu ya kutokutii na ukengeufu, bali kwanza alisema: ‘Mvueni nguo hizi zenye uchafu.’ Ndipo aliposema: “Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi.” Nikasema, ‘Na wampige kilemba kizuri kichwani pake.’ Basi, wakampiga kilemba kizuri kichwani pake, na kilemba kile kilikuwa na maandishi haya “Mtakatifu kwa Bwana.” (Manuscript Releases, vol. 20, pp. 190, 191)
Mkristo anatakiwa kusimama kama mwakilishi wa kanuni za mbinguni. Anafungwa na wajibu mtakatifu kuwakilisha ukweli kwa sifa njema na upendo. Maneno yake na matendo yake na yawe na alama za upole, wema, na ukweli usiotiliwa mashaka wala kupinda. Akiwa amewekwa wakfu kwa Mungu na kutengwa kwa ajili ya huduma yake siku zote ataheshimu imani ya dini yake. Katika tabia yake hautaonekana unyuzi hata mmoja wa ubinafsi. Tunatakiwa kujifundisha kudhihirisha Roho wa Mungu katika utendaji wote wa maisha yetu. Kamwe Roho wa Mungu hawezi kuongoza hatua za watoto wake mahali pasipofaa. Tunaweza kupalilia na kuondoa kila jambo linaloleta maswali katika maisha yetu kupitia katika uwezo ambao Roho Mtakatifu anatoa. Ikiwa tutatoka katika giza linalofunika nafsi, na kuweka maisha yetu penye nuru inayong’aa ya Neno la Mungu, hiyo nuru itatuangazia na kutuongoza hatua kwa hatua katika mapito yanayoelekeza kwenye utakatifu. (This Day with God, uk. 281)
Tangu milele Mungu alichagua watu wawe watakatifu. “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu.” Mwangwi wa sauti yake unatujia daima ukisema, “Mtakatifu, mtakatifu zaidi.” Na jibu letu daima liwe, “Naam, Bwana, mtakatifu zaidi.”
Hakuna anayeweza kupata utakatifu kama unavyopata haki ya kuzaliwa, au kama zawadi kutoka kwa mwanadamu mwenzake. Hii ni zawadi ya Mungu kupitia kwa Yesu Kristo. Wale ambao watampokea Mwokozi, wanahesabiwa kuwa wana wa Mungu. Hawa wamekuwa watoto wake kiroho, wamezaliwa upya, wamebadilishwa katika haki na utakatifu wa kweli. Fikra zao zimebadilishwa. Wakiwa na maono dhahiri wanautazamia uhalisia wa umilele. Wamekubaliwa katika familia ya Mungu, na wamekuwa sawa na mwonekano wake kwa kubadilishwa na Roho kutoka utukufu hadi utukufu. Walikuwa wanatunza upendo wa ubinafsi, lakini sasa wanadhihirisha upendo mkuu kwa Mungu na kwa Kristo. (Signs of the Times, Dec. 17, 1902).
Mwokozi wetu ni Mwokozi anayemkamilisha mwanadamu kwa utimilifu wote. Sio Mungu wa sehemu ya ubinadamu tu. Neema ya Kristo inafanya kazi ikinidhamisha kila kipengele cha ubinadamu. Yeye ndiye aliyefanya yote, ndiye atakomboa yote. Yeye ndiye aliyeumba akili, nguvu, mwili hata na nafsi ambayo ndiyo yenye asili ya kimbingu, na kila kitu ni vya kwake lakini alivinunua tena vikawa ni mali yake. Ni lazima atumikiwe kwa akili zote, kwa moyo wote kwa roho yote na kwa nguvu zote. Ndipo Bwana atakapotukuzwa kati ya watakatifu wake na hata kati ya watu wa kawaida, pamoja na vitu vya kupita hivi ambavyo wameunganishwa navyo. Chapa ya
“Utakatifu ni kwa Bwana” itaonekana imewekwa juu yao. (God’s Amazing Grace, uk. 230)
Ikiwa kuna watu wanajaribu kuboresha fursa zao na kuwa na hekima na utendaji ulio mzuri, basi wale wanaotumia uwezo wao katika kujenga ufalme wa Mungu katika ulimwengu huu wangekuwa wa kwanza. Ukichukulia kwamba tunaishi katika nyakati ambazo karibu historia ya ulimwengu huu itafungwa, ni lazima pawepo na umakini katika utendaji kazi, kusubiri kwa matazamio, kukesha, kuomba na kufanya kazi. Huduma zote za kidini na nyanja zote za biashara ni lazima ziwe na chapa ya mbinguni. “Utukufu ni kwa Bwana” na liwe ndilo tamko la watendakazi kila idara. Kila wakala wa kibinadamu na ahangaike ili kupata ukamilifu, na kwamba aoneshe mfano mwema wa Ukristo, akikamilika katika Kristo Yesu. (Review and Herald, Oct. 5, 1905)
“Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” (1 Petro 1:15, 16)
MIGUU ILIYO WAZI
Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. (Kutoka 3:5)
Mungu alimwonya Musa asikaribie bila kicho. Kitendo cha kuvua viatu kinaashiria mwonekano wa heshima ambao ni muhimu katika ibada ya kweli.
Mwonekano wa unyenyekevu na kicho unatakiwa kuonesha mwenendo wa wote wale wanaosogelea uwepo wa Mungu (Patriarch and Prophets, uk. 252)
Tunaweza kuja kwake kwa kujiamini kwa jina la Yesu, lakini tusimsogelee kwa kiburi kana kwamba tupo ngazi moja naye. Wapo wale ambao wanamchukulia Mungu mkuu mwenye uwezo wote, akaaye mahali pa juu pasipofikika kwenye nuru ya ajabu isiyoweza kupenyeka, kama mwenza wao au aliye duni kuliko wao. Wapo wale ambao wanapachukulia mahali pa kuabudia kama vile wako mbele ya wafalme wa dunia hii tu. Mungu ni mkuu anayestahili kuheshimika kwa hali ya juu, wote ambao wanatambua kwa dhati uwepo wake, watasujudu kwa unyenyekevu mbele yake. (Patriarch and Prophets, uk. 252).
Kule kuvikwa na hali ya unyenyekevu hakumaanishi kwamba tutageuka na kuwa wadumavu kiakili, tukapungua katika matarajio, na kuwa waoga maishani tukikwepa mizigo kwa kuogopa kuibeba kwa mafanikio. Unyenyekevu wa kweli unatimiza kusudi la Mungu kwa kutufanya tutegemee uweza wake (God’s Amazing Grace uk. 270).
Lakini anatujalia neema zaidi. Kwa hiyo anasema, “…Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.” (Yakobo 4:6)
Mungu anafanya kazi kupitia kwa yeye anayemtaka. Wakati mwingine anachagua vyombo dhaifu lakini vinyenyekevu ili kufanya kazi kubwa, kwani uweza wake unadhihirishwa katika udhaifu wa wanadamu. Tunavyo viwango vya kibinadamu ambavyo vinatuwezesha kutamka kitu kimoja kuwa kikubwa na kingine kuwa kidogo; lakini Mungu hakadirii kulingana na viwango na kanuni za kibinadamu. Hatutakiwi kudhani kuwa kile kilicho kikubwa kwa viwango vyetu basi kitakuwa kikubwa mbele za Mungu, au kile kilicho kidogo kwetu kitakuwa kidogo mbele zake.
Kujisifu kunaokoonekana kwa wanadamu hakuna nafasi mbele zake… Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira hauhesabiwi kwa matendo yake mtu yeyote asije akajisifu, bali ihesabiwe kuwa ni neema. Hakuna dini ambayo inajitawalisha yenyewe, yeye anayefanya kujitukuza kuwe ndilo lengo lake, mwisho wake atajikuta akikosa neema ambayo ingemfanya kuwa bora katika kazi ya Kristo. Pale kiburi na kujiona bora kunapo tawala maisha, kazi inaharibiwa.
Mkristo ambaye katika maisha yake anajitoa kila siku na kuondoa ubinafsi, akiwa na kusudi la dhati kwa usafi wa fikra, akionesha unyenyekevu anaposhambuliwa, kwa imani na kicho, katika uadilifu kwa kila hali, yeye ambaye anawakilisha tabia ya Kristo nyumbani kwake, huyo atakuwa wa thamani machoni pa Mungu kuliko mmisionari mwingine wa aina yoyote au hata mfia dini. (God’s Amazing Grace uk. 270).
“Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake.” Mbingu yote inaingia katika ubia na wale wanaokuja kwa Kristo kwa ajili ya maisha ya milele, wakijitoa kwake kana kwamba wamekabidhi yote kwa Mungu. Mungu anahitaji watumishi wake wasimame chini ya bendera yenye damu ya Mfalme Emanueli, wakipambana kwa uweza wake kuhakikisha misingi ya kweli inabakia safi bila kuchafuliwa. Hawapaswi kuepuka mapito ya kujikana nafsi na unyenyekevu ambayo ni lazima Mkristo wa kweli ayapitie. Kadiri wanavyoshirikiana na Mungu, basi Kristo anaumbika ndani yao ambaye ni tumaini la utukufu. Wakijitoa kikamilifu katika unyenyekevu na kujishusha, wanapitia katika uzoefu wa furaha isiyo na kipimo kwa kushiriki katika huduma yake. Mivuto ya kidunia inatoa nafasi kwa haja ya kumtumikia Bwana. (Review and Herald, May 11, 1897, aya ya 14)
Tunahitaji kumsogelea Mungu ili tuone kama kuna vitendo vya wivu au kijicho vinazokuzuia kuelekea kwa Mwokozi. Ubinafsi, na kujiona kuwa unajitosheleza hufunga mlango wa moyo dhidi ya Yesu, na kusema “Sihitaji mapito yako, nitafuata njia zangu.” “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake.” Toba ya dhati inayotoka moyoni, kutoka katika moyo uliofanywa mgumu kwa anasa za ulimwengu huu itasikiwa na Mungu, na dhambi zote zitaonekana kwa mhusika jinsi zinavyoonekana machoni pa Mungu aliye Mtakatifu. (Testimonies to Southern Africa, uk. 78)
Mungu anao watu wake aliowachagua atakaowatumia katika kazi yake ikiwa watamruhusu awatumie kama apendavyo. Hawezi kumtumia tu yeyote anayetaka kumnyenyekeza mwingine. Ndugu zangu tujinyenyekeze mbele zake, unapofanya hivi, malaika watakatifu wanaweza kuwasiliana nawe na kukuweka mahali palipoinuka. Ndipo uzoefu wako utajazwa na furaha badala ya kusikitika. Tafuta uhusiano wa upatanifu na Mungu ili akuongoze, ndipo utakapopata hisia za kuguswa na Roho Mtakatifu. (North Union Gleaner, March 23, 1910, aya ya 5)
JOHO (LA KUHANI)
Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo
Joho ni ishara ya haki ya Kristo inayofunika uchi wetu pale tunapoikubali.
Wale wote waliojivika vazi la haki ya Kristo watasimama mbele zake kama waliochaguliwa, waaminifu na wakweli. Shetani hana nguvu tena kuwang’oa kutoka mikononi mwa Kristo. Hakuna roho itakayokuwa katika majuto ya dhati, itakayodai ulinzi wake na kuachiwa chini ya uweza wa adui. Neno lake limeahidi kuwa, “Au azishike nguvu zangu, Afanye amani nami; Naam, afanye amani nami.” (Isaya 27:5). Ahadi aliyopewa Yoshua ni kwa ajili yetu wote: “Kama ukienda katika njia zangu, na kama ukishika maagizo yangu, ndipo utakapoihukumu nyumba yangu, nawe utazilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi ya kunikaribia kati yao wasimamao karibu.” (Zekaria 3:7). Malaika wa Mungu watatembea pande zote, hata ulimwenguni humu, mwishowe watasimama kati ya malaika wanaozunguka kiti cha enzi cha Mungu. (Counsels for the Church, uk. 351, 352)
Ni haki ya Kristo ndiyo inayomfanya mwenye dhambi aliyetubu kukubaliwa mbele za Mungu kwa kazi yake ya kuhesabiwa haki. Bila kujali jinsi maisha yake yalivyojawa na dhambi, akimwamini Yesu kama Mwokozi wake binafsi, atasimama mbele za Mungu akiwa amevikwa vazi la haki ya Kristo lisilo na doa. (Faith and Works, uk. 106)
“Tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani.” (Wafilipi 3:9)
Mwenye dhambi ambaye ni mfu katika dhambi anahuishwa kwa imani katika Kristo. Kwa imani anaona kwamba Yesu ni Mwokozi wake, na anaishi milele akiwa na uwezo wa kuokoa wale wote wanaokuja kwa Mungu kupitia kwake. Mwenye dhambi anaona mapana na marefu na kina cha ubora katika upatanisho uliofanywa kwa ajili yake. Anaona ukamilifu wa wokovu, akiwa amenunuliwa kwa gharama isiyopimika, ndipo nafsi yake inajawa na sifa na shukrani. Anaona utukufu wa Bwana kupitia katika kioo na anabadiliswa na kufanana naye kama vile katika roho ya Bwana. Analiona vazi la haki ya Kristo likiwa limefumwa kwa chombo cha mfumaji cha mbinguni kwa nyuzi za utii, ili kumwezesha yeye aliyeungama kupitia kwa imani katika jina lake.
Pale mwenye dhambi anapoona furaha ya Yesu, dhambi inakoma kuonekana nzuri kwake, kwani anakuwa amemtazama mkuu katika maelfu, yeye ambaye anampenda. Ndipo anapotambua kwa uzoefu binafsi wa nguvu ya injili, ambayo upeo wake wa ubunifu unalinganishwa tu na makusudi yake. (Faith and Works, uk. 106, 107).
Kadiri watu wa Mungu wanavyopitia katika maumivu mioyoni mwao, wakililia usafi wa mioyo, agizo linatolewa kwamba, “Mvueni nguo hizi zenye uchafu.” Na maneno ya kutia moyo yanatamkwa kwamba, “Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi.” Yule aliyechoka kwa majaribu na akawa mwaminifu wa Mungu anavishwa vazi lisilo na doa la haki ya Kristo. Wale walio masalia ambao walibezwa, sasa wanavikwa vazi la utukufu, wasije tena wakachafuliwa na uharibifu uliomo ulimwenguni. Majina yao yanabakizwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwana Kondoo yakiwa yameorodheshwa pamoja na waaminifu wengine wa vizazi vyote. Wamekataa vishawishi vya Yule mdanganyifu, hawakuondolewa kutoka kwenye uaminifu kwa kuunguruma kwake simba. Sasa wako salama milele, wapo ng’ambo ya mbinu zote za yule mjaribu. Dhambi zao zimehamishiwa kwa yule mwanzilishi wa dhambi. (Counsels for the church, uk. 353)
Imani ya kawaida tu haitoshi. Ni lazima tujivike vazi la haki ya Kristo na kulivaa wazi wazi, kwa ujasiri tukiwa tumedhamiria, tukimdhihirisha Kristo bila kutazamia chochote kutoka kwa mwanadamu, tukimtazama Yesu ili tupate kufananishwa na ukamilifu wake wa tabia. Ndipo kila mmoja wetu atadhihirisha tabia ya Yesu na kuonesha kwamba tumejawa na kweli; kwa sababu kweli inatakasa nafsi na kuteka kila fikra ipate kumtii Kristo. (Reflecting Christ, uk. 108)
Wale ambao kwa kweli ni wenye haki, ambao wanampenda na kumheshim Mungu kwa dhati watavaa vazi la haki ya Kristo ima kwa mafanikio au kwa mateso. Kujikana nafsi, kujitoa kafara, kutenda wema, upendo, ustahimilivu, kudhamiria na imani ya Kikristo ndiyo matunda ya kweli ya kila siku yanayooneshwa na wale ambao kwa kweli wameunganika na Mungu. Inawezekana matendo yao yasifahamike kabisa duniani, lakini wao wenyewe wanapambana na uovu kila uchao, huku wakishinda majaribu na mabaya yanayojitokeza. (God’s Amazing Grace, uk. 31).
“Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.” (1 Petro 2:24)
Kila mmoja atakabilana na pambano ili kushinda dhambi ndani ya moyo wake mwenyewe. Wakati mwingine zoezi hili linaweza kuwa chungu na la kukatisha tamaa kwa sababu mara nyingi tunajaribiwa kuelekeza fikra zetu katika mapungufu ya tabia zetu badala ya kumwangalia na kujivika vazi la haki yake. Kila mmoja atakayeingia katika malango ya lulu ya ule mji wa Mungu, ataingia kama mshindi, na ushindi wake mkuu utakuwa ni ushindi dhidi ya nafsi. (God’s Amazing Grace, uk. 31)
“Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.” (Zaburi 23:3)
NAIVERA
“Na hata uzee wenu mimi ndiye, na hata wakati wenu wa mvi nitawachukueni; nimefanya, nami nitachukua; naam, nitachukua na kuokoa.” (Isaya 46:4)
Kwa namna ambavyo kuhani mkuu alivyobeba ile naivera katika mabega yake, ndivyo Kuhani Mkuu anavyobeba mizigo yetu, akitutegemeza na kutuimarisha katika majaribu yanayotukabili na kutuwezesha kumshuhudia hata katika mazingira magumu. Mwokozi wetu wa thamani ametukaribisha kujiungamanisha kwake na kuunganisha udhaifu wetu kwenye Uwezo Wake, kutokujua kwetu katika Hekima yake, kutokustahili kwetu katika kustahili kwake. (The Faith I Live By, uk. 96)
“Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.” 1 Petro 5:7
Kwa wale waliovunjika mioyo kuna msaada – imani, maombi, kazi, na kujishughulisha kutawezesha kupata uhakika na kuridhika ambako kutaongezeka siku kwa siku. Je unajaribiwa kujiachia katika fikra na hisia za kukata tama? Katika siku ambayo unaona giza, unapoona kila kitu hakiko upande wako, usiogope. Mwamini Mungu tu. Anafahamu kile unachohitaji, na hatabadilisha agano lake kwa wale wampendao. Naye atawajalia watumishi wake waaminifu kipimo cha ubora wanachohitaji. Mtume Paulo anashuhudia kwamba, “Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.” (2 Wakorintho 12:9, 10). Prophets and Kings, uk. 164
Nguvu za wale ambao wanampenda na kumtumikia zitaongezwa na kufanywa upya siku hadi siku. Ufahamu wake utakuwa juu yao katika kazi yake ili wasikosee katika kutimiza kusudi lake. Sio vema kukata tama katika kazi ya Mungu. Imani yetu inatakiwa kustahimili msukumo unaojitokeza. Mungu anaweza na yupo tayari kuwapatia watumishi wake nguvu wanayohitaji. Atatimiza matazamio yao kwa upeo wa juu kuliko wanavotazamia wale wanaoweka matumaini yao kwake. Atawapatia hekima wanayohitaji katika utendaji mbali mbali. (Testimonies for the Church, vol. 8 uk. 10, 11)
Sisi wenyewe hatuwezi kupata au kufanyia mazoezi dini ya Kristo kwa sababu mioyo yetu ni midanganyifu kuliko vitu vyote, ila Yesu ambaye ni tabibu mkuu wa roho zetu, ambaye ana ustadi usiokosea, ndiye anayeweza kusoma mioyo ya wanadamu kuliko wao wenyewe, ametuonesha jinsi tunavyoweza kusafishwa kutoka katika dhambi. Kwa wale ambao wanahuzunikia ukosefu wa ubora, anasema “Neema yangu yakutosha,” kisha anasema “Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Yeye anafahamu mizigo hiyo kabla hata haijawekwa mabegani mwetu. Yesu anaiambia kila roho iliyojaribiwa kwamba, nipo tayari kukuimarisha kwa ajili ya majukumu ya maisha ya Kikristo. Tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; tutaangazwa na nuru kutoka katika paji la uso wake, itakayoakisi sura yake na kutufanya tukue na kufikia utimilifu wa kimo cha wanaume na wanawake katika Kristo Yesu. Dini yetu itavutia kwa sababu itanukia manukato ya haki ya Kristo. Tutafurahi kwa sababu chakula chetu na kinywaji chetu kitakuwa ni haki yake na amani na furaha. (Review and Herald, May 4, 1897, aya ya 11).
Ni jambo kubwa, tena jema ukiwa na uhusiano mzuri na Mungu, roho zetu kuwa na upatanifu na Muumba wetu. Malaika watatumwa kuokoa kutoka kati kati ya mifano ya uovu inayoambukiza, ambayo kwa udanganyifu wake unaoambukiza inaweza kushawishi roho kutoka katika wajibu. Lakini ikiwa tutakaribisha majaribu, hatuwezi kupata msaada wa kimbingu wa kutuwezesha kuyashinda. Wale vijana watatu walistahimili tanuru ya moto kwa sababu Yesu alitembea nao ndani ya ile miali ya moto. Kama wao wenyewe wangeingia ndani ya tanuru na kujaribu kutembea ndani ya moto, wangeungua mara moja. Ndivyo itakavyokuwa kwetu, ikiwa hatutaingia katika majaribu kwa makusudi tu, Mungu atatutegemeza pale majaribu yanapotukabili. (Signs of the Times, Sept. 2, 1897, aya ya 11)
Bwana anainua watu na kuwajaza Roho wake ndani yao akiwatayarisha kwa ajili ya kazi ambayo ni lazima ifanyike. Yeye mwenyewe ambaye ni Mungu wa kweli atawafanya wastahili kuwa ushuhuda ulio hai kwa ajili yake. Watakuwa mashahidi wa Mungu. Hawatajitokeza kwa msukumo wao wenyewe bali watashurutishwa na Roho wa Mungu kujitolea ili kutangaza ukweli. Mungu atawategemeza. Kila mwaka anaona kile kinachohitajika na kupanga mipango ya utendaji. Hatawaacha waende tu jinsi wanavyotaka. Ikiwa watu watakuwa tu ni watu, Mungu atatenda kazi ndani yao na kupitia kwao. (Review and Herald, May 25, 1897, aya ya 11)
MSHIPI
“Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.” (1 Petro 3:15)
Kwa kuhani mkuu kuweza kufungwa kwa mshipi wake ilimaanisha kwamba tayari alikuwa amevaa nguo zake zote, na yupo tayari kuhudumu. Vivyo hivyo, daima tunapaswa kuwa tayari kuhudumu na kushuhudia. Watu wa Mungu wanapaswa kutofautishwa kama watu wanaomtumikia wakati wote, kwa mioyo yao yote, wasiojichukulia heshima wenyewe, na wanaokumbuka kwamba agano la pekee kabisa ambalo wamejitoa kumtumikia Mungu, na Yeye peke yake. (Christian Service, uk. 236)
Kumtumikia Mungu kuna maana gani? – Ni kufanana naye katika tabia, kumdhihirisha. Kumtumikia Mungu, ni kumtii na kuzishika amri zake, kufanya ungamo la wazi la kusimama, si chini ya bango jeusi la yule muasi mkuu, lakini chini ya bango lenye damu ya Emanueli mwana wa Mfalme. Wale wanaomtumikia Mungu wanapambana kwa dhati kutii nia yake. Hivyo wanaonyesha kwamba ni jeshi gani wanalotumikia. (Signs of the Times, Feb. 1, 1889, aya. 3)
Katika kazi yoyote tutakayojihusisha nayo, neno la Mungu linatufundisha kutenda, “kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana.” “Lolote mkono wako utakalopata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako zote,” “mkijua ya kuwa mtapokwa kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo.” Warumi 12:11; Mhubiri 9:10; Wakolosai 3:24. (Christ Object Lessons, uk. 346)
Daima uwe tayari kuwapatia wengine nuru uliyoipokea. Dhihirisha kanuni za matendo yako; dharau kuficha kile chema ulichopata. Kunjua rangi zako; kwani wewe ni miwani kwa ulimwengu, kwa malaika, na kwa wanadamu. Usikwepe majukumu. Huwezi kumtumikia Mungu na Baali. Mungu anatamani wana na binti zake kusimama kwa hekima katika kweli, ili kwamba ulimwengu uweze kufahamu upande watakaosimama wakati wa hukumu. (Signs of the Times, Agost. 1, 1900, aya. 4)
Bwana anatamani muwe watu wa kuongoa roho; kwa sababu hiyo msipende kulazimisha mambo ya kiroho kwa watu, bali “Mwe tayari siku zote kumjibu kia mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.” 1 Petro 3:15. Kwa nini uhofu? – ogopa kwamba maneno yako yanakufanya ufurahie kujiona bora, usitamke maneno yasiyofunikwa na ushauri, maneno yako na matendo yako yasikose kufanana na Kristo. Jiunganishe kikamilifu na Kristo, na uonyesha ukweli kama ulivyo ndani yake. (Manual for Canvassers, uk. 34)
“Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele za watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” (Mathayo 5:16).
Mungu anatamani kila muumini awe muongoaji wa roho; na atawabariki wale wote wanaomtazama kwa ujasiri ili wapate hekima na uongozi. Kadiri wanavyotembea wakilindwa, wakitembea katika njia ya hekima, na kudumu kuwa wa kweli kwa Mungu wa Israeli, usafi na urahisi wa Kristo uliodhihirishwa katika uzoefu wa maisha, utashuhudia uwepo wa uchaji wa Mungu. Katika yote wanayosema na kutenda, watalitukuza jina la yule wanayemtumikia.
Muumini aliyejazwa na roho ya kweli ya umisionari, ni barua iliyo hai, inayofahamika na kusomwa na watu wote. Ukweli hutoka katika vinywa vyake bila maneno ya kujionyesha. Uchaji wake wa Mungu na ari pamoja na maamuzi yaliyotakaswa hukua kadri siku zinavyosonga, na dunia isiyoamini huona kwamba anaishi katika ushirika na Mungu akijifunza kutoka kwake. Maneno yanayonenwa na vinywa vilivyobadilishwa husindikizwa na nguvu inayogusa mioyo iliyo baridi ya wasioamini; hata wale wasiomfahamu Mungu wanaweza kutofautisha kati ya ubinadamu na uungu.
Ndugu na dada zangu, je, unaihisi nguvu ya utakaso ya ukweli mtakatifu katika moyo wako, na maisha yako, na tabia yako? Je, una uhakika kwamba Mungu, kwa sababu ya mwanawe wa pekee, amesamehe dhambi zako? Je, unapambana kuishi kwa dhamiri safi isiyo na hatia mbele za Mungu na mwanadamu? Je, unamsihi Mungu daima kwa niaba ya rafiki na jirani zako? Kama umefanya amani na Mungu, na umeweka yote juu ya madhabahu, unawea kujihusisha katika huduma ya kuongoa roho kwa faida. (Manuscript Release, vol. 8, pp. 212, 213)
Hebu maneno yetu na yawe ya upole kadri tunavyotafuta kuokoa roho. Mungu atakuwa hekima kwa yule anayetafuta hekima kutoka katika chanzo cha kimbingu. Tunapaswa kutafuta fursa kila mahali. Tunapaswa kukesha na kuomba, na kuwa tayari siku zote kumjibu kila mtu atuulizaye habari za tumaini lililo ndani yetu; lakini kwa upole na kwa hofu. Tusije tukawa na mguso mbaya kwa roho hata moja ambayo Kristo aliifia, tunapaswa kuinua mioyo yetu kwa Mungu, ili fursa inapojitokeza, tuweze kuwa na maneno sahihi ya kuzungumza kwa wakati muafaka. Hivyo unapojitoa kufanya kazi ya Mungu, Roho wake atakuwa msaidizi wako. Roho Mtakatifu atathibitisha ukweli uliozungumzwa kwa upendo kwa ajili ya nafsi hiyo. Ukweli utakuwa na nguvu ya kuwezesha utakapozungumzwa katika msukumo wa neema ya Kristo. (The Publishing Ministry, uk. 307)
KIFUKO CHA KIFUANI
“Basi ndugu, nawasihi kwa jina la Bwan wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja.” 1 Wakorintho 1:10
Mawe 12 yanayowakilisha makabila 12 ya Israeli yaliwekwa katika kifuko cha kifuani karibu na moyo wa Kuhani Mkuu. Kutoka katika hili tunajifunza ilivyo muhimu kwetu kusihi pamoja ili tuunganishwe katika upendo wa Kristo, na kudhihirisha upendo huo kwa watu, ndani na nje ya kanisa.
Siri ya mafanikio yetu katika kazi ya Mungu itapatikana kwa watu wetu kufanya kazi kwa umoja. Lazima kuwepo na utendaji wa pamoja. Kila mshiriki wa kanisa la Kristo anapaswa kufanya sehemu yake katika kazi ya Mungu, kulingana na uwezo aliopewa na Mungu. Tunapaswa kupambana pamoja dhidi ya vikwazo na magumu, bega kwa bega, kwa moyo mmoja.
Kama Wakristo wangetenda kazi kwa pamoja, wakisonga mbele kwa umoja, chini ya uongozi wa Nguvu moja, kwa ukamilishaji wa lengo moja, wangeugusa ulimwengu. (Christian Service, uk. 75)
Hakuna kazi kubwa zaidi kuliko uinjilisti wa vitabu, kwani uinjilisti huo unahusisha utendaji kazi wa majukumu ya kimaadili. Wale wanaoingia katika kazi hii wanahitaji kuwa chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu daima. Haitakiwi pawepo na kujitukuza. Tuna nini ambacho hatukukipokea kutoka kwa Kristo? Tunapaswa kupenda kama ndugu, kudhihirisha upendo wetu kwa kusaidiana. Tunapaswa kuwa na huruma na heshima. Tunapaswa kupambana pamoja, tukienda sambamba. Wale tu wanaoishi ombi la Kristo, wakilifanyia kazi katika maisha halisi, watashinda jaribu linaloujia ulimwengu. Wale wanaojitukuza wanajiweka katika nguvu za shetani, wakijiandaa kupokea uongo wake. Neno la Bwana kwa watu wake ni kwamba tuinue viwango juu na juu zaidi. Kama tukitii sauti, atafanya kazi pamoja nasi, na juhudi zetu zitatunukiwa mafanikio. Katika kazi yetu tutapokea Baraka nyingi kutoka juu na tutaweka hazina pembeni ya kiti cha enzi cha Mungu. (The Colporteur Evangelist, uk. 25)
“Ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja. Msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno, bali kwa unyenyekevu, kia mtu na mahesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.” (Wafilipi 2:2,3)
Kuna roho ya kujitegemea kwa wingi iliyojikita kati ya wajumbe. Hii inapaswa kuwekwa kando, na na kazi ya Mungu ifanyike kwa pamoja kwa watumishi wake. Kumekuwa na roho ya kuuliza kwa wingi kusema, “Kwani mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Alisema malaika, “Ndiyo, wewe ni mlinzi wa ndugu yako. Unapaswa kuwa mwangalizi wa ndugu yako, uwe na shauku kwa maendeleo yake, na kukuza roho njema yenye upendo kwake. Songeni mbele pamoja, songeni mbele pamoja,” Mungu alidhamiria kwamba mwanadamu awe na moyo mweupe na mkweli, bila tabia ya kujifanya, mpole, mnyenyekevu, na mwepesi. Hii ni kanuni ya mbinguni; Mungu aliiagiza hivyo. (Gospel Workers [1892], uk. 259)
Kuna ubaridi na utofauti mkubwa sana – roho iliyopo kwa wingi ni ya “Sijali” – na inatenda kazi kati ya wafuasi wa Kristo. Wote wanapaswa kuhisi hali ya kujali wenzake, kujali ustawi wa wengine na kulea roho ya upendo kwao. “Pendanpeni.” Ndipo tutakaposimama kama ukuta ulio imara dhidi ya mbinu za Shetani. Katikati ya upinzani na mateso hatutajiunga na wale wasiosamehe, hatutaungana na wafuasi wa mwasi mkuu, ambao kazi yao ya pekee ni kuwashtaki ndugu, kukashfu na kuchafua tabia zao.
Hebu masalia wa mwaka huu waboreshe katika kuharibu kila mzizi wa uchungu, na kuuzika katika kaburi pamoja na mwaka uliopita. Anza mwaka mpya na heshima, na upendo wa kina, kwa kila mshiriki wa familia ya Bwana. Songeni mbele pamoja. “Kwa umoja, tunasimama; kwa kutengana, tunaanguka.” Chukua nafasi ya juu na yenye heshima zaidi kuliko ulivyofanya hapo kabla. (Our High Calling, uk. 370)
Ikiwa Shetani atachochea ukosoaji kati ya watu wa Bwana waliochaguliwa, utasambaa kama mwali wa moto kutoka kwa mmoja kwenda kwa mwingine. Usiipatie roho ya ukosoaji nafasi, kwani ni sayansi ya Shetani. Ukiikubali sayansi hii, ukaionea shauku, wivu, na dhana ovu za kuhisi hisi zinajitokeza.
Sogeleaneni kwa pamoja, ni agizo ninalolisikia kutoka kwa Nahodha wa wokovu wetu. Sogeleaneni kwa pamoja. Panapokuwa na umoja, pana nguvu. Wote walio katika upande wa Bwana watasonga mbele kwa pamoja. Kuna hitaji la umoja na upendo thabiti kati ya wale wanaoamini katika kweli, na chochote kinachopelekea mafarakano ni cha mwovu. Mungu amekusudia kwamba watu wake wawe na umoja na yeye kwa namna matawi yalivyo na umoja na mzabibu. Kisha watakuwa na umoja wao kwa wao. (Selected Messages, kitabu cha 3, aya. 351, 352)
Hebu kila mmoja atafute kujibu ombi la Kristo: “Kwamba wawe na umoja, kama wewe, Baba, Ulivyo ndani yangu, name ndani yako.” Ni umoja wa aina gani huu! Na Kristo anasema: “Hivyo wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” (Testimonies for the Church, vol 5, aya. 488, 489)
URIMU NA THUMIMU
“Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahaamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.” (Waefeso 5:15-17)
Upande wa kulia na wa kushoto wa kifuko cha kifuani kulikuwa na mawe mawili yaliyokuwa na mng’ao mkubwa. Haya yalijulikana kama Urimu na Thumimu. Haya mawe yalimsaidia kuhani kutambua mapenzi ya Mungu. Swali lilipoletwa mbele za Mungu ili aamue, udhihirisho wa ukubali ulionekana kwa kung’aa jiwe la upande wa kulia. La, kama Mungu hakuridhia, ukungu wenye weusi ulizunguka jiwe la upande wa kushoto. Ni muhimu kwetu kuelewa kazi ya Kristo kwa niaba yetu na mapenzi Yake kwa maisha yetu leo.
Kila mtu ana nafsi ya kuokoa au kupoteza. Kila mmoja ana kesi inayosubiri kusikilizwa na Mungu. Kila mmoja anapswa kukutana na Hakimu mkuu uso kwa uso. Hivyo, ni muhimu kiasi gani, kwamba kila akili itafakari mara kwa mara tukio hili linalohusu wakati hukumu itakapowekwa na vitabu vitakapofunuliwa, wakati kila mtu anapaswa kusimama pamoja na Danieli, katika sehemu yake, katika mwisho wa siku. (Evangelism, uk. 222)
Katika mambo madogo na makubwa ya maisha swali la kwanza linapaswa kuwa, “Mapenzi ya Mungu ni yapi?” Kutii ni bora kuliko dhabihu, na kusikia kuliko mafuta ya beberu.” Kristo anawaita watoto wake kuachana na ubinafsi wa kila aina, tamaa zote, uchafu wote. “Njooni kwangu,” Anasema, “nami nitawapumzisha.” Jikiteni katika mafundisho yangu. Salimisheni mapenzi yenu kwa mapenzi yangu, njia zenu kwa njia zangu. Ruhusu maisha yenu yawe mamoja na maisha yangu. Hivyo mtapata thawabu ambayo itadumu hata uzima wa milele. (Signs of the Times, Feb. 19, 1902. aya. 13)
Mapenzi ya Mungu ni yapi? Nifanye nini ili nimtukuze Mungu? Ninawiwa kumtumikia Mwokozi wangu kwa moyo wote. Nikiyahesabu mambo yote kuwa kama mavi ili nipate Kristo. Mbingu, uzima wa milele, una thamani kuliko kila kitu kwangu, na Kristo alikufa ili niweze kumiliki utukufu ulio mzito wa milele… (That I May Know Him, uk. 203)
Kila jitihada inayofanywa kuvunja nguvu za tabia mbaya ni jitihada za kibinadamu. Ni mapenzi ya Mungu kwamba, kwa jitihada thabiti, tuinuke katika heshima ya usafi wa maisha, tukipata nguvu za kiroho, na kupata nguvu za kimaadili kupitia mazoezi ya vitengo Mungu alivyotupatia. Kuna furaha katika uwepo wa malaika wa mbinguni wakati vijana wanapopata ushindi katika jina la Yesu. (The Youth Instructor, Nov 12, 1896. aya. 6)
“Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu,” aliandika mtume Paulo, “kutakaswa kwenu.” 1 Thesalonike 4:3. Utakaso wa kanisa ni kusudi la Mungu katika mambo yake yote anayofanya kwa wanadamu. Amewachagua tangu milele, kwamba wawe watakatifu. Akamtoa mwanawe ili kufa kwa ajili yao, ili waweze kutakaswa kupitia katika kutii ukweli, kuvuliwa ubinafsi wa kila aina. Kutoka kwao anahitaji jitihada binafsi na kujisalimisha kikamilifu. Mungu anaweza kuheshimiwa na wale wanaotangaza kumwamini, kadri wanavyohakikishwa katika sura yake na kuongozwa na Roho wake. Kisha, kama mashahidi wa Mwokozi, wanaweza kutangaza kile neema ya kimbingu ilichowatendea. (The Acts of the Apostle, uk 559)
“Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu,” aliandika mtume Paulo, “kutakaswa kwenu.” 1 Thesalonike 4:3. Je, ni mapenzi yako pia? Dhambi zako zinaweza kuwa kama milima mbele yako; lakini kama ukinyenyekeza moyo wako na kuungama, ukiamini faida ya Mwokozi aliyesulubiwa na kufufuka, atakusamehe na kukusafisha na udhalimu wote. Mungu anahitaji utii wako kamili wa sheria yake. Sheria hii ni mwangwi wa sauti yake ikikwambia, takatifu zaidi, ndio, takatifu zaidi. Tamani ujazo wa neema ya Kristo. Ruhusu moyo wako kujazwa na shauku kubwa ya haki yake, kazi ambayo Neno la Mungu hutangaza kwamba ni amani, na matokeo yake ni ukimya na uhakikisho wa milele. (Acts of Apostles, uk. 566)
Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya. (2 Wakorintho 5:17)
Fursa kubwa imetolewa ili watu wa Mungu wapate ukamilifu wa tabia. Mtume anasema, “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu.” Hebu kila mmoja ajichotee kutoka katika chanzo kisichokoma cha nguvu za maadili na akili, ili kwamba aweze kufanya kazi za haki. Kupitia msalaba wa Kalvari kila kitu kimetengenezwa ambapo mwanadamu anaweaza kuwa na umoja na wanadamu wenzake, pia umoja na Kristo ndani ya Mungu. Baba anasema kwamba atawapenda wale wanaoamini kwamba Kristo aliwafia, kama anavyompenda Mwanawe pekee. Msalaba wa Kristo ni uthibitisho kwamba tunaweza kukamilika katika yeye. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Katika Kristo kuna uzuri, katika yeye kuna akili nyingi na maadili ya kutosha. (Review and Herald, Nov 30, 1897, aya 9)
Mungu anakunyooshea mkono mmoja, imani itashikilia mkono wake wenye nguvu, na kwa mkono mwingine, upendo uzifikie roho zinazopotea. Kristo ndiye njia, kweli, na uzima. Mfuate yeye, usitembee katika mwili, bali katika Roho. Tembea kama alivyotembea. Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu. Kazi unayotakiwa kuifanya ni kuyatenda mapenzi yake yeye anayehudumia maisha yako kwa utukufu wake. Mkifanya kazi kwa ajili yenu wenyewe, haitawafaidia kitu. Kufanya kazi kwa mafanikio ya wengine, kutojijali sana na zaidi katika udhati kujitoa kikamilifu kwa Mungu, kutakubalika mbele yake na atawalipa kwa neema yake yenye utajiri. (Testimonies for the Church, vol. 2, uk. 170)
CHETEZO
Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee. (Waebrania 7:25)
Chetezo na uvumba ni ishara ya maombezi ya Kristo kwa ajili yetu.
Kama mwombezi wetu, anatimiza kazi yake aliyojipa mwenyewe, akishikilia chetezo chenye maombi ya thamani ya mitume wake mbele ya Mungu yakichanganyika na maungamo, na shukrani za watu wake. (Christ Object Lessons, uk. 156).
Kristo kama mpatanishi wetu, akiwa mkono wa kuume wa Baba, siku zote anatuona. Ni muhimu kwamba atuombee kwa vile alitukomboa kwa damu yake. (Our High Calling, uk. 50).
Ninashukuru kwa sababu tunaweza kumwamini Mungu, naye anaheshimiwa tunapomwamini, tukimpelekea mashaka yetu. Bwana ambaye ni Yehova hakuona kuwa kanuni ya ukombozi ilikamilika kwa kuwekeza kwenye upendo wake. Kwa uteuzi wake mwenyewe ameweka katika madhabahu yake wakili aliyevikwa hali ya asili. Kama mwombezi wetu, kazi yake kubwa ni kututambulisha kwa Mungu kama wana wake na binti zake. Kristo anafanya maombezi kwa niaba ya wale waliompokea. Hao anawapa uwezo, kwa faida yake mwenyewe anawafanya ni sehemu ya familia ya kifalme, wazao wa mfalme wa mbinguni. Na Baba anadhihirisha upendo wake usio na kikomo kwa Kristo ambaye alilipa gharama ya ukombozi kwa damu yake na hivyo kuwapokea na kuwakaribisha marafiki wa Kristo kama marafiki wake. Ameridhika na upatanisho uliofanyika. Ametukuzwa kwa kuzaliwa kwa Mwana wake, kuishi na kufa na hatimaye kufanya upatanisho.
Ni kujishusha kwa namna gani huko? Ni fursa kubwa kiasi gani hiyo tuliyopewa? Kristo ndiye kiungo kati ya Mungu na mwanadamu. Kadiri tunavyomsogelea Mungu kupitia kwa mema ya Kristo, tunavikwa joho lake la kikuhani. Anatusogeza pembeni yake, akitukumbatia kwa mkono wa kibinadamu na mwingine ukishikilia kiti cha enzi cha milele. Anafanya kustahili kwake kuwe kama uvumba mzuri ndani ya chetezo kilichopo mikononi mwetu ili kuhimiza kusihi kwetu. Anaahidi kusikia na kujibu maombi yetu. Naam, Kristo amekuwa ni mapito ya maombi kati ya mwanadamu na Mungu. Yeye pia amekuwa ni mapito ya mibaraka kati ya mwanadamu na Mungu. Ameunganisha uungu na ubinadamu. (In Heavenly Places, uk. 77)
Na kadiri Kristo anavyotuombea, Roho wa Mungu anafanya kazi ndani ya mioyo yetu, akiweka ndani yetu sala na toba, sifa na shukrani. Shukrani inayobubujika kutoka katika midomo ya mwanadamu ni matokeo ya mguso wa Roho, akigusa nyuzi za roho na kuamsha muziki mtakatifu.
Maombi, sifa na toba ya watu wa Mungu inapanda kama kafara hadi hekalu la mbinguni. Kupanda huku hakufanyiki katika usafi usio na doa, bali hupitia kwenye mifereji ya kibinadamu iliyoharibiwa na dhambi kiasi kwamba isingekuwa kutakaswa na haki ya Kuhani wetu Mkuu, haya maombi, sifa na toba visingekubaliwa na Mungu. Kristo anakusanya maombi, sifa na kafara za watu wake na kuziweka katika chetezo, pamoja na hivyo anachanganya na kustahili kwa haki yake isiyokuwa na doa. Kisha kwa manukato ya uvumba wa upatanisho wa Kristo, maombi yetu yanakamilishwa na kupaa mbele za Mungu. Ndipo majibu ya utukufu yanarudi. (The Youth’s Instructor, April 16, 1903, aya ya 11, 12)
Uteuzi wa Mungu na vipaji vyake kwa niaba yetu havina kikomo. Kile kiti cha enzi chenyewe ni kivutio cha hali ya juu kwa sababu kinakaliwa na Yeye ambaye anaturuhusu tumwite Baba. Lakini Mungu hakuona kama kanuni ya ukombozi ilikuwa imekamilika akiwa amewekeza tu katika upendo wake. Kwa uteuzi wake mwenyewe aliweka katika madhabahu yake wakili aliyevikwa hali ya asili. (Testimonies for the Church, vol. 6, uk. 363)
“Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.” (Waebrania 4:15, 16)
Pale mwanadamu anapoelekea kwenye kiti cha rehema ndipo anapokuwa mteja wa Wakili Mkuu. Anapoanza tu kutamka toba yake na kuomba msamaha, Kristo anamkubali na kupokea kesi hiyo na kuifanya ni ya kwake. Ndipo anapoiwakilisha kwa kusihi mbele ya Baba kana kwamba ni ya kwake yeye mwenyewe.
Kadiri Kristo anavyoendelea na maombezi kwa niaba yetu, Baba anafungua hazina zote za Neema yake kwa ajili yetu. Ili tuzifurahie na kuziwakilisha kwa wengine. Yesu anasema, “Ombeni kwa jina langu” na kuongezea kwamba, “Sisemi kwamba nitawaombea kwa Baba, kwani Baba mwenyewe anawapenda kwa sababu mmenipenda. Tumieni jina langu, litayapatia maombi yenu ubora wa pekee, na Baba yangu atawapeni utajiri wa neema. Hivyo “ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.” Yohana 16:24. (Testimonies for the Church, vol. 6, uk. 364).
NJUGA NA MAKOMAMANGA
“Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.” Luka 21:28
Njuga katika kanzu ya Kuhani Mkuu iliwapatia watu waliokuwa nje ishara inayosikika kwamba alikuwa hai na anaendelea kufanya maombezi kwa ajili yao katika mahali patakatifu pa patakatifu. Kadiri Kristo anavyoendelea na maombezi katika chumba cha Patakatifu pa patakatifu, hata kama hatuwezi kusikia njuga hizo katika joho lake, tunatakiwa kuwa makini kwa ishara ambazo zinaashiria kumalizika kwa kazi yake kama Kuhani Mkuu na kisha aje kama Hakimu na Mfalme
Kuhani mkuu aliingia katika chumba cha pili (patakatifu pa patakatifu) mara moja baada ya matayarisho makubwa. Hakuna jicho la mtu mwingine lililoruhusiwa kuchungulia ndani ya kile chumba na kuona utukufu mkuu uliokuwa pale ila la kuhai mkuu peke yake. Hapo palikuwa ni mahali ambapo Mungu alichagua kudhihirisha utukufu wake. Kuhani mkuu aliingia mahali pale siku zote kwa kutetemeka. Watu waliokuwa nje walimsubiri kwa ukimya usiopimika wakifanya maungamo ya dhati. Tamaa yao kubwa ilikuwa ni kwamba Mungu awasamehe dhambi zao na kuwabariki. Mungu aliwasiliana na Kuhani Mkuu kutoka kwenye kile kiti cha rehema. Alipokawia kwa muda ndani ya hicho chumba, hofu iliwaingia watu wakidhani kuwa labda ni kwa ajili ya dhambi zao, au pengine ni za kuhani mkuu ndiyo maana utukufu wa Mungu umemwangamiza. Lakini pale sauti ya njuga zilizokuwa zimefungwa kwenye joho lake ziliposikika, walikuwa na amani wakijua kwamba yu hai humo. Ndipo hatimaye alitoka nje na kuwabariki watu. (The Spirit of Prophecy, vol. 1, uk. 274, 275)
Yesu alipokuwa akihudumu ndani ya chumba cha patakatifu pa patakatifu, nilisikia mlio wa njuga zilizokuwa zimening’inizwa kwenye joho lake, na alipotoka, wingu zito liliwafunika wakazi wa dunia hii. Wakati huo hapakuwa na mpatanishi kati ya mwanadamu mwenye hatia na Mungu aliyekosewa. (Early Writings, uk. 280)
Kristo aliwaagiza watu watu wake watazamie ishara za kuja kwake, na wafurahi kadiri zinavyoonekana kuashiria kuja kwa Mfalme. Aliwaambia kwamba, “Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.” Aliwaelekeza wafuasi wake kwenye mtini akisema, “…Utazameni mtini na miti mingine yote. Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu. Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu.” (Luka 21:28-31) (The Great Controversy, [1888], uk. 308)
Pale kwenye mlima wa mizeituni Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuhusu tukio la kuja kwake mara ya pili hapa duniani. Alitaja ishara maalum zitakazoonesha kwamba kuja kwake kumekaribia, na akawaagiza wakeshe na kuwa tayari. Alirudia maneno ya maonyo akisema, “Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa atakayokuja mwana wa Adam.” Kisha akawaonesha maana ya kukesha kwa ajili ya kuja kwake. Muda hautakiwi kutumiwa kwa kukaa tu na kusubiri kizemba, bali kufurahia kufanya kazi yake. (Christ Object Lesson, uk. 325)
Wapo watu duniani leo hii ambao wanafumbia macho ushuhuda ambao Kristo aliutoa kutahadharisha watu kuhusu kuja kwake. Wanajaribu kuzima ule uwezo wa watu wa kuelewa, wakati hizo ishara alizotaja zikitimia kwa haraka sana na ulimwengu unajitayarisha kwa wakati huo ambao Mwana wa Adam atadhihirishwa katika mawingu ya mbinguni. Paulo anafundisha kwamba ni dhambi kujifanya haujui hizo ishara zinazoashiria kuja mara ya pili kwa Kristo. Yesu aliwaita wale walio na hatia ya uzembe huu kuwa ni wana wa usiku na wa giza. Anawahimiza wanaokesha kwa maneno haya: “Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.” (1 Thesalonike 5:4-6) (The Acts of Apostles, uk. 260)
Tunasumbuka sana kuhusu hali halisi ya sasa ya kanisa lenye washiriki ambao kwa muda mrefu wamekuwa na uelewa na elimu ya haya matukio yanayoendelea kutimia karibu na mwisho wa wakati katika kutimiza historia ya unabii. Yesu anakuja na uweza na utukufu mkuu, “na hao wafu watahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.” Yule aliyesimama kama mwombezi wetu, anayesikia maombi yote ya toba na maungamo, anayewakilishwa na upinde wa mvua ambayo ni ishara ya neema na upendo, ukiwa umezunguka juu ya kichwa chake, hivi karibuni atakoma kufanya kazi anayofanya katika hekalu la mbinguni. Ndipo neema na rehema vitashuka kutoka katika kiti cha enzi, na haki itachukua nafasi. Yeye ambaye watu wake wamekuwa wakimwangalia, atashika nafasi yake – yaani ofisi ya Hakimu Mkuu. “Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote… Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu.” Petro anasema kuwa ni yeye aliyeagizwa kwamba, “Nao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.” Amechagua siku atakayouhukumu ulimwengu kwa haki kwa yule mtu aliyemchagua na kumweka wakfu. (Review and Herald, Jan.1 1889, aya ya 1)
AHADI ZA KUDAI KATIKA MAOMBI
Ahadi za Roho Mtakatifu
“Mwombeni Bwana mvua wakati wa masika, naam, Bwana afanyaye umeme, naye atawapa manyny ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni.” Zakaria 10:1
“Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao.” Luka 11:13
“Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia… Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.” Yohana 14:26;16:8
“Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.” Yohana 14:12-14
“Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.” Zakaria 4:6
Ahadi kwamba Mungu Hujibu Maombi
“Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.” Yohana 15:7
“Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.” Waebrania 4:16
“Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” Marko 11:24
“Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.” Zaburi 50:15
“Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.” Mathayo 18:19
“Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.” Mathayo 21:22
“Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.” Yohana 14:13, 14
“Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu.”Yohana 16:23, 24
“Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.” 1 Yohana 5:14, 15
Ahadi Kuhusu Nguvu ya Mungu
“Kuna neno gani lililo humu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na sara atapata mwana wa kiume.” Mwanzo 18:14
“Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.” Kutoka 14:14
“Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu.” Marko 10:27
“Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya.” 1 Thesalonike 5:24
“Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.” Ayubu 42:2
“Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?” Warumi 8:31, 32
“Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?” Hesabu 23:19
“Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu wala hawatazimia.” Isaya 40:28-31
Ahadi kwa ajili ya Ulinzi wa Mungu
“Je! Si mimi niliyekumuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.” Yoshua 1:9
“Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.” Mwanzo 28:15
“Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengenezea.” Kutoka 23:20
“Lakini huko, kama mkimtafuta Bwana, Mungu wako, utampata, ukimtafuta kwa moyo wako wote, na roho yako yote.” Torati 4:29
“Niite, nami nitakuitikia, nami nitakonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.” Yeremia 33:3
“Kila bonde litainuliwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patasawazishwa.” Isaya 40:4, 5
“Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.” Zaburi 32:8
“Naye Bwana, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.” Torati 31:8
“Ni nani amchaye Bwana? Atamfundisha katika njia anayoichagua.” Zaburi 25:12
“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.” Mithali 3:5, 6
“Na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri.” Isaya 58:10, 11
“Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia.” Isaya 65:24
Ahadi kwa ajili ya Moyo Uliobadilishwa
“Nami nitawapa moyo, wanijue ya kuwa mimi ni Bwana; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao; kwa maana watanirudia kwa moyo wao wote.” Yeremia 24:7
“Bwana, Mungu wako, atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao wako, ili umpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai.” Torati 30:6
“Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama.” Ezekieli 36:26
“Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu.” Wafilipi 1:6
“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.” 2 Wakorintho 5:17
“Nimesulubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa
Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” Wagalatia 2: 20
“Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu n miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” 1 Wathesalonike 5:23, 24
Ahadi kwa Msamaha
“Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.” 2 Nyakati 7:14
“Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao.” Zaburi 86:5
“Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.” Marko 11:25
“Tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.” Waefeso 4:32
“Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” 1 Yohana 19
“Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” Isaya 1:18
“Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.” Isaya 43:25
“Maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.” Yeremia 32: 34
“Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.” Waefeso 1:7
Ahadi kwa Ushindi Dhidi ya Dhambi
“Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.” 1 Yohana 5:4
“Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.” Warumi 8:37
“Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.” 1 Wakorintho 15:57
“Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.” Isaya 41:10
“Zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya Yule mwovu.” Waefeso 6:16
“Nimesulubiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa
Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” Wagalatia 2: 20
“Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.” Wafilipi 2:13
“Basi nasema, Enendeni kwa Roho, waa hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.” Wagalatia 5:16
“Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema yaBwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi. Amina.” Warumi 16:20
“Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” Warumi 12:2
“Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.” 1 Yohana 2:15
Ahadi za Uponyaji
“Akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzshika amri zake, mimi sitatia juu yako maadhi yo yote niliyowatia Wamisi; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.” Kutoka 15:26
“Makomeo yako yatakuwa ya chuma na shaba; Na kadiri ya siku zako ndivyo zitakavyokuwa nguvu zako.” Torati 33:25
“Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema, Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai.” Zaburi 103:2-5
“Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.” Mithali 3:7, 8
“Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” Isaya 53:3-5
“Uniponye, Ee Bwana, name nitaponyeka; uniokoe, name nitaokoka; kwa maana wewe ndiwe uliye sifa zangu.” Yeremia 17:14
“Maana nitkurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema bwana, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye.” Yeremia 30:17
“Tazama, nitauletea afya na kupona, name nitawaponya; name nitawafunulia wingi wa amani na kweli.” Yeremia 33:6
“Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langum jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake; nanyi mtatoka nje, na kucheza-cheza kama ndama wa mazizini.” Malaki 4:2
“Mtu kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.” Yakobo 5:14, 15
Ahadi kwa ajili ya Nguvu za Kufanya Mapenzi ya Mungu
“Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.” Zaburi 27:14
“Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku wa siku. Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana; tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.” 2 Wakorintho 4:16-18
“Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.” Wagalatia 6:9
“Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” Wafilipi 4:13
“Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.” Wafilipi 2:13
“Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza kwa Kristo ukae juu yangu.” 2 Wakorintho 12:9
Ahadi Kuhusu Kuwa Mashahidi wa Mungu
“Msiogope wala msifanye hofu; je! Sikukuhubiri haya zamani na kuyaonyesha? Na ninyi ni mashahidi wangu. Je! Yuko Mungu zaidi yangu mimi? Hakika hapana Mwamba; mimi sijui mwingine.” Isaya 44:8
“Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia.” Isaya 60:1
“Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho.” 2 Wakorintho 5:18
“Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru.” Yeremia 1:7
“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Matendo 1:8
“Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.” 1 Petro 2:9
“Mwe tayari siku zote kumjibu kila awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.”
Kuhani Mkuu
Mavazi ya Kuhani Mkuu yalitengenezwa kwa aina ya vitambaa vilivyokuwa vya gharama sana, na yalitengenezwa kwa namna ya kupendeza kwa ufundi mkubwa sawasawa na daraja hilo lililokuwa la juu sana. Pamoja na vazi la kitani alilovaa kuhani, alikuwa na joho la rangi ya samawi juu yake, ambalo pia lilifumwa kuwa kipande kimoja. Kwenye upindo wake liliwekewa njuga za dhahabu na makomamanga ya rangi ya samawi, zambarau, na nyekundu. Upande wa nje kulikuwa na naivera, ambayo ilikuwa ni vazi fupi la rangi ya samawi, zambarau, nyekundu na nyeupe. Ilishikizwa na mkanda wenye mchanganyiko wa rangi hizo hizo ukitengenezwa kwa namna ya kupendeza. Naivera haikuwa na mikono, na katika mabega yaliyokuwa yametarizwa na nyuzi za dhahabu kulikuwa na vito viwili vya shohamu, vilivyokuwa na majina ya makabila kumi na mawili ya Israeli.
Juu ya naivera kulikuwa na kifuko cha kifuani, hiki kilikuwa ni kitakatifu sana katika mavazi ya kikuhani. Kilitengenezwa kwa namna naivera ilivyotengenezwa. Sura yake kifuko cha kifuani ilikuwa ni ya mraba upana wa naivera, kilining’inizwa kutoka mabegani kwa utepe wa samawi ulioshikizwa kwa pete za dhahabu. Upindo wa kifuko hiki uliwekewa vito kadhaa vya thamani sawa sawa na vito vinavyooneshwa kutengeneza misingi ya ule Mji wa Mungu. Pembeni kabisa kulikuwa na mawe kumi na mawili ya dhahabu yaliyopangwa kwa safu nne, na haya pia yalichongwa majina ya makabila ya Israeli. Agizo la Bwana lilikuwa ni kuwa, “Na Haruni atayachukua majina ya wana wa Israeli katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu juu ya moyo wake, hapo atakapoingia ndani ya mahali patakatifu, kuwa ukumbusho mbele ya Bwana daima.” Kutoka 28:29. Kwa hiyo Kristo aliye Kuhani Mkuu, akimsihi Baba kwa ajili ya damu yake kwa niaba ya wenye dhambi, anayo majina katika moyo wake ya walioamini wakatubu na kuungama . Mtunga Zaburi anasema, “Nami ni maskini na mhitaji, Bwana atanitunza. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee Mungu wangu, usikawie.” Zaburi 40:17
Upande wa kulia na wa kushoto wa kifuko cha kifuani kulikuwa na mawe mawili yaliyokuwa na mng’ao mkubwa. Haya yalijulikana kama Urimu na Thumimu. Haya mawe yalimsaidia kuhani kutambua mapenzi ya Mungu. Swali lilipoletwa mbele za Mungu ili aamue, udhihirisho wa ukubali ulionekana kwa kung’aa jiwe la upande wa kulia. La, kama Mungu hakuridhia, ukungu wenye weusi ulizunguka jiwe la upande wa kushoto.Kofia ya kuhani mkuu ilikuwa ya kitani nyeupe ikiwa na upindo wa samawi, na utepe wa dhahabu wenye maneno haya: “Mtakatifu kwa Yehova.” Kila kitu kilichounganika na mavazi pamoja na mwenendo wa kuhani mkuu kilikusudiwa kuleta mguso kwa yeyote aliyemwona na kuhisi utukufu wa Mungu, utakatifu wa ibada yake, na usafi unaotakiwa kwa wale wanaosogelea uwepo wake. (Partiarchs and Prophets, uk. 350, 351).
Play Now ᐈ Find the Best Casino Games In India | DRMCD
JibuFutaLooking for the 평택 출장마사지 best casino slots for Indian players? Get instant access to 경상남도 출장샵 top 원주 출장샵 casino games in 포항 출장안마 India including top slots, 전주 출장안마 blackjack, roulette,