Jumapili, 4 Februari 2018

UNABII WA BIBLIA

UTHIBITISHO KWAMBA MUNGU YUPO
Biblia ni kitabu cha ajabu kuliko vyote. Maelezo yake kuhusu chanzo cha uovu; taarifa yake isiyo na kasoro kuhusu
mahusiano ya Mungu na taifa la Israel; ujumbe wake unaopenya kupitia kwa manabii wao; ‘habari njema’ yake
iliyohubiriwa na Yesu Kristo na mitume wake; na juu ya yote uchambuzi wake sahihi uhusuo mapungufu ya silka ya
mwanadamu ukilinganishwa na utakatifu, kweli na rehema ya Mungu, iliyodhihirishwa zaidi hasa katika Mwanawe
- haya yote ni mambo ya kipekee yasiopatikana katika kitabu kingine chochote duniani. Haya yalimfanya Henry
Rogers, miaka 100 iliyopita kusema: “Biblia sio namna ya kitabu ambacho mwanadamu angekuwa ameandika kama
angeweza, au angeweza kuandika angeweza”. Kwa maneno mengine, Mungu anahitajika katika kuelezea uwepo
wake.
Katika kazi hii fupi tutaangalia mojawapo ya mambo yake ya ajabu: unabii wake. Kihalisi, unabii sio kuelezea tu
mambo ya mbeleni. Nabii alikuwa ni mtu ‘aliyesema kwa niaba’ ya mwingine, msemaji; na unabii ulikuwa ni
ujembe alioutoa nabii kwa niaba ya Mungu. Lakini kwa kuwa unabii wa Biblia unao pia ‘utabiri’ mwingi wa mambo
yajayo, kwa lengo hili tu tutazingatia maana hiyo hapa.
NANI MWENYE MAMLAKA YA UNABII?
Lakini kwanza inabidi tukubaliane juu ya swali moja la muhimu: Biblia inadai kwamba mamlaka ya unabii inatoka
kwa Mungu tu na ni uthibitisho wa uweza wake?
Kwa hili lipo jibu muafaka katika unabii wa Isaya. Katika kifungu cha 41 Mungu anazitaka sanamu na
wanaoziabudu wa nyakati zile kuthibitisha kama wanazo nguvu za kiungu. Hivi ndivyo anavyoziambia: “Haya
leteni maneno yenu, asema BWANA; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema Mfalme wa Yakobo. Wayatangaze na
kutujulisha yatakayokuwa; watuonyeshe mambo ya zamani, ni mambo gani, tukapate kuyatia moyoni, tukajue
mwisho wake; au wamdhihirishie yatakayotokea baadaye.” (Ms. 21 – 22)
Msingi wa changamoto hii ni dhahiri: Wanaoabudu kipagani wanadai kuwa sanamu zao ni Miungu. Sawa;
wathibitishe basi! Na uthibitisho unaotakiwa na Mungu mwenyewe ni kwamba sanamu zitabiri mambo yajayo na
pia kutangaza ‘yaliyopita’, yaani kueleza jinsi uumbaji ulivyokuwa hapo mwanzo. Katika msitari unaofuata dhana
hii iko wazi sana.
“Tujulisheni yatakayokuwa baadaye, nasi tutakiri ya kuwa ninyi ni miungu….” (Ms. 23)
Hapa Mungu mwenyewe anatujulisha kwamba kuweza kutabiri mambo yajayo ingekuwa uthibitisho wa uweza wa
kiungu. Kwa zaidi ya mara moja katika sehemu hii ya unabii wa Isaya, Mungu anatangaza ya kwamba Ni yeye
pekee aliye na uwezo huo; kwa kuwa Ni yeye pekee aliye Mungu, hakuna mwingine.
“Kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine, mimi ni Mungu, wala
hapana aliye kama mimi……” (46:9)
Mungu wa Israeli hapa anatangaza kwamba hakuna kitu kinachostahili kuabudiwa ila yeye; na anaendelea kusemea
ishara za nguvu zake kwa maneo haya.
“…nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, shauri langu
litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.” (46:10)
Lifikirie, nani awezaye kusema, “Mapenzi yangu yatasimama…” zaidi ya Mungu? Ni nani katika dunia nzima
awezaye kusema kitu kama hicho? Kusemea hili inahitaji mwenye uwezo wa kujua mambo yajayo kabla
hayajatokea, lakini awezaye kuhakikisha yanaenda alivyopanga. Kwa maneno mengine, kutoa unabii utakaotimia
kwa vyovyote, unamhitaji Mungu. Hakuna namna nyingine ya kuelezea.
Agano jipya linadai hivyo hivyo. Wakati Yesu alipokuwa anakaribia kuwaacha wanafunzi wake, aliwaahidia
msaada wa Roho Mtakatifu katika jukumu lao la kuihubiri injili duniani. Mojawapo ya matokeo ya karama hiyo
ingekuwa, “na mambo yajayo atawapasha habari yake.” (Yoh. 16:13); kwa maneno mengine wafuasi wangepewa
ufahamu wa mambo yajayo. Kwa vyovyote inamaanisha wasingepewa karama hiyo ya kipekee wasingeweza
kuyajua. Uweza wao kutambua yajayo ndio ungekuwa ushahidi wa nguvu ya kiungu waliyotunukiwa.
Tena, katika kitabu cha mwisho cha Biblia, kifungu 1, msitari 1, inaelezwa kwamba Mungu alimpa Yesu Kristo
Ufunuo, “awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi…” (Uf. 1:1). Ufahamu
wa mambo yajayo ulitoka kwa Mungu, kupitia kwa Kristo; bila ufunuo huo watumishi wake wasingelijua lolote
linalouhusu.
Hitimisho ni wazi: Biblia inasema kiuhakika ya kwamba uweza wa kutabiri yajayo ni wa Mungu pekee.
BIBLIA INATABIRI YAJAYO?
Tunaweza tu kuchunguza historia na uzoefu wetu kutambua kwamba wanadamu kwa jinsi walivyo, hawawezi kujua
hata kidogo ya mbeleni. Kwa nini? Hatuwezi hata kujua litakalotupata usiku wa leo, au kesho tukienda kazini,
achilia mbali mwaka kesho; au litakaloipata dunia katika miaka 100, hata tusiposemea miaka 2000! Watu
wangekuwa na utambuzi kidogo tu wa mambo yajayo, maamuzi mengi yangebadilika kiasi gani! Ajali nyingi kiasi
gani zingeepukwa! Maafa mengi kiasi gani yasingeliachiwa yatokee. Vita vingi kiasi gani visingeanzishwa! Uzoefu
katika maisha yetu wenyewe, na wa historia ya mwanadamu unatuonyesha kuwa mwanadamu hana ufahamu
wowote wa hakika wa litakalotokea.
Lakini chukulia kwamba mambo yajayo yameelezewa, sio mara moja, bali mara nyingi. Na kwa nyakati zote katika
kitabu hicho hicho, Biblia na sio katika kingine chochote duniani! Halipaswi hilo kutufanya tukae chini na
kuzingatia? Ndio maana tunasema kwamba unabii wa Biblia ni wa maana sana, na unapaswa kuchunguzwa kwa
makini, kwa kuwa mambo mengi mno yanautegemea. Ni kiashiria ya kwamba upo katika dunia uweza mkuu na
nguvu impitayo mwanadamu.
“ndio, lakini…”
Wale wasioamini kwamba Biblia ni Neno la Mungu, hawapendi kabisa unabii wake. Unapokubali imetabiri kisahihi
mambo kabla ya kutokea utakuwa umeanza kukubali uwepo wa Mungu… Kwa hiyo wanajaribu kuielezea mbali.
“Unabii,” wanasema, “haukuwa hasa utabiri wa mambo. Uliandikwa baada ya matukio ‘unayoyabashiri.’
Sasa hii hoja inaweza kuwa na nguvu kama unaweza kuthibitisha kuwa yale yaliyoandikwa katika Biblia, na hasa
yale ya Agano la Kale kwamba yaliandikwa baada ya matukio yanayodaiwa kutokea. Lazima tuseme hapa wazi
kwamba hawana uthibitisho wa moja kwa moja juu ya hili; hitimisho lao ni matokeo tu ya kutafsiri mambo
kujiridhisha wapendavyo. Ukweli ni kwamba, utafiti wote uliofanywa katika miaka 100 iliyopita unaonyesha
kwamba yaliyoandikwa katika Biblia ni halisi; ni ya nyakati zinazodaiwa kuandikwa.
Lakini kuna njia ya mkato katika jambo hili inayoweza kutusaidia katika lengo letu. Hakuna anayeweza kubisha
kudai kwamba maandiko ya Agano la Kale hayakuwepo miaka 200 kabla ya kuzaliwa Kristo, kwa kuwa
yalitafsiriwa katika Kiyunani wakati huo, na huwezi kutafsiri kitu kisichokuwepo!
Ubishi mwingine ni kusema, “Ndio, unabii huu wa Biblia ni utabiri wa kijanja wa kisiasa wa watu waliokuwa
wakichunguza matukio enzi zao na kuona mwelekeo wa matokeo yake.”
Utabiri wa kijanja kisiasa! Uliotolewa karne nyingi kabla ya Kristo na unaoendelea kuwa kweli miaka 2000 hadi
leo! Hao manabii walikuwa wachawi wa namna gani kuweza kufanikisha hilo bao? Kusema hivyo ni kuonyesha tu
yasivyowezekana maelezo yake.
Lakini jibu la hakika kwa ubishi huu kama ilivyo kwa ubishi mwingine wowote, ni kusoma sehemu ya unabii
wenyewe. Kwa hiyo tunaanza na:-
UNABII KUHUSU BABELI
Katika enzi ya manabii wa Israeli (Kama 850-560 K.K) kuliinukia dola mbili kuu katika maeneo yanayoizunguka
mito ya Frati na Tigrisi, katika Iraki ya sasa. Ya kwanza ilikuwa dola ya Ashuru iliyokuwa na makao makuu Ninawi.
Kwa karne mbili, Waashuru walivamia ardhi ya mataifa waliowazunguka: kusini wakawatawala Wakaldayo na
makao makuu yake Babeli; Magharibi wakaikalia Shamu, na kuendelea chini katika pwani ya Bahari ya Kati,
kupitia Israeli mpaka Misri. Sera yao ilikuwa ya kigaidi. Lengo lao lilikuwa kuwatisha wakazi wa maeneo hayo
watii na kulipa kodi kwa mwaka. Kufanikisha hili waliiswaga miji kiuporaji na kuichoma moto, wakavibamiza vijiji,
na kuua wakazi na kuchukua maelfu ya mateka Ashuru.

Katika nusu ya pili ya karne ya saba (K.K), nguvu ya Ashuru ilipungua na Babeli ikaanza kupanda. Katika mwaka

612 (K.K), Ninawi uliangushwa. Nebukadreza, mfalme wa Wakaldayo, haraka akaanzisha dola mpya. Mataifa
madogo madogo Mashariki ya Kati yalipokuwa yanashangilia uhuru wao kutoka Ashuru, mara yakajikuta
wakivamiwa na majeshi ya Babeli. Na hasa Nebukadreza akaivamia Israeli akaiteka Yerusalemu, akalichoma hekalu
lake na kuchukua maelfu ya mateka Babeli. Akaendelea kusini zaidi na kuivamia Misri. Dola ya Babeli ilikuwa ni
awamu ya pili ya utawala huu wa kijeshi. Ulikuwa katika eneo la Frati.
Na hasa Nebukadreza, mfalme wake mkuu kabisa aliujenga mji mkuu wa Babeli kuwa fahari ya dunia katika
Mashariki ya Karibu. Alijenga Mahekalu makubwa na majumba ya kifalme, na kuzungushia jiji hilo ukuta mkubwa
sana kuulinda. Babeli ukawa utukufu na fahari kuu kwa Nebukadreza mwenyewe na Wakaldayo wake.
Ni vigumu kwetu sisi kwa sasa kutambua athari za utawala kama huo wa kimabavu na uharibifu wa mali kwa
wakazi wa mataifa madogo. Kwao dola za Ashuru na Babeli zitakuwa zilionekana tishio na zisizoshindwa.
MAANGUKO KAMILI
La ajabu, miaka 100 kabla Babeli haijafikia kilele cha ukuu wake, nabii Isaya alishatabiria kuangushwa kwake kwa
maneno thabiti sana. Katika kifungu kilichopewa kichwa cha habari ‘Mzigo wa Babeli’ ni hivi alivyosema.
“…Siku ya BWANA i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu…Tazama,
nitawaamsha Wamedi juu yao…Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama
Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza. Hautakaliwa na watu tena kabisa… Mwarabu hatapiga hema yake
huko, wala wachungaji hawatalaza makundi yao huko. Lakini huko watalala hayawani wakali wa nyikani” (Isaya
13:6,17,19-21)
Hatima ya Babeli inaeleweka: wavamizi watakuwa Wamedi (taifa mashariki ya Babeli); jiji litakuwa maganjo,
lisilokaliwa na mtu wala mnyama pori. Tukumbuke utabiri huu ulitolewa miaka 100 kabla ya Babeli kukua kufikia
nguvu na utukufu wake.
Nabii mwingine, Yeremia, akiandika miaka 100 baadaye, wakati Nebukadreza alipokuwa akikaribia kuivamia
Yerusalemu, aliongeza mtazamo juu ya anguko la Babeli.
“BWANA asema hivi, Angalia, nitaamsha juu ya Babeli upepo uharibuo… Babeli umeanguka na kuangamia
ghafla… Wekeni mataifa tayari juu yake, wafalme wa Wamedi… Babeli utakuwa magofu, makao ya mbwa-mwitu,
ajabu, na mazomeo pasipo mtu kukaa huko… kuta pana za Babeli zitabomelewa kabisa, na malango yake marefu
yatateketezwa… Ee BWANA, umenena habari za mji huu kwamba utakatiliwa mbali, usikaliwe na awaye yote,
wala wanadamu wala wanyama, lakini uwe ukiwa hata milele…”
Na mwishowe nabii anaamriwa kufunga jiwe kwenye gombo la unabii ule na kulitupia ndani ya mto Frati, aseme,
“Hivyo ndivyo utakavyozama Babeli, wala hautazuka tena…”(Yer:51:1,8,28,37,58,62-64)
Uwiano kati ya unabii wa Isaya, ulioandikwa miaka 100 kabla ya mamlaka ya Babeli kushamiri, na ule wa Yeremia,
ulioandikwa wakati dola na jiji vilipokuwa katika kilele cha utukufu wake ni mtimilifu. Kwa watu wa siku zile
itakuwa ilionekana kama ilivyo kwetu leo tuambiwe miji mikubwa kama London, New York au Sydney
itaangamizwa ibakie magofu milele. Katika enzi hii ya silaha za nyuklia, jambo hilo linawezekana; lakini manabii
wa Israeli walitamka hayo zaidi ya miaka 2500 iliyopita wakati hakuna ambaye angeweza kuota kwamba uharibifu
kamili namna hiyo ungewezekana.
Historia inaonyesha jinsi ambavyo unabii huo wa maanguko ya Babeli ulivyotimizwa hatua kwa hatua. Wavunjaji
wa Kwanza walikuwa Wamedi na Wajemi katika karne ya sita (K.K). Kuanzia wakati huo umwamba wa Babeli
ulianza kufifia. Baadaye walikuja Wayunani chini ya Aleksanda Mkuu, wakifuatiwa na Warumi; baada yao
makabila kadhaa yapendayo vita kama Wapathi, Waarabu na Watarta.

Kwa karne nyingi mahali halisi pa jiji la Kale la Babeli palikuwa mahame, yaliyoepukwa - wasafiri wasemavyo - na

wahamaji wanaotangatanga. Ni hivi karibuni tu wataalamu wa kihistoria wachimbuao chini (Archaeologists),
walipochunguza eneo hilo katika nusu ya kwanza ya karne ya 19, na kugundua mabaki ya kuta kubwa, mahekalu ya
nguvu na malango, na masanamu makubwa yaliyoonyesha ulimwengu ulioshikwa na butwaa jinsi ukuu wa Babeli
ulivyokuwa enzi zake.
Kwa hiyo historia inatuonyesha jinsi Babeli ‘Utukufu wa falme,’ ulivyoangushwa na kuachwa, kama manabii wa
Israeli walivyotabiri ingekuwa.
Sasa tunageukia mfano wa pili unaotofautiana, unaotuonyesha pia uhakika wa unabii wa Biblia katika:-
HATIMA YA MISRI
Misri iliwahi pia kuwa dola yenye nguvu kubwa katika Mashariki ya Kati. Ukubwa wake ulikuwa kama 1600 (K.K)
wakati majeshi ya Mafarao wavamizi walipojisogeza kusini ndani ya Sudani, Magharibi kuambaa pwani ya Afrika
ya kaskazini, kaskazini kupita ardhi ya Kaanani (baadaye Israeli), na ndani ya Syria. Uvumbuzi kaatika baadhi ya
Mahekalu ya kale, minara na makaburi umedhihirisha utukufu wa Mafarao ulivyokuwa katika kilele cha kuu wao.
Lakini ilipofikia miaka ya 1400 K.K nguvu ya Misri ilianza kurudi nyuma kutokana na vita vya wenyewe kwa
wenyewe na kukua kwa Ashuru, na baadaye Babeli. Hata hivyo katika kipindi Waisraeli walipokuwa wakiikalia
Kanaani, 1400-600 K.K, Wamisri waliingilia kati kwa nyakati mbalimbali siasa za Mashariki ya Kati, kwa
mafanikio fulani. Waisraeli, walipokuwa wakiogopa uvamizi kutoka Ashuru na Babeli mara kwa mara
walishawishika kutafuta msaada Misri badala ya kumtumainia Mungu wao.
Sasa manabii wa Israeli walikuwa na kitu maalum sana kusema juu ya hatima ya Misri. Nabii Ezekiel, ambaye
matamko yake yalitolewa katika siku za Nebukadreza, mfalme wa Babeli, kuanzia kama 600 K.K, alitangaza
kwamba kutokana na hukumu ya Mungu, Misri ingekuwa upweke kwa miaka 40. Baada ya hapo kungekuwa na
uamsho, lakini usiofikia ukuu wa nguvu zake za awali.
“Maana Bwana MUNGU aseme hivi; Mwisho wa miaka arobaini nitawakusanya Wamisri, na kuwatoa katika hizo
kabila za watu, ambazo walitawanyika kati yao; nani nitawarudisha hata nchi ya Pathrosi, hata nchi ya kuzaliwa
kwao; na huko watakuwa ufalme duni (ufalme wa chini). Utakuwa duni kuliko falme zote; wala hatajiinua tena juu
ya mataifa; nami nitawapunguza ili wasitawale tena juu ya mataifa… Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaviharibu
vinyago, nami nitavikomesha vitu vya ubatili katika Nofu (Memphis), wala hapatakuwa na mkuu tena atokaye
katika nchi ya Misri. Ezk. 29:13-15; 30:13
Hapa napo maana ya unabii huu inaeleweka: Misri ingekabiliwa na matatizo ya uvamizi na watu kuchukuliwa
mateka. Ingawa hakuna kumbukumbu halisi zilizobakia za matukio hayo, lazima yatakuwa ni matokeo ya uvamizi
wa Wababeli kwa Misri, kama Ezekiel mwenyewe alivyotabiri (tazama Ezek: 30:17-20). Lakini huo usingekuwa
mwisho wa Misri. Maana baada ya miaka 40, mateka wangerudi tena katika nchi yao wenyewe. Misri, kama ufalme
usingeangamizwa: ungedumu lakini nguvu yake ingeshushwa sana - “Ufalme mdogo,” usioweza kutumainia nguvu
zake kukabili mataifa yanayopakana nayo tena.
Ufalme mdogo
Na ndivyo ilivyotokea. Tangu kama mwaka 600 K.K, Misri aliangukia chini ya watawala wa kivamizi, kwanza wa
Wababeli katika karne ya 6 K.K; kisha Waajemi kati ya karne ya 6 na 4; alafu Wayunani katika karne ya 4;
wakifuatiwa na Warumi karne ya kwanza K.K mpaka karne ya 5 B.K. Walifuatiwa na Waarabu na Waturuki kutoka
karne ya 7 B.K na kuendelea. Hata Waingereza wameitawala Misri kwa kipindi katika karne ya 19. Kwa miaka
2500, Misri imebakia kama alivyotabiri Ezekiel kuwa ingekuwa, “Ufalme wa chini,” wakati wote ikikaliwa na
wengine. Lakini Misri na Wamisri hawakutokomea. Bado wapo, na wameponea uhuru kiasi miaka ya karibuni,
washukuru misaada mikubwa ya fedha wanayopata kutoka Marekani na Saudi Arabia.
Tuweke pembeni kidogo mawazoni swala la Misri wakati tukiangalia mfano wa tatu wa utabiri wa Biblia wa
matukio ya mbele, kwa kutazama.

UNABII KUHUSU ISRAELI

Huu ndio uliojaa kuliko wote, kimaelezo ya utabiri wake, na pia katika wingi wa thibitisho zihusuzo ukweli wake
kimatukio kihistoria. Tutazingatia tu mambo halisi mepesi yahusuyo hatima ya ajabu ya Waisraeli.
Agano la Kale limeandika kwa ajili yetu jinsi Mungu alivyofanya ahadi madhubuti kwa Ibrahim (Kama 1800 K.K),
iliyokuwa imemaanisha kati ya mengi kwamba, uzao wake ungekuwa taifa (Israeli), ambalo lingeimiliki nchi ya
Kanaani, iliyoitwa baadaye Palestina. Kama 1400 K.K. Waisraeli walitolewa Misri wakati wa ‘Kutoka’ chini ya
Mussa, na miaka 40 baadaye walianza kurithishwa nchi waliyoahidiwa. Lakini kabla ya hapo, kabla hawajaingia
hiyo nchi, walionywa sana na Mungu kupitia kwa Mussa mkosi ambao ungewapata kama wakimwacha Mungu wao
na kuabudu sanamu, na kuiga mambo ya Wapagani wa Kikanaani. Katika mlango wa 28 wa Kumbukumbu la Torati,
kuna unabii wa ajabu sana – na ulikuwa onyo kali – juu ya balaa ambalo lingewafika Waisraeli kama hawakuwa
watiifu. Msomaji anashauriwa kujisomea kifungu chote mwenyewe. Hapa tuna nafasi ndogo tu ya kuonyesha yaliyo
msingi kimtazamo.
“Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote…
BWANA atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako…
Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza BWANA… BWANA
atakutawanya katika mataifa yote, tokea ncha hii ya dunia hata ncha hii ya dunia…wala katika mataifa hayo
hutapata raha iwayo yote..” Kumb. 28:15,36-37,64-65.
Hapa napo unabii ulikuwa unaeleweka: Waisraeli wangetawanywa katika mataifa, kuishi huko katika mazingira ya
taabu, wakibezwa na kudharauliwa. Ni ajabu iliyoje kuona maisha yao yalivyothibitisha uhakika wa maneno hayo!
Mtawanyo wa Wayahudi dunia nzima ulianza katika enzi za Waashuru katika karne ya 8, K.K. Jambo hili liliendelea
wakati wa Wababeli kwenye karne ya sita. Baada ya sehemu yao kurudi kutoka Babeli siku za Wafalme wa Kiajemi,
jumuia ya Waisraeli iliishi katika ardhi yao kama 500 K.K mpaka siku za Kristo, chini ya tawala za kiajemi,
Kiyunani na waliowafuata, na mwishowe Warumi. Katika mwaka 70 B.K, miaka 40 baada ya Kristo kusulubiwa
msalabani, palitokea patashika mbaya kuliko zote. Jiji la Yerusalemu lilishambuliwa na kuporwa na majeshi ya
Kirumi kwa sababu ya uasi; hekalu likateketezwa kwa moto na Wayahudi kutawanywa mateka dunia yote (ya
Kirumi) – tazama kielelezo kwenye jalada. Wamekuwa huko tangu wakati huo, kama ilivyotokea; ncha moja wa
dunia hata ncha nyingine!
Na wamekosa, kama ilivyoandikwa mpaka hivi karibuni ‘utulivu’, wakipata mateso na mara nyingine maangamizi.
Wapogrom wa Urusi katika karne ya 19 na mpango wa Hitler wa uhilikishaji katika karne ya 20 ni mifano michache
tu ya karibuni. Wayahudi wamekuwa kila mahali wakikabiliwa na chuki na kukataliwa, kiasi kwamba uwepo wao
kama jamii ya watu, ni mojawapo wa maajabu ya kihistoria. Tunaona vile vile ya kwamba Unabii huu juu ya hatima
ya Waisraeli umeendelea kuwa kweli kwa zaidi ya miaka 2500 sasa. Nani angeweza kuliona hilo, tukizingatia
mtawanyo ulivyokuwa na mateso, kwamba Wayahudi wangeendele kwa karne nyingi kuwa jamii kamili ya watu
inayoendelea kutambulika hadi sasa!
Lakini ni zaidi ya hayo…
Lakini jambo la ajabu zaidi juu ya unabii kuhusu Israeli halijasemewa, kwani manabii walitabiri pia wazi wazi
badiliko lisilotegemewa la mafanikio kwa Waisraeli. Fikiria, kwa mfano, utabiri wa nabii Yeremia, uliotolewa
karibu miaka 600 K.K.
“Kwa maana, tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapowarejeza watu wangu wa Israeli na Yuda
waliofungwa… nani nitawarudisha hata nchi niliyowapa baba zao, nao wataimiliki (30:3)
“Basi sasa, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi…Tazama, nitawakusanya, na kuwatoa katika nchi zote
nilikowafukuza, katika hasira yangu… nami nitawaleta tena hata mahali hapa, nami nitawakalisha salama salimini;
nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao…” (32:36-38)
 “Nami nitawarudisha wafungwa wa Yuda, na wafungwa wa Israeli, na kuwajenga kama kwanza. Nami
nitawasafisha na uovu wao wote…” (33:7)

Na hapa pia hakuna utata juu ya lile alilokuwa akisema nabii: Kitendo kile cha kutawanywa na mateso kwa

Waisraeli kitageuzwa. Wayahudi watarudi tena katika nchi ile ile ambayo kutoka kwao walifukuzwa zaidi ya miaka
1990 iliyopita, na kuishi hapo kwa amani zaidi. Madondoo hayo mafupi kutoka kwa Yeremia, yanaweza kuzidishwa
mara nyingi kwa matamko kama hayo kutoka Isaya na Ezekieli.
Hatuhitaji hasa kuzama sana ili kuonyesha jinsi utabiri huo wa kurudishwa upya Israeli ulivyotimizwa kikamilifu.
Ushirika wa kisayuni ulikuwa na nguvu kati ya Wayahudi waliotawanywa katika nchi nyingi mwishoni mwa karne
ya 19. Uanzishwaji wa Palestina kuwa makao ya kitaifa ya Wayahudi mwaka 1917 ulisababisha idadi yao kukua
haraka katika nchi hiyo. Hili lilipozua chuki kali kwa Waarabu, Wayahudi walipambana na jaribio lao la
kuwakandamiza mwaka 1948, na kuanzisha taifa lao la Kiyahudi. Nalo lilipanuliwa mwaka 1967 katika jaribio la
pili kwenye vita vya siku sita, ambapo Israeli ilijichukulia upya sehemu kubwa ya ardhi yake ya kale, na
Yerusalemu kuwa makao makuu ya taifa lao chini ya utawala wao wenyewe, kwa mara ya kwanza katika miaka
2500. Kwa kifupi, kuibuka kwa taifa huru la Wayahudi Mashariki ya Kati imekuwa ni kitu kisichotegemewa kabisa.
Chini ya miaka 100 iliyopita hakuna mchunguzi wa kisiasa aliyedhani inawezekana.
Hatujihusishi hapa na ‘siasa’ za jambo hilo. Tunachoangalia hasa ni unabii wa Biblia. Kuna mengi mengine Biblia
inayosema juu ya Wayahudi. Manabii wanasema, kwa mfano, kwamba kutakuwa na matatizo makubwa Mashariki
ya Kati, na kwamba Israeli itafikishwa kwenye toba mbele ya Mungu wake. Hapo ndipo unabii wa mwisho wa
kurudishwa upya na amani utakapotimia. Hapa tungependa kusisitiza tu kwamba manabii walitabiria kurudi kwa
Waisraeli kwenye ardhi yao wenyewe, na sisi katika karne hii tumeona kwa macho yetu utabiri huu ukianza
kutimizwa.
UNABII AINA TATU – HATIMA TATU
Baada ya kufika hapa, ni kitu cha manufaa kufanya muhtasari wa yale tuliyoona.
Babeli: Ile dola kuu kabisa Mashariki ya Kati, ilikuwa ipoteze mamlaka yake, na jiji lake kuu maridadi sana liwe
mahame, likiepukwa na watu na wanyama pori. Na ndivyo ilivyotokea.
Misri: Nayo dola kuu nyingine, ingelibakia kuwa ufalme unaotambulika. Wamisri wangeendelea kukaa katika nchi
yao wenyewe. Lakini mara zote wangetawaliwa na mamlaka zingine, wakibakia ‘ufalme wa chini.’ Na ndivyo
ilivyokuwa.
Hatima ya Israeli haikuwa ya kufananishwa na yoyote kati ya hizi. Wakiwa wametawanywa mbali na nchi yao
kwenye nchi nyingine, na kupata mateso makali na manyanyaso, wangerudi tena katika nchi ile ile walipotawanywa,
na kujianzisha tena hapo.
Tuzingatie kwa makini yafuatayo:-
1. Unabii kuhusu mataifa haya ulitolewa kama miaka 2500 iliyopita.
2. Ukweli wake umekuwa matukio halisi ya kihistoria mpaka leo.
3. Mifano hiyo hapo juu ilihusu mamlaka tatu tofauti, zenye hatima tatu tofauti kabisa. Moja ilikuwa
kutoweka; ya pili kubakia, lakini kukaliwa na mataifa mengine; ya tatu kuangamizwa, na watu wake
kufukuzwa na kutawanywa dunia nzima, na bado hatimaye kurudishwa katika nchi ya awali.
4. Hii sio ‘mitazamo ya mbeleni ya kisiasa,’ ya wachunguzi wajanja wa kisiasa, bali ni utabiri usiokosea wa
mambo.
Nani angeweza kujua?
Utabiri wa mambo wa muda mrefu hivyo unawezekanaje? Kuna jibu moja tu linaloridhisha; Lazima awepo
aliyeyajua kabla; lakini ni nani? Kwa hakika hakuna mtu wa miaka 2500 iliyopita au tangu hapo, angeweza kujua.
Tukiupima utabiri wa namna hii kibinadamu tu hauelezeki. Lakini hata hivyo, manabii wa Agano la Kale hawakudai
wanatabiri kwa uwezo wao. Walisema walikuwa wakisema maneno yaliyotoka kwa Mungu. “ Hivi ndivyo
asemavyo BWANA,” ndivyo walivyokuwa wakianza kusema wakati wote. Kama Mungu alikuwa nyuma ya yale
waliyosema, tunapata jibu la nani aliyejua.’ Hakuna maelezo mengine yanayoleta maana. Unabii tuliouchunguza
hapa ulihitaji uwepo wa Mungu kama chanzo chake. Inaleta maana.

Mifano hii mtatu tuliyoinukulu ilichaguliwa kuonyesha aina tofauti za unabii wa Biblia. Lakini mifano iko mingi.

Tungeweza, kwa mfano, kuchunguza ule unaomhusu Yesu Kristo: alipaswa kuwa na mzao wa Ibrahim, na wa
Daudi; alikuwa azaliwe Bethlehem; alikuwa akataliwe na watu wake; na bado afe kifo cha upatanisho kwa ajili yao;
na maelezo mengi mengineyo - yote yakiwa yametamkwa mamia ya miaka kabla hajazaliwa, na bado yakawa hivyo
hivyo katika kuzaliwa, kwa Yesu, utumishi, kifo na kufufuka kwake.
Lakini tutahitimisha uchunguzi wetu mfupi kwa mifano miwili zaidi itakayoleta mpango wa kiunabii mpaka kufikia
wakati tulionao.
BIBLIA NA MATAIFA
Unabii wa Daniel unao mpango wa kuvutia unaohusu kukua na kuanguka kwa dola, na hali ya mataifa ya kile
kilichokuwa kikiitwa ‘Dunia iliyostaarabika,’ yaani mataifa ya Ulaya, Mashariki ya Kati, Misri na pwani ya
kaskazini mwa Afrika, yote yanayoizunguka Bahari ya Kati (Mediterranean sea). Unabii huu ulitolewa wakati
Daniel alipokuwa mateka katika boma Babeli karne ya 6 K.K. Ukweli wake umejidhihirisha katika historia tangu
siku hizo hadi sasa.
Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akiwa amejaa kujikinai na ufahari, aliona katika ndoto sanamu moja kubwa sana
ya mtu, yenye sehemu tano (tazama uk. 16,17):
1. Kichwa cha sanamu kilikuwa cha dhahabu.
2. Kifua chake na mikono kilikuwa cha fedha.
3. Tumbo lake na mapaja lilikuwa la shaba.
4. Miguu yake miwili ilikuwa ya Chuma.
5. Lakini nyayo na vidole zilikuwa mchanganyiko wa chuma na udongo wa mfinyanzi.
Kisha jiwe likatokeza ‘lililokatwa kutoka mlimani bila kazi ya mikono.’ Likaangukia nyayo za sanamu ile,
likaiangusha yote chini, na kuzisaga sehemu zake kuwa unga, kiasi kwamba upepo ukaupeperushia mbali. Baada ya
hapa lile jiwe likakua kuwa mlima mkubwa na kuijaza dunia yote.
Nebukadreza alisumbuliwa sana na hatima ya sanamu ile, kwa sababu hakuna kati ya watu wake wajuzi aliyeweza
kumwambia ilikuwa na maana gani. lakini Daniel, nabii wa Israel alimwambia “kuna Mungu mbinguni afunuaye
siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho “Dan. 2:28
Kwa hiyo Daniel alielezea maana ya sanamu ile. Kichwa cha dhahabu kiliwakilisha utawala wa Nebukadreza
mwenyewe. Ulikuwa ufuatiwe na mwingine, wa hali ya chini zaidi (kifua na mikono ya fedha); na baada ya huo wa
tatu (wa shaba); alafu wa nne (miguu ya chuma) ambao ungekuwa na nguvu na kishindo, lakini nyayo na vidole
viliwakilisha falme zilizogawanyika, nusu nguvu na nusu dhaifu”. (Ms. 37 – 42)
Kitu kimoja ni wazi: Sanamu hii iliwakilisha makabidhiano ya falme zenye nguvu, na sio vigumu kuzitambua. Wa
kwanza tunafahamu; ulikuwa ni dola ya Babeli. Katika kifungu cha 8 (Mstari wa 20 – 21) tunaambiwa afuataye
angekuwa Mwajemi na Myunani. Dola ya nne, ‘ kuu na inayotisha’, haikutajwa wazi wazi katika unabii wa Daniel.
Historia inathibitisha tabiri hizi kwa wingi. Kama 530 K.K. mamlaka ya Babeli iliangushwa na Wamedi na
Waajemi, ambao mwishoni walianzisha dola ya kiajemi. Ilidumu miaka 200, na baadaye kuangushwa kama 330
K.K. na Aleksanda Mkuu (Alexander the Great) aliyesimamisha dola ya Kiyunani.
Ni dola gani kubwa iliyofuata falme za mrithi wa Aleksanda? Hakuna mashaka juu ya jibu: ilikuwa dola ya Rumi.
Warumi walivamia maeneo ya iliyokuwa dola ya Kiyunani kuanzia karne ya 2 K.K. na kuendelea. Kwa miaka 500
iliyofuata, Rumi ilikuwa mamlaka kuu kuliko zote duniani. Dola yake ilitanda kama sehemu yote ya dola zile tatu,
na kuenea mbali ndani ya Ulaya, Mashariki ya Kati na nchi zote zinazozunguka Mediterranean. Walifanikisha
uvamizi wao kwa ukatili mwingi kama ilivyodokezwa na maneno “nguvu kama chuma.” Katika karne zake mbili za
mwisho za kuwepo kwake, iligawanyika sehemu mbili: ya magharibi makao yake makuu yakiwa Rumi, na ya
mashariki makao yake makuu yakiwa Constantinople – miguu miwili ya ile sanamu.

Mungu anayefunua siri

Lakini ni nini kilichotokea baada ya dola ya Warumi kuvunjika katika karne ya 5 B. K. Haikufuatiwa na dola
nyingine yoyote kuu, na kwa kweli haijakuwapo dola ya tano ya kulinganishwa kimamlaka, pamoja na kuwepo
jitihada kubwa za watu wenye tamaa kuunda nyingine. Maeneo ya dola ya Kirumi yalimeguka kutokana na uvamizi
wa makabila jeuri ya Kihan, Kigoti, Kivisigoti na Kivandali, yaliyoanzisha tawala zao wenyewe tofauti. Mataifa ya
sasa ya Ulaya yametokana na falme hizo. Katika kipindi chote cha historia ya miaka 1500 mpaka sasa, mataifa hayo
yamebakia katika mgawanyiko, kama ilivyoashiriwa na nyayo za ile sanamu – nusu chuma na nusu udongo: “ nusu
una nguvu, na nusu yake umevunjika … hawatashikamana. “(Dan. 2:42-43)
Angewezaje Daniel kujua kuwa mamlaka ile kuu ya Nebukadreza ingefuatiwa na zingine tatu, ya nne ikiwa na
nguvu zisizo za kawaida, ambayo kamwe isingelifuatiwa na ya tano? Angejuaje kuwa baada ya ile ya nne kuanguka,
watu wake wangesambaratika kuwa nchi zilizomeguka, zisizo na umoja kati yake? Kwa vyovyote, kwa yeye
mwenyewe asingeweza kujua kitu, wala yeyote mwingine. Lakini Daniel hatuachi bila maelezo:
“Yupo Mungu mbinguni afunuaye siri.. Mungu aliye mkuu amemjulisha mfalme mambo yatakayokuwa baadaye, na
ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti.” (Ms. 28,45)
Unawezaje kuuelezea uwepo wa unabii wa Daniel 2, karne kadhaa K.K, na bado kuwa na mtizamo sahihi wa
madola na mataifa mpaka hivi leo, baada ya zaidi ya miaka 2000? Kama kweli kuna ‘Mungu mbinguni,’ unaweza
kuelewa. Kama Hayupo, hakuna maelezo yanayoridhisha.
Tutatoa maoni katika sehemu ya hitimisho, juu ya jiwe linaloigonga ile sanamu miguuni na kuiangusha yote chini.
Kwa ajili ya mfano wetu wa mwisho wa kinabii tuone kwanza.
NYAKATI TULIZO NAZO
Ingawa unabii tuliouzingatia mpaka sasa umeendelea kutimia hadi hivi leo, ulihusu zaidi matukio ya siku nyingi za
nyuma (ukiacha urudishwaji upya wa Waisraeli hivi karibuni katika ardhi yao ya kale). Je, kuna kinachosemwa na
unabii wa Biblia juu ya nyakati tulizo nazo kuweza kutuongoza katika siku hizi?
Kipo hasa! Tena ni ajabu kinavyotofautiana sana na matazamio na fikra za kibinadamu. Karne ya 19 ilikuwa kipindi
cha matumaini. Maendeleo makubwa yalikuwa yakipigwa. Ujuzi wa Kisayansi ulivyoongezeka ulileta maendeleo
haraka kiufundi na uzalishaji mkubwa viwandani. Hili lilikuwa lilete neema (ingawa sio kwa walio maskini sana).
Elimu ilipanuliwa kuwafikia wengi, na matumaini ya maana yalipatikana. Watu walioelimika zaidi, ilidaiwa,
wangejishughulisha na sanaa kama fasihi, muziki na uchoraji. Maadili ya jamii kwa ujumla yengeboreka. Wanasiasa
waliahidi kuleta mpango mpya wa kijamii wa haki na usawa kwa wote. Vile ambavyo watu wangetajirika, ndivyo
ambavyo wasingeoneana kijicho. “Tokomeza umaskini, na ndivyo utakavyotokomeza uovu, lilikuwa ndilo bango.
Wakati uwezo wa juu wa akili ya mwanadamu ukitumiwa, ilikuwa amani ijengeke kati ya mataifa. Viongozi wa
kanisa nao wakatazamia kwa dhati kueneza Injili dunia nzima. Kujiendeleza mwanadamu na kuboresha maisha, kwa
mtu binafsi na kwa jamii, vilichukuliwa juu juu tu. Hali ya baadaye ikaonekana nzuri.
Amani na maendeleo?
Kinyume cha matazamio hayo, matukio ya karne ya 20 yamekuwa mfadhaiko. Ndoto za maendeleo na amani
zimefifia. Vita viwili vibaya sana vya dunia, vikiwa vimechinja mamilioni na kuleta uharibifu usiosemekana wa
mali na mateso, vimefuatiwa na uundaji wa silaha kali za maangamizi ambazo hazijawahi kutengenezwa. Mawazo
ya utatuzi ya aina mbalimbali ya ‘wenye busara’ wa karne ya 19 yamekuwa bure. Kupanuliwa elimu hakujafuatiwa
na maadili zaidi, badala yake na kukua kwa dhuluma, choyo, vurugu na uvunjaji sheria. Dini ya Kikristo, mbali na
kuwabadili mataifa, imekuwa katika kurudi nyuma duniani pote.
Demokrasia katika siasa haijajidhihirisha kuwa muarobaini wa maovu katika jamii kama ilivyotarajiwa. Mwishowe
pigo baya zaidi – sayansi imethibitika kuwa silaha ya kutisha ya makali kuwili. Mbali na kuwa enzi ya amani, karne
ya 20, ya ustaarabu, imekuwa wakati wa migogoro na mapambano. Ndio maana mtizamo wa wengi umekuwa ule
wa kukata tamaa. Inaonekana kama hakuna anayeweza kufanya kitu.
Sasa unabii wa Biblia unasemeaje hali hizi?

Biblia ina utabiri wa kueleweka kabisa juu ya siku za mwisho, ‘nyakati za mwisho,’ wakati harakati za mwanadamu

katika nchi zitakapofikia hatua mbaya. Sio picha ya maendeleo endelevu na amani, bali ya matatizo duniani na hofu.
Mfano wa wazi sana na unaotugusa upo katika yale Yesu aliyowaambia wanafunzi wake walipomuuliza nini
ingekuwa ishara ya kurudi kwake duniani na ya ‘mwisho wa dunia.’ Anawaambia kwanza juu ya hatima ya
Wayahudi.
“Wataanguka (Wayahudi) kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na
Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa (wasio Wayahudi), hata majira ya Mataifa yatakapotimia.” (Luka 21:24)
Sasa haya ni maelezo mafupi juu ya yale tuliyoyaangalia yahusuyo unabii kwa Israeli. Wayahudi wangeng’olewa
kuwa mateka kati ya mataifa yote; Yerusalemu ingekaliwa na mamlaka za kimataifa. Gundua kwamba Yesu
anasemea mwisho wa hili ‘hata majira ya Mataifa yatakapotimia.’ Tumeona mwanzo wa jambo hili katika wakati
wetu. Yerusalemu haikaliwi tena na watu wa nje – unakaliwa na Israeli yenyewe.
Mashaka na hofu duniani
Kwa hiyo yale anayoendelea kusema lazima yahusiane na siku hizo – siku za Israeli kurudishwa katika nchi yao
wenyewe. Hivi ndivyo anavyotabiri.
“Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya Mataifa wakishangaa kwa uvumi
wa bahari na msukosuko wake; watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata
ulimwengu; kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika.” (Ms. 25 – 26)
Hii sio picha ya amani na maendeleo. Ni dunia ya hekaheka na kuchanganyikiwa, hofu ikiikumba mioyo ya watu
wanapofikiria mambo yanayotokea katika ‘makao ya watu duniani’ kama neno alilotumia Yesu linavyomaanisha.
Mtume Paulo, akiwa anaandika kama miaka 35 baada ya unabii huo wa Yesu, anasema hivi juu ya hali ya siku za
mwisho.
“…siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, na wenye
kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,
wasiopenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti,
wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana
nguvu zake;..”
Hii ni sura ya ajabu ya ustaarabu; mtu anatupilia mbali vizuizi vyote na kuzifuata tamaa zake mwenyewe bila kujali
matokeo yake. Hakuna asiyeona uwiano wa hali hiyo na mambo yalivyo katika dunia yetu ya sasa.
Kwa hiyo hali ni hiyo; wakati wajuzi wa mambo miaka 100 tu iliyopita walitazamia kwa dhati sana, kipindi cha
maendeleo na amani kwa mataifa ya dunia, Biblia, katika maneno ya Yesu na Paulo ilitabiria dunia ya fujo, hofu na
kuchanganyikiwa, nyakati za migogoro, kujifanyia mtu atakacho, na chuki. Wanafalsafa wetu wa kibinadamu
walikosea; Yesu na Paulo walikuwa sawa! Lakini waliongea na kuandika zaidi ya miaka 1900 iliyopita. Waliwezaje
kujua? Sababu pekee ni kwamba hawakusema maneno yao wenyewe, bali maneno ya Mungu Mwenyewe. Ni
Mungu aliyejua, akampa uwezo Mwanawe na mtume wake kutufunulia hali ya siku za mwisho.
HITIMISHO
Kuna majumuisho kadhaa muhimu tunayoweza kuyafikia kutokana na kuchunguza kwetu unabii wa Biblia.
Kama Biblia imejithibitisha kuwa sahihi kiasi hiki katika utabiri wake wa matukio katika historia ya mwanadamu –
hatima ya Babeli, Misri na Israeli, na pia katika kukua na kuanguka dola, na hali ya dunia kwa wakati huu – itakosa
kuwa sawa katika utabiri wake wa matukio yaliyobaki?
Chukulia yale maono katika sanamu katika Daniel, kwa mfano. Hatujatolea maoni bado juu ya ile hatua ya mwisho:
Jiwe, “ lililokatwa kutoka mlimani bila kazi ya mikono,” liliipiga ile sanamu chini ya miguu, likaivunjavunja, na
lenyewe “likawa mlima mkubwa, na kuijaza dunia yote “(Dan. 2:35). Sasa maana ya jumla ya hili iko wazi: kitu
kigeni, kisichokuwa sehemu ya dola za sanamu na falme, kinaziharibu na kuchukua nafasi zake duniani. Kwa kuwa
‘bila mikono,’ maana yake ni ‘bila mikono ya mwanadamu’, lile jiwe lazima litakuwa linasimama badala ya nguvu
isiyokuwa ya kawaida ya kibinadamu.


Lakini Daniel anatuambia mwenyewe maana yake:

“Katika siku za wafalme hao, Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele…
utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele. “ (Ms. 44)
Serikali za sasa na mamlaka za dunia zitaondolewa, katika tukio moja la aina yake, Mungu atakapoingilia kati na
kusimamisha Serikali yake Mwenyewe. Kuondoa utata ieleweke kwamba, sio umati wa watu unaoangamizwa: ni
nguvu na mamlaka za falme za kibinadamu, zitakazong’olewa na ufalme mpya wa Mungu. Unabii mwingi
mwingine unatueleza jinsi ufalme huo utakavyokuwa; maongozi yake timamu, mafundisho yake yenye kweli, na
amani utakayoleta hatimaye duniani kwa watu wote kutokana na kumtambua kwao ‘Mungu wa mbinguni!’ Soma
kwa mfano Isaya 2:1-4 kupata picha kamili na ya kusisimua juu ya mataifa katika enzi hiyo ijayo.
Lakini ni kwa namna gani mageuzi hayo makubwa yanaweza kufanikishwa duniani? Agano jipya linatupa jibu. Na
hasa ni Yesu mwenyewe anayetuambia katika unabii ule wa nyakati za taabu na hofu kwa mataifa yote. Maneno
yake yaliyofuata ni haya
“Hapo ndipo watakapomwona mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi” (Luka
21:27)
Anasema atarudi tena mwenyewe. Kurudi kwa Kristo duniani ni wazo mojawapo kuu katika mafundisho ya Yesu na
mitume katika Agano Jipya na linakubaliana kabisa na manabii. Soma zaburi 72 kupata kinachosemwa juu ya
utawala wake.
Sasa, kwa hakika, hili ndilo linalopaswa kutushughulisha sana: Kama unabii wa Biblia kuhusu mataifa na dola
umekuwa kweli kama ilivyo kwa zaidi ya miaka 2000, hayo mengine yaliyotabiriwa yatakosa kutimia? Sio kukosa
busara kusema: “sawa nakubali manabii walikuwa sahihi katika utabiri wao katika mambo haya ya kihistoria, lakini
siamini wanayosema juu ya yajayo kutuhusu sisi.” Kwa nini? Wametoa uthibitisho kwamba hawakuwa wakitoa
mawazo yao wenyewe, bali makusudio hasa ya Mungu. Yote yale wanayosema yanapaswa kutufanya tujali sana.
Kitu cha muhimu
Lakini bila shaka kuna zaidi. Unabii huu wa ajabu unapatikana katika Biblia, na sio mahali pengine popote duniani.
Hakuna maandiko mengine, hakuna vitabu, hakuna matamko mengine yoyote ya mwanadamu yanayoweza hata kwa
mbali kulinganishwa na Biblia. Lakini Biblia inatuambia kwamba Yesu alikuwa mwana wa Mungu; mambo
aliyosema yamehifadhiwa kwa ajili yetu katika Injili za Agano Jipya. Pamoja na mafundisho ya mitume wake Petro,
Yohana na Paulo, wanatufunulia ukweli ambao hatuwezi vinginevyo kuujua. Wanatuonya juu ya ukweli kuhusu
kifo; wanaeleza kwa nini Injili ni ‘habari njema,’ ‘uweza wa Mungu uuletao wokovu’ (Warumi 1:16). Wanatutia
moyo na ahadi ya uzima wa milele katika mpango mpya atakaouanzisha Kristo atakapokuja. Ndio maana inatupasa
kuisoma Bilia. Inaweza kutupa utofauti wa muhimu kati ya utupu wa kifo, na tumaini la nguvu la maisha yasiyo na
mwisho.
Usomaji wa makini wa Biblia utatuhakikishia kuwa Mungu yupo, anatawala, na kwamba anatuita tuwe wafuasi wa
mwanawe. Biblia ipo kwa ajili yetu. Tunafanya vizuri kujali inachosema.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

HUDUMA ZA MAZISHI

Huduma ya Mazishi  (Mchungaji, mzee wa kanisa, au shemasi anaweza kufanya huduma hii). Ushauri umetolewa kwamba, kadiri inavyowezekana, maz...